Monday 29 September 2014

UNANG’ANG’ANIA KUPENDA USIPOPENDEKA ILI IWEJE?

Bila shaka wasomaji wa safu hii mko vizuri na mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku. Kwa upande wangu mimi ni mzima wa afya.Ni siku nyingine Mungu ametujalia uzima tunakutana kupeana mawili matatu yahusuyo maisha ya uhusiano.
Mapenzi yana nafasi kubwa katika maisha ya wanadamu, mapenzi ni hisia kali zilizoko ndani ya miili yetu ndiyo maana inatokea mtu anampenda mtu kiasi cha kutaka hata dunia nzima ijue kama amependa.
Uzuri wa mapenzi ni kupendana, kila mmoja ampende mwenzake. Ikitokea mmoja amempenda mwenzake halafu huyo anayependwa haoneshi ushirikiano hapo ndipo kunapokuwa na tatizo.
Anayependa anafanya jitihada za nguvu kuhakikisha somo lake linaeleweka lakini wapi, jibu linakuwa ni ‘no’. Jibu linakuwa hilo kwa sababu unayempenda yeye hakupendi.
Nimekuwa nikipata maswali mengi katika safu ya ushauri, wengi wanang’ang’ania kupenda mahali ambapo kimsingi hapapendeki. Yule anayependwa, moyo wake unakuwa hautaki tu kuridhia. Upendo haupo kwake, kuna aina ya mtu ambaye yeye anampenda na si wewe.
Kwa kuwa mapenzi ni hisia, mtu anakuwa mgumu kukubaliana na matokeo. Anang’ang’aniza penzi kwa nguvu zote. Anakuwa tayari kuligharamia penzi hilo kwa namna yoyote. Akili inamtuma kwamba ipo siku atamuelewa na moyo wake upate pumziko.
Akili yake hapo haiwazi kabisa kwamba kuna mtu unaweza ukampenda na yeye asikupende. Anasahau kabisa ule msemo wa ndege mzuri  hutua katika mti aupendao. Hawazi kwamba sifa alizoziona kwa huyo anayempenda naye ana sifa zake kwa mtu anayempenda.
Kabla hatujaendelea, ngoja nikupe mfano hai. Kuna mtu tumpe jina la A (jina lake halisi lipo). A yeye ameteseka kwa muda mrefu kumpenda mtu ambaye hampendi, amefanya jitihada nyingi kuhakikisha anampata binti mmoja lakini wapi. Majibu anayopewa ni zaidi ya kuudhi lakini eti akawa hakati tamaa.
Anasema amemweleza binti huyo kwamba anampenda, amewatuma marafiki zake, ametuma zawadi mbalimbali kama maua, vocha na nyinginezo lakini vyote hivyo vilikuwa ni kazi bure.
Mtoto wa kike haoni wala hasikii, hataki tu! Alionyesha msimamo wa hali ya juu. Hakutaka kugeuka nyuma. Sasa je, kupitia mfano huo tunajifunza nini?
Binti alifanya vile kwa sababu moyo wake haupo pale. Kama ingekuwa ni tamaa basi pengine angekubali mapema kutokana na mbinu mbalimbali ambazo A alizitumia. Ndugu zangu, penzi halilazimishwi maana ukilazimisha athari zake ni kubwa huko mbele ya safari.
Mbaya zaidi, uking’ang’ania sana, anaweza kukubalia leo kwa kuwa umemwonyesha fedha au zawadi mbalimbali, kesho zinaweza kuwa hazipo, hawezi kuona umuhimu wako tena. Wapo watu wa aina hiyo, wanaweza kukuvumilia kwa muda mrefu wakachoka na kwa kuona unazo, wanaamua kukubali ili wakutumie.
Watu wa namna hiyo ndiyo wale wanaosema: “acha nimlie maana kila unavyomueleza hakuelewi. Mwanaume king’ang’anizi huyu.” Atakula, atatumia fedha zako lakini akili na mawazo yake yanakuwa kwa mtu mwingine tofauti ampendaye.
Atakuficha juu ya mpenzi wake, atakuongopea na kukurubuni kwa maneno ya wizi ili aweze kukuibia vizuri kumbe akili yake haipo kwako. Utamsindikiza katika safari yake ya kuelekea kwenye ndoa huku wewe ukiamini ndiyo mume wako, kisha anakuacha solemba.
Watu wa namna hiyo ni hatari. Wanakuua huku unajiona. Tena wengine wanakuchekea kabisa machoni kumbe akili zao hazipo kabisa. Hatoangalia ameishi na wewe muda gani zaidi ya kuufuata moyo wake unapopenda. Utajuta!
Wakati anataka kuchukua maamuzi magumu, hatoangalia umedumu naye miaka kumi au kumi na tano. Siku moja tu anaamka na kukwambia hakutaki, hakutaki kwa sababu hakupendi...

No comments:

Post a Comment