WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema amevutiwa na kasi ya 
mabadiliko katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na hasa 
uanzishwaji wa kozi mpya zinazolenga uongezaji thamani wa mazao ya 
kilimo (Agri-processing).
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Oktoba 9, 2014) 
wakati akizungumza na wahadhiri, wakufunzi, wanafunzi na wanajumuiya ya 
SUA mara baada ya kutembelea chuo hicho na kukagua utekelezaji wa mradi 
wa Sayansi na Teknolojia ya Elimu ya Juu (Science and Technology Higher 
Education Project - STHEP).
“Nimefurahia sana hili suala la Agri-processing kwa sababu 
hivi tuna mzigo mkubwa unaoisumbua Serikali nao ni namna ya kununua 
mazao ya wakulima. Tuna ziada ya tani milioni 1.5 za mahindi na tani 
laki nane za mpunga wakati uwezo wa NFRA ni kununua tani 240,000 tu. 
Haya ni matokeo ya wahitimu waliotoka SUA na kupelekwa wilayani na 
vijijini wakahimiza kilimo bora kwa wananchi,” alifafanua.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili Morogoro jana mchana akitokea 
Dodoma, alifanya ziara ya siku kwa kutembelea Chuo Kikuu hicho pamoja na
 kiwanda cha kutengeneza nguo cha 21stCentury.
Akiwa chuoni hapo, Waziri Mkuu alikagua majengo matatu 
yaliyojengwa chini ya mradi wa STHEP na kuzindua mawili kati ya hayo, 
alitembelea maabara za upimaji ubora wa vyakula na kisha kuzungumza na 
wanaSUA.
Akizungumza na wanajumuiya hao, Waziri Mkuu aliwataka wawe 
ni viongozi wa mfano kwa kumiliki walau ekari moja ya shamba, walime au 
kuweka mifugo ili yale wanayofundisha darasani yaonekane kwa vitendo 
katika mashamba hayo.
“Tatizo la sasa hivi miongoni mwa wasomi wengi ni kudhani 
kwamba kazi ya kilimo ni ya watu wa hali ya chini lakini wakifika mezani
 wao ndiyo wa kwanza kudai ubwabwa na kuku. Sisi wenye upeo ndiyo 
tunapaswa tuonyeshe njia na mashamba au mifugo yetu yawe ni ya mfano kwa
 wengine,” alisema.
Mapema,akiwasilisha taarifa ya mradi wa STHEP, 
Profesa Gerald Monella alisema mradi huo wenye thamani ya dola za 
Marekani milioni 7.48 (sawa na sh. milioni 12.5/-) umekisaidia chuo 
hicho kupata majengo manne yenye kati ya ghorofa moja na mbili, ambayo 
yameongeza nafasi za kufundishia wanafunzi, vyumba vya maabara na vifaa 
vyake, kuanzisha mitaala miwili pamoja na kusomesha walimu 21.
Kwa kutumia majengo hayo, Chuo kinaweza kufundisha 
wanafunzi 807 kwa wakati mmoja ambayo ni sawa na wanafunzi 10,565 kwa 
wiki moja. Chuo hicho pia kimeweza kupata vifaa vya maabara vyenye 
thamani ya dola za marekani milioni 1.71 ambavyo vimenunuliwa na 
kufungwa kwenye maabara hizo.
“Kwa upande wa elimu ya juu, mradi umeweza kusomesha walimu
 21, miongoni mwao 11 wakiwa ni wa shahada ya uzamivu (PhD) na 10 ni wa 
shahada za uzamili (Masters’).
Aliiomba Serikali iongeze muda wa kustaafu kwa wahadhiri wa
 vyuo vikuu kwani wanapozeeka ndiyo wanapata muda wa kufanya tafiti 
zaidi. “Fani nyingie watumishi wanastaafu wakiwa na miaka 60 au zaidi, 
nasi tunaomba tuongezewe muda badala ya kutumia mfumo wa sasa wa 
kuongezewa miaka miwili miwili halafu mmoja,” alisema.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Mama Kate 
Kamba wakati akitoa salamu za shukrani kwa Waziri Mkuu, alisema Serikali
 iangalie uwezekano wa kuongeza bajeti ya Chuo kwani kinahitaji fedha 
zaidi kwa ajili ya kufanya tafiti na kuboresha miundombinu.
“Tunahitaji fedha za kufanya tafiti zaidi, fedha za 
kuboresha miundombinu ya kufundishia ili tuweze kwenda sambamba na azma 
ya Serikali ya kuimarisha viwanda vya usindikaji mazao ya kilimo, uvuvi 
na mifugo,” alisema.
No comments:
Post a Comment