Saturday 27 September 2014

MAAJABU::Yajue maisha ya Drogba wa pori la Selous yanavyompatia kipato


KATIKA kipindi cha miaka minne iliyopita hadi kufikia leo, watalii wanaoenda kutembelea Pori la Akiba la Selous lililopo katika Kijiji cha Mloka kilichopo Kata ya Mwaseni wilayani Rufiji mkoani Pwani, wanapata fursa ya kufurahia utalii wa aina yake pindi wanapokutana na mmoja wa wanakijiji wa eneo hilo anayejulikana kwa jina la Mwananyika lakini kwa sasa amepewa jina la Drogba kutokana na umaarufu aliojipatia miaka ya hivi karibuni. Inaelezwa kuwa amefanana na Drogba yule mwanasoka anayechezea timu ya Chelsea kwa sasa.

Imeelezwa kuwa, Kijiji hiki ni kijiji cha mwisho kabisa kabla ya kufika kwenye geti la Mtemere, moja ya mageti ya kuingilia kwenye pori hili. Watalii kutoka ndani na nje ya nchi (hususani raia wa kigeni) wanapofika katika kijiji hiki hukutana na Drogba ambaye inaelezwa kuwa amepata umaarufu mkubwa kuanzia mwaka 2011 hadi sasa.
Drogba 2
Wenyeji wa kijiji hiki wanasema Drogba ni mmoja wa wajasiriamali aliyewekeza nguvu na uelewa wake wa mambo ya wanyama pori na mazingira yao kwa kutoe elimu kwa wageni wanaungana naye katika kuelewa tabia za wanyama. Yeye haingii kwenye hifadhi bali anazunguka nje ya pori hili kutokana na maeneo mengi kupitika kirahisi na wanyama kupata nafasi ya kuzunguka katika moja ya vijiji vilivyopo kijijini humo na maeneo ya jirani.
Yeye safari zake hujulikana kama bush walk na wageni wake hupata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu maisha ya mwanakijiji na wanyamapori. Vitu kama dawa mbalimbali za asili, hadithi za kale huwa ni sehemu ya vitu wanavyojifunza wageni wa ‘Drogba’.
Shughuli za Mwananyika au Drogba
Watumiaji wa njia inayoelekea katika geti hilo wanaeleza kuwa moja ya shughuli anazofanya Drogba ni kuelekeza wageni kwenye matembezi wanaoingia kwenye pori hilo na kujipatia kipato cha kuendeshea maisha yake pamoja na familia yake (anatumia lugha tatu hadi sasa, Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa).
Mwenyewe hujigamba kwa kuziita true Africa walking safari na anapokuwa kazini huwa anavaa mavazi ya asili kabisa (baadae huvaa mavazi ya kawaida) ambayo huyatengeneza kwa magome ya miti huku akiwa amebeba ngao, mkuki na kikapu chake cha kubebea mitishamba na vitu vingine anavyoweza kuvipata akiwa katika eneo lake la kazi pia anazunguka kwenye barabara zilizopo kando kando na pori hilo na wakati mwingine hulazimika kuingia kwenye baadhi ya mapori na kuzunguka na wageni wake nje ya hifadhi japo wapo wanyama (wakali na wapole) wapo katika maeneo anayotembelea.
Kwa ajili ya tahadhari na usalama anapofanya safari za miguu na wageni wake siku zote huwa anaambatana na Askari wa hoteli (campsite) waliofikia wageni wake, askari anakuwa na bunduki kwa ajili ya tahadhari kwa chochote kinachoweza kutokea.
Mara zote mgeni anayefanya utalii katika pori hili, husindikizwa na askari wa Maliasili na wakati huo Drogba yeye anaendelea kuzunguka nje ya hifadhi bila kuwa na woga.
Safari zake huwa na vituo vingi ndani yake na kwenye kila kituo kuna jambo ambalo huona ni vyema wageni wake wanastahili kulifahamu na pia endapo mnaweza kukutana na wanyama anatumia nafasi hiyo kuwafundisha wageni mazingira ya wanyama.
Miongoni mwa mambo wageni wanayofaidi wanapokuwa na Drogba ni kufundishwa namna ya kutambua nyayo za wanyama mbalimbali ambazo huwa wanakutana nazo wakiwa safarini.
Drogba
Historia yake kwa ufupi
Hadi sasa ukifika kijiji hicho kama mtalii ukasikia watu wanamzungumzia Drogba basi kuna uwezekano mkubwa wakawa wanamzungumzia Drogba wanayemjua wao anayetembeza wageni wanaotoka ndani nan je ya nchi. na sio yule ambaye watu mbalimbali wamemzoea kumsikia (anayechezea timu ya Chelsea).
Drogba Selous
Kwa hivi sasa watu wengi wanaeleza kuwa hata jina lake kamili hawalijui kutokana na umaarufu aliojipatia (ni mmoja kati ya watu maarufu sana kijiji hapo) na hususani kwa wadau wa utalii ambao hupeleka wageni kwenye pori hilo kupitia lango la Mtemere linalopakana na kijiji cha Mloka ambapo wanyama hutoka nje na kuzunguka vijijini na maeneo ya karibu.
Hali hii inawafanya wageni kufanya kutembelea maeneo ya nje ya pori ambazo huwaleta karibu na wanyama wa porini, baadhi ya wanyama wanaopatikana nje ya pori hilo ni Swala, Nyati,Tembo, Twiga na Viboko, na wanyama wengineo ambao huonekana katika maeneo ambayo Drogba hupendelea kuzunguka akiwa na wageni wake.
Ni nadra sana kuweza kumsogelea Twiga mpaka muwe na usawa wa karibu mara nyingi Drogba yeye anamkaribia bila Twiga kutimua mbio. Inaelezwa kuwa mara chache Twiga huvumilia kwa muda kidogo na baadae kuanza kulala akiwa na Drogba.
Unapoanza kukiacha kijiji cha Mloka na kisha kuelekea lilipo geti la kuingilia Selous (Mtemere) utaanza kukutana na vibao vikikuonyesha zilizopo kambi kadhaa. Kambi nyingi za Mloka zimejengwa pembezoni mwa mto Rufiji ukiwa unaelekea Mtemere nyingi zipo upande wa Kushoto wa barabara.

No comments:

Post a Comment