WAKATI
 ikiwa imezoeleka kuwa baadhi ya walimu wa kiume huwarubuni wanafunzi 
wao wa kike na hata kuwaharibia kabisa ndoto zao za kielimu kutokana na 
kuwapa ujauzito, hali imekuwa tofauti mkoani Rukwa ambako mwanafunzi wa 
Kidato cha Pili anadaiwa kumzalisha mwalimu wake.
  
Mwanafunzi
 huyo aliyemzalisha mwalimu wake ana umri wa miaka 17, wakati mwalimu 
huyo anayefundisha katika Shule ya Sekondari ya Umma ya Nkasi, iliyopo 
mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi, Rukwa, ana umri wa miaka 25.
Tukio hilo linalotajwa kuwa la kwanza kutokea wilayani hapa, limekuwa gumzo kubwa kwa wakazi wa Nkasi na wilaya jirani.
Hata
 hivyo, kwa wanafunzi, wamekuwa wakimpongeza mwenzao kwa kujaliwa kupata
 mtoto katika umri wake huo mdogo, huku mzazi mwenzake akiwa na uhakika 
wa maisha kutokana na kuwa ni mtumishi serikalini.
Imeelezwa
 kuwa licha ya tukio hilo, mwalimu huyo aliyezaa na mwanafunzi wake bado
 anaendelea na masomo shuleni hapo, huku `mzazi’ huyo wa kiume 
akifundishwa na mzazi mwenzake.
Akizungumza
 na mwandishi wa habari hizi mjini Namanyere hivi karibuni, Mkuu wa 
Shule ya Sekondari Nkasi mjini Namanyere ambayo ni ya mchanganyiko ya 
umma, Amiamie Nanga alisema mwalimu huyo alianza kazi shuleni hapo ikiwa
 ni mara yake ya kwanza kufundisha baada ya kuhitimu mafunzo ya ualimu 
chuoni.
“Yameshatokea,
 lakini haileti picha nzuri sana, lakini mimi nina uzoefu mkubwa na 
wakazi wa mwambao wa Ziwa Tanganyika, kwao si ajabu kuwa na uhusiano na 
watu waliowazidi umri, iwe kwa mtoto wa kike au wa kiume, wote ni sawa 
tu…
“Lakini
 katika kisa hiki, inaonesha walimu sasa wanapoteza haiba ya ualimu. Hii
 kazi ina miiko na maadili yake …kwa mwalimu huyu hii ni ajira yake ya 
kwanza, nikimaanisha ni kituo chake cha kwanza cha kazi tangu ahitimu 
masomo yake…” alisema.
 Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob 
Mwaruanda alisema hakuna kosa kwa mwalimu huyo wa kike kwa kuwa tayari 
ni mtu mzima.
“Isitoshe
 katika kisa hiki ni nadra kumpata mlalamikaji … Mwalimu mwenyewe huyu 
wa kike hawezi kuwa tayari kujidhalilisha kuwa amebakwa, yalikuwa 
maamuzi yake.”
Aliongeza
 kuwa, kwa mwalimu huyo kupata ujauzito wa mwanafunzi wake hakuwezi 
kuathiri ajira yake, tofauti na mwalimu wa kiume akimpatia ujauzito 
mwanafunzi wake wa kike ambaye huathirika kwa kukatisha masomo.
Jitihada
 za kumpata mwalimu huyo wa kike na mwanafunzi huyo zimegonga mwamba 
baada ya watu wao wa karibu kumweleza  mwandishi  kuwa hawako tayari 
kuuzungumzia mkasa huo.
Baadhi
 ya wanafunzi wa shule hiyo waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi kwa 
masharti ya kutoandikwa majina yao  kwa hofu ya kuchukuliwa hatua za 
kinidhamu shuleni hapo, pamoja na kukiri kutambua uhusiano baina ya 
mwanafunzi mwenzao na mwalimu wao, lakini walisema hivi sasa mwalimu 
huyo amesitisha uhusiano na mwenzao na kuanzisha uhusiano mpya na 
mwalimu mwenzao.
Walisema
 pamoja na mambo mengine ni kama mwanafunzi mwenzao ameathirika 
kisaikolojia baada ya ‘kupinduliwa’ na mwalimu wake wa kiume ambaye kwa 
sasa ndiye baba mlezi wa mtoto.
“Huyu
 mwalimu wa kike sisi sasa tunamwita shemeji yetu alikuwa na uhusiano wa
 kimapenzi na mwenzetu… penzi lao lilikolea hadi sasa ameweza kumzalia 
mtoto huyo…, lakini kwa sasa inavyoelezwa ni kwamba penzi limehamia kwa 
mwalimu mwenzake,“ alisema mmoja wao.
Baadhi
 ya watu wa karibu na mwanafunzi huyo wanakiri kuwa mwanafunzi huyo hana
 uwezo wa kifedha kumudu kumpatia malezi stahiki mtoto wake huyo, hivyo 
hata mzazi mwenzake alipoanza uhusiano na mwalimu mwenzake hakuwa na 
jinsi, bali kukubaliana na matokeo.
“Usiniandike
 jina, sisi tunashauri mwalimu huyo wa kike na mpenzi wake huyo wa kiume
 ambaye ni mwalimu mwenzake wahamishiwe shule nyingine kwa sababu kama 
kioo katika jamii wameteleza kwa kiasi kikubwa na watashindwa kuwajenga 
na kuwalea wanafunzi wao kimaadili.
“Isitoshe
 tunajiuliza sheria hapa inasemaje maana kama angekuwa ni mwalimu wa 
kiume amempatia mwanafunzi wake wa kike ujauzito angeshitakiwa na 
kufikishwa mahakamani na pengine kuhukumiwa kifungo kisichopungua miaka 
30 jela, sasa kwa hili sheria inasemaje?”Alihoji.
Baadhi
 ya wazazi mkoani hapo waliohojiwa na mwandishi kwa nyakati tofauti 
wameelezea kushangazwa na tukio hilo, na hasa kwa jinsi mwalimu 
alivyoshindwa kujizuia `kujiachia’ kimapenzi kwa mwanafunzi wake.
No comments:
Post a Comment