August 19, 2014
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Mkurugenzi
Msaidizi Habari, Elimu na Mawasiliano toka Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu Bw. Cosmas Mwaisobwa akiongea na waandishi
wa habari(hawapo pichani) kuhusu maandalizi ya utoaji mikopo kwa
mwaka wa masomo 2014/2015, wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini
Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO)
Bi. Zamaradi Kawawa.
Baadhi
ya Waaandishi wa Habari wakimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi Habari,
Elimu na Mawasiliano toka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
Bw. Cosmas Mwaisobwa wakati wa mkutano uliofanyika leo Jijini Dar es
Salaam.
MCHAKATO
WA MAOMBI
YA MIKOPO KWA MWAKA WA MASOMO 2014/2015
- MAANDALIZI YA UTOAJI MKOPO KWA MWAKA WA MASOMO 2014/2015
Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu
ya Juu ilitangaza mwongozo na vigezo vya utoaji mikopo kwa mwaka wa
masomo 2014/2015
kupitia magazeti na tovuti yake mnamo wezi Aprili 2014. Mwongozo
huo, pamoja na mambo mengine, uliainisha sifa za waombaji mikopo na
ruzuku, vipengele vya Mikopo, programu za vipaumbele kwa waombaji wa
shahada ya kwanza, shahada za uzamili na uzamivu waliodahiliwa katika
taasisi za elimu ya juu zinazotambulika. Maombi ya mikopo kwa
waombaji wapya yalifanyika kwa njia ya mtandao kwa anuani ya
http://olas.heslb.go.tz
au kupitia anuani ya tovuti ya Bodi ya Mikopo ambayo ni:
www.heslb.go.tz.
Kulingana
na Mwongozo wa Utoaji Mikopo na Ruzuku kwa mwaka wa masomo 2014/2015,
Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilifungua maombi ya mikopo kwa
njia ya mtandao (OLAS) kuanzia Aprili
23, 2014
na kuendelea kupokea maombi hayo hadi Julai
31, 2014.
Mabadiliko
machache yamefanyika, kubwa likiwa ni kwa wanufaika wanaoendelea na
masomo, tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita, hawakutakiwa kujaza
tena fomu kuthibitisha uhitaji wao wa mikopo kwa mwaka unaofuatia,
isipokuwa kwa wale ambao waliopenda kusitisha kuendelea kupokea mkopo
kutoka Bodi. Wanufaika wa mikopo wanaoendelea na masomo wataendelea
kupata mikopo yao kulingana na viwango walivyopangiwa awali.
- Maombi yaliyopokelewa
Jumla
ya maombi 58,037
yalikuwa yamepokelewa hadi kufikia tarehe 31 Julai, 2014. Kati ya
maombi hayo, jumla ya maombi 37,689
ni ya waombaji wa kiume na maombi 19,592
ni ya waombaji wa kike. Uchambuzi zaidi wa waombaji wa mikopo
unaonyesha kuwa Waombaji wa kundi la diploma ya ualimu wa sayansi ni
480
(Me – 324, Ke – 156), Waombaji wa shahada ya uzamili/uzamivu (kwa
vyuo vya ndani ya nchi) ni 276
(Me – 194, Ke – 82), Waombaji wa shahada ya kwanza (kwa vyuo vya
ndani ya nchi) ni 56,922
(Me – 37,460, Ke – 19,462), Waombaji wa shahada ya
uzamili/uzamivu (nje ya nchi) ni 126
(Me- 88, Ke – 38) na Waombaji wa shahada ya kwanza (nje ya nchi) ni
233
(Me
– 141, Ke – 92).
1.2 Uchambuzi wa
Maombi
Baada
ya kufungwa
rasmi kwa kipindi cha kupokea maombi ya mikopo, hatua inayoendelea
kwa sasa ni uhakiki (verification) wa taarifa za waombaji, kwa
kuzipitia nyaraka mbalimbali zilizoambatanishwa na waombaji mikopo
ambazo ni cheti cha kuzaliwa, vyeti vya taaluma, vielelezo vya
mdhamini, saini ya mwombaji na mdhamini wake na ushuhuda wa
Mwanasheria au Hakimu kwamba vivuli vya nyaraka zilizowasilishwa
kwenye Bodi ni halisi.
1.3
Upangaji
wa mikopo
Mchakato
wa uchambuzi
na upangaji wa mikopo utakamilika baada ya majina ya wanafunzi
waliodahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) kujiunga na vyuo
mbalimbali yanapowasilishwa rasmi kwenye Bodi ya Mikopo. Udahili wa
wanafunzi unafanywa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwa mfumo wa pamoja
wa udahili (CAS) unaotumiwa na vyuo takribani vyote vya elimu ya juu
nchini. Kwa vyuo ambavyo havimo katika mfumo wa pamoja wa udahili
(CAS) hutuma TCU majina ya wanafunzi ambao vimewadahili ili waweze
kuthibitishwa kabla ya kupatiwa mikopo. Taarifa za udahili ni
muhimu katika zoezi la upangaji wa mikopo kwa kuwa zinatoa mwongozo
wa gharama halisi za programu za mafunzo. Wanafunzi wanaostahili na
waliotimiza masharti na vigezo vya ukopeshaji ndio hupangiwa mikopo
kulingana na bajeti iliyotengwa na Serikali.
1.4
Kutangazwa
kwa majina ya wanafunzi waliopata mikopo
Majina
ya wanafunzi waliopata mikopo kulingana na udahili yatatangazwa
kwenye tovuti ya Bodi na taarifa hiyo pia itatangazwa katika vyombo
vya habari ili kuwataarifu wadau wote ikiwa ni pamoja na wanafunzi,
vyuo vya elimu ya juu, wazazi na umma kwa ujumla. Nakala za majina ya
wanafunzi waliopangiwa mikopo zitatumwa kwenye vyuo husika.
- WANAFUNZI WA MASOMO YA STASHAHADA YA UALIMU
Kwa kutambua umuhimu wa
masomo ya Sayansi na kukabiliana na upungufu
wa
walimu wa masomo hayo katika ngazi ya shule za Msingi na Sekondari,
mwaka huu serikali imetoa fursa ya mikopo kwa wanafunzi watakaojiunga
na masomo ya Stashahada maalum ya Ualimu wa masomo ya Sayansi na
Hisabati.
Wanafunzi
wapatao 5,000
wanatarajiwa kujiunga na Stashahada hii maalum katika Chuo Kikuu cha
Dodoma na wote watanufaika na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
- HITIMISHO
Kwa
Taarifa hii,
Bodi inapenda kuwataarifu wadau wote kuwa mchakato wa utoaji mikopo
kwa mwaka wa masomo 2014/2015 unaendelea vema.
Aidha,
Bodi inawasisitizia waombaji wa Mikopo, wazazi/walezi na umma kwa
ujumla kutambua kuwa Mikopo ya Wanafunzi wa elimu ya juu ni sehemu ya
utekelezaji wa Sera ya Uchangiaji wa Elimu ya juu na hivyo iwapo kuna
waombaji wanaoweza kujigharamia, wasiombe mikopo ili kutoa nafasi kwa
wahitaji wengi zaidi kunufaika.
Imetolewa
na:
KITENGO CHA HABARI,
ELIMU NA MAWASILIANO
BODI
YA MIKOPO YA
WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU.
na fredy mgunda