Tuesday 16 September 2014

USHAURI WA NDOA::NDOA YENYE MZOZO KILA SIKU, MKE ANA KASORO!


NAFURAHI sana kukutana nanyi wapenzi wasomaji wangu wa safu hii inayozungumzia maisha ya mapenzi kwa ujumla.Wiki iliyopita tulikuwa na mada iliyokuwa na utambulisho usemao; Ni afadhali ukimfumania mumeo na demu mzuri kuliko anayepaka wanja wa ‘sina bwana?’Leo tuko na mada mpya; NYUMBA YENYE MZOZO KILA SIKU, MKE ANA KASORO.
Sina nia mbaya ya kuwashambulia wanawake, bali najaribu kukumbusha majukumu ya kila mmoja ndani ya uhusiano huku watu wakitakiwa kufahamu nini maana ya ndoa.
Mada hii italenga ukweli, umuhimu na ujuzi anaoweza kuupata mwanamke ili atengeneze ndoa yake na maisha yaendelee mbele.
NDOA  NI MPANGO WA NANI?
Kwanza ieleweke kwamba, Mungu alipotangaza ndoa kwa mwanamke na mwanaume hakuchagua kundi! Alimaanisha mwanamke yeyote na mwanaume yeyote wenye akili timamu. Kwa hiyo ndoa ni mpango wa Mungu na si utaratibu wa mwanadamu.
KUSHINDWANA
Kumekuwa na ndoa nyingi zinazovunjika madai yakiwa ‘kushindwana’. Utasikia mke au mume anasema niliachana na mwenzangu, kisa tulishindwana tu!
Kwa nini wanandoa washindwane? Ukiwauliza wengi kwa nini mlishindwana? Watajibu tulikuwa hatuelewani ndani ya nyumba.
Watu hao ni wale walioapa kuishi katika shida na raha hadi kifo! Wengi wamekuwa wakila hiki kiapo bila kujua maana yake! Wanaongea kwa kukariri.
Kuishi kwa shida (tabu) ni pamoja na kushindwana na kutoelewana, kuishi kwa raha ni wakati wa maelewano. Sasa wanandoa wakishafika nyumbani baada ya kufunga ndoa hupenda kuishi kwa raha tu.
MKE NA ITIFAKI YA UONGOZI
Mimi naamini, mke na mume kila mmoja ndani ya ndoa anajua nafasi yake ilipo. Mume anajua yeye ni kiongozi mkuu (kichwa) na mke anajua yeye ni msaidizi, sasa kushindwana kunatokea wapi hadi ndoa ivunjike?Katika safu ya uongozi wa kiserikali kuna itifaki, rais wa nchi naye ana msaidizi wake, kwa Tanzania tunasema makamu wa rais. Haiwezekani hawa wawili wakagombana kwa sababu kila mmoja ana mipaka yake ya kazi na anaijua.
Haiwezekani rais yuko nje ya nchi, makamu akaamua kuteua mawaziri na kuwabadilisha wakuu wa mikoa kwa kadiri apendavyo yeye, hiyo ni kazi ya rais.
Lakini ndoa nyingi za leo, kati ya 100, 85 zimevunjika kwa sababu ya migogoro ya kutojua itifaki hii. Wanawake wengi wamekuwa wakitaka kuwa na nafasi ya urais ili na wao waweze kuchagua wakuu wa mikoa na kubadili mawaziri kwa vile watakavyoona inafaa.
Mizozo mingi ndani ya ndoa za leo ni mwanamke kulilia usawa wa kufikia levo ya mume kama kichwa! Hivyo kujikuta ndani ya nyumba kunakuwa na marais (viongozi) wawili lakini usukani mmoja! Mh!
USAWA MGUMU
Ziko ndoa, mume anaposema sitaki hiki, mke anasema mimi nataka. Tena wapo wanawake kwa kutojua au kujua na kupuuza wametunga hadi msemo wenye kuwaaibisha wao wenyewe wakisema ‘kama mume ni kichwa cha nyumba, mke ni shingo’
maana yao ni kwamba kichwa hakiwezi kugeuka bila shingo.
Wamesahau kuwa, ili iitwe shingo lazima kuwe na kichwa ndiyo maana kichwa kikitoka, mwili unaitwa kiwiliwili lakini kichwa kikiwa pembeni ya kiwiliwili kinaendelea kuitwa kichwa.
MANENO YENYE HEKIMA KWA MWANAMKE
Yupo dada yangu wa hiyari anaitwa Mary aliwahi kuniambia maneno ambayo sikuamini kama yalitoka kichwani mwake au alimsikia mtu, alisema:
“Mimi mpaka mwanaume wangu anipige nitakuwa nimejibizana naye nini? Kama akinijia juu kwa maneno makali nitatulia, baadaye akiwa amepunguza hasira nitakaa naye kwa upole na kuongea naye vizuri, ataelewa tu. Sasa utakuta mwanamke mwingine, mume anasema yeye anasema, tena yeye kwa sauti ya juu, basi ndani ya nyumba ni kelele tu.
“Ukiona hivyo, mke ni tatizo! Kujibizana na mume ndani ya nyumba ni kukosa heshima kwani mume ni kiongozi, huwezi kujibizana na kiongozi wako ndiyo maana Mungu alisema mke mwema hutoka kwake lakini hajasema popote kuhusu mume mwema anakotokea.”

No comments:

Post a Comment