Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda akisalimiana na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
Aggrey Mwanri mara baada ya kuwasili kwenye makao makuu ya jumuiya ya
Afrika Mashariki kufunga Mkutano wa kupiga vita dhidi ujangili wa
wanyamapori na kuendeleza uhifadhi wa wanayamapori mjini Arusha Novemba
8, 2014. Kushoto ni Waziri wa Mali asili na utalii Mh. Lazaro Nyalandu
na wa pili kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais
(Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu.(Picha zote na Zainul Mzige wa MOblog).
* Ataka iundwe timu kufuatilia utekelezaji wa Azimio la Arusha 2014
Na Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
amesema inahitajika dhamira ya kweli kutoka kwa wadau wote katika
kutekeleza Azimio la Arusha la kukabiliana na ujangili na kuendeleza
hifadhi za wanyama katika nchi za Afrika Mashariki na zilizo Kusini mwa
Ikweta.
Akizungumza na waandishi
wa habari juzi mara baada ya kufunga mkutano wa kikanda wa siku mbili
uliojadili mbinu za kupambana na biashara haramu ya wanyamapori
ulioandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Arusha, Waziri Mkuu
alisema: “Suala hili linataka uwajibikaji wa pamoja. Mashirika na
taasisi, wananchi na viongozi sote kama wadau wakuu, kila mmoja anapaswa
kushiriki vita hii kama kweli tunataka tuitokomeze.”
“Kwenye hili Azimio la
Arusha na nyie waaandishi wa habari pia mna sehemu yenu mmetajwa...
wamesema wanatafuta jinsi ya kushirikiana na vyombo vya habari ili
visaidie kutoa elimu kwa jamii kama njia ya kuelimisha umma,” alisema.
Waziri Mkuu aliwaeleza
waandishi hao kwamba Azimio hilo lina vipengele 20 ambavyo vinataka
utekelezaji katika ngazi ya nchi mojamoja, ngazi na kanda na ngazi ya
kimataifa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda akielekea kwenye chumba cha mapumziko kabla ya kufunga mkutano wa
kupiga vita dhidi ujangili wa wanyamapori na kuendeleza uhifadhi wa
wanyamapori mjini Arusha Novemba 8, 2014. Kushoto ni Waziri wa Mali
asili na utalii Mh. Lazaro Nyalandu, wa pili kulia ni Naibu Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Aggrey Mwanri na kulia ni Naibu Waziri, Ofisi
ya Makamu wa Makamu wa Rais (Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu.
“Nimepata faraja kwamba
mkutano huu haukuisha kijumlajumla tu, bali umekuja na maazimio 20
ambayo yametengwa kwa ajili yetu sisi wa ndani, mengine yanahusisha
ushirikiano wa kikanda na yako mengine yanawahusisha wadau wa
maendeleo,” alifafanua.
Ili kutekeleza azimio
hili, nimeshauri iundwe timu itakayoshirikisha vyombo vingi zaidi badala
ya kuiachia Wizara ya Maliasili na Utalii peke yake. Timu hii ikutane
kila baada ya miezi sita ili kufuatilia utekelezaji wa maazimio haya na
ikibidi Waziri atoe taarifa bungeni kuhusu utekelezaji huo,” alisema
Waziri Mkuu.
Mapema, akizungumza na
washiriki wa mkutano huo wakati wa kuufunga, Waziri Mkuu alisema kuwepo
kwa watu wa ngazi tofauti kwenye mkutano huo ni kielelezo tosha cha
umakini wao na nia thabiti ya kutokomeza ujangili katika ukanda huu.
Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda akiteta jambo na Waziri mdogo wa Marekani anayeshughulikia Uchumi,
Nishati na Mazingira, Bi. Catherine Novelli kwenye chumba maalum cha
mapumziko kabla ya kuelekea kwenye ukumbi wa mikutano makao makuu ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki kufunga mkutano wa kupiga vita dhidi
ujangili wa wanyamapori na kuendeleza uhifadhi wa wanayamapori mjini
Arusha Novemba 8, 2014.
“Tumeanzisha vita,
tusisahau kwamba bado kuna kazi kubwa mbele yetu na vita haijaisha.
Tuzidishe mapambano katika sehemu tatu: kwenye nchi unakofanyika
ujangili, nchi ambazo nyara zinapitishwa na nchi zinazopokea ama kununua
hizo nyara,” alisema Waziri Mkuu.
“Nakubaliana nanyi kwamba
hakuna nchi inayoweza kukabili suala la ujangili ikiwa peke yake.
Tunahitaji tuwe na sera mahsusi, sera ya pamoja ya kutuunganisha na
kutuongoza wakati tukitekeleza Azimio hili kwa kusaidiana na wadau wa
maendeleo,” alisema.
Alisema Azimio hilo
litaipa kazi ya ziada ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo kazi kubwa
itakuwa ni kusimamia na kuhakikisha utekelezaji wa wa Azimio hilo
unakuwa wa ufanisi.
Jumla ya nchi tisa zimetia
saini azimio hilo mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Nchi hizo ni
Burundi, Kenya, Uganda, Msumbiji, Tanzania, Sudan Kusini, Zambia, Rwanda
na Malawi.
Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda akisalimiana na Mbunge wa Kahama, James Lembeli, huku Waziri wa
Mali asili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu akifurahi jambo ndani ya
chumba cha mapumziko kabla ya kuelekea kwenye chumba cha mikutano.
Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda akizungumza na Waziri mdogo wa Marekani anayeshughulikia Uchumi,
Nishati na Mazingira, Bi. Catherine Novelli (wa pili kulia) kwenye
chumba cha mapumziko baada ya kuwasili ukumbi hapo. Kushoto ni Mratibu
Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez na kulia
ni Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Mazingira) Mhe. Ummy
Mwalimu.
Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, akibadilishana mawazo na Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa
Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)
nchini, Alvaro Rodriguez, kwenye chumba maalum cha mapumziko.
Waziri wa Mali asili na
utalii, Mh. Lazaro Nyalandu akimkaribisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda (wa
pili kushoto) kufunga rasmi mkutano wa kupiga vita dhidi ujangili wa
wanayamapori na kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori mjini Arusha Novemba
8, 2014. Kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mh. Magese Mulongo,
Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Mazingira) Mhe. Ummy
Mwalimu, Mbunge wa Kahama, James Lembeli na Waziri mdogo wa Marekani
anayeshughulikia Uchumi, Nishati na Mazingira, Bi. Catherine Novelli
wakiwa meza kuu.
Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, akizungumza na wadau waliohudhuria mkutano wa kupiga vita dhidi
ujangili wa wanayamapori na kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori mjini
Arusha Novemba 8, 2014 wakati akifunga rasmi mkutano huo wa siku mbili.
Mwakilishi wa Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania akichukua taswira za baadhi ya matukio yaliyokuwa yakiendelea mkutanoni hapo.
Baadhi ya wadau mbalimbali walioshiriki mkutano huo.
Baadhi ya wawakilishi
kutoka nchi tisa wakitia saini Azimio la Arusha la kukabili ujangili
mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Nchi hizo ni Burundi, Kenya,
Uganda, Msumbiji, Tanzania, Sudan Kusini, Zambia, Rwanda na Malawi.
Mratibu Mkazi wa
mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la
Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, akizungumza kwa niaba
ya Umoja wa Mataifa kwenye ufungaji wa mkutano wa kupiga vita dhidi
ujangili wa wanyamapori na kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori mjini
Arusha Novemba 8, 2014.
Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke, akizungumza kwa niaba ya serikali ya Ujerumani.
Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda akiteta jambo na Waziri wa Mali asili na utalii, Mh. Lazaro
Nyalandu wakati wa ufungaji rasmi wa mkutano huo uliodumu siku mbili
jijini Arusha.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiondoka ukumbini hapo mara baada ya kuufunga rasmi mkutano huo.