Friday, 3 October 2014

MAHESABU YA MBARALI::HALMASHAURI YA WILAYA YA MBARALI YAPITISHA HESABU ZA MWAKA 2013/2014.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kenneth Ndingo, akifungua mkutano wa baraza la madiwani.

 Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Dk. Boniface Kasululu akitoa taarifa katika mkutano wa baraza la madiwani.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali wakifuatilia kwa makini kikao kikiendelea.

Baadhi wa madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.

Wakuu wa idara mbali mbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali wakifuatilia mkutano wa Baraza la Madiwani.

Baraza la madiwani likiendelea na mkutano wa kupitia na kupisha Hesabu za mwisho wa mwaka.

KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Dk. Boniface Kasululu, ambaye pia ni Mganga mkuu wa Halmashauri hiyo, amewasilisha hesabu za mwaka 2013/2014 katika Baraza la Madiwani.
Alisema mali za Halmashauri kwa mwaka huo ziliingia uchakavu wa zaidi ya Bilioni 1.1 ukilinganisha na uchakavu wa mwaka 2012/2013 uliokuwa shilingi Bilioni 1.
Alisema Mali za kudumu kwa mwaka wa fedha 2013/2014 ziliongezeka kwa kiasi cha Shilingi Bilioni 4.4 kutoka Bilioni 17 hadi kufikia Bilioni 21.4, Ruzuku toka serikali  kuu kwa mwaka 2013/2014 zilipokelewa shilingi Bilioni 20 zikilinganishwa na Bilioni 19.8 kwa mwaka 2012/2013.
Aliongeza kuwa mapato kutokavyanzo vya Halmashauri kwa mwaka 2013/2014 vilikuwa ni shilingi Bilioni 1.5 zikilinganishwa na Shilingi Bilioni 1 zilizokusanywa  mwaka 2012/2013, na kwamba makusanyo hayo yamejumuisha ada za wanafunzi wa shule za Sekondari na Mfuko wa jamii(CHF).
Alisema hadi tarehe ya mwisho ya kufunga hesabu za mwaka wa fedha wa 2013/2014 zilizofanyika Juni 30, mwaka huu, Halmashauri ilikuwa na fedha taslimu benki kiasi cha shilingi Bilioni 1.2.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Kenneth Ndingo, ametoa wito kwa Madiwani  kuwahamasisha Wananchi kuendelea kuchangia katika shughuli za maendeleo ili Halmashauri ipunguze utegemezi kutoka serikali kuu.
Ndingo alisema Halmashauri imejipanga kujitegemea katika kujiendesha kwa kupunguza utegemezi kutoka serikali kuu kwa kuboresha miundombinu ya ukusanyaji wa mapato na kuwahamasisha wananchi kuchangia shughuli za maendeleo zinazofanywa na Halmashauri yao.
Alisema taarifa ya hesabu za Mwisho za Halmashauri inajumuisha mambo muhimu kama vile Mali za Halmashauri zikiwemo fedha taslimu na mali za kudumu, mikakati ya muda mrefu na muda mfupi ya Halmashauri pamoja na Matarajio ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha unaofuata.
Mwenyekiti huo alisema utaratibu wa kujadili na kupitia taarifa za mwisho za fedha ni kutokana na kanuni ambazo zimeainishwa katika muongozo wa taratibu za fedha za serikali za mitaa ya mwaka 2009, kifungu cha 31 (1).
“ Halmashauri kama taasisi zingine za serikali inapaswa kuhakikisha kuwa hesabu za mwisho zinaandaliwa kwa umakini na kwa wakati kwa ajili ya kuwasilishwa katika vikao mbali mbali vya kisheria na kuwasilishwa kwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ndani ya miezi mitatu ya mwaka wa fedha kuisha” alifafanua Mwenyekiti.
Mwisho.
Na Mbeya yetu

No comments:

Post a Comment