Leo
nataka kuzungumzia suala la uhongaji katika uhusiano. Kuhonga ni tabia
ambayo imeshamiri sana katika jamii yetu. Kipindi cha nyuma tumezoea
kusikia ama kuona wanaume wakiwahonga wanawake lakini sasa hivi mambo
yamebadilika.Wanawake
nao wameingia katika mkumbo wa kuwahonga wanaume ili wakubali kuwa nao
kimapenzi tu ama waoane kabisa.Tabia hii imekuwa ikiwatia majaribuni
walio wengi hali ambayo imesababisha baadhi ya watu wenye tamaa za
kijinga kushawishika kufanya ngono na watu ambao katika mazingira ya
kawaida wasingeweza kufanya nao.
Ni kitu cha kawaida kabisa kumkuta kijana wa kiume mwenye umri mdogo
kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mama mtu mzima ambaye angeweza kuwa
mama yake. Lakini hafanyi hivyo kwa matakwa yake bali kwa kushawishiwa
na pesa ama vitu vingine vya thamani.
Kuna utata kidogo katika neno hili kuhonga, wapo wanaojiuliza kwamba
hivi ninapompatia mpenzi wangu fedha kwa ajili ya matumizi madogomadogo
nitakuwa nimemhonga? Katika uhalisia neno kuhonga ni kitendo cha
mwanaume kutoa fedha ama zawadi kumpa mwanamke hasa pale anapomtongoza
ili awe mpenzi wake ama mke wake.
Pia katika kamusi ya kiswahili sanifu neno hilo limetafsiriwa kama
malipo ama zawadi itolewayo ili kupata kile unachohitaji au kutaka jambo
f’lani liharakishwe, kwa maana nyingine ni rushwa.Maana halisi ya
kuhonga itapatikana kutokana na nia ya mwanaume hasa pale anapotoa pesa
ama kitu kingine kwenda kwa mwanamke. Kwa mfano kama unatoa pesa kwa
ajili ya kumsadia mpenzi wako ama kumkidhia haja mke wako kutokana na
tatizo fulani alilonalo, hapo haiwezi ikachukuliwa kwamba umemhonga.
Lakini kama unatoa kitu ama pesa kutaka kulazimisha ama kumshawishi
awe rafiki yako, mpenzi wako, mke wako ama kwa kutaka kufanya naye
mapenzi, hapo itachukuliwa kwamba umehonga.Kikubwa unachotakiwa kujua ni
kwamba, hakuna uhusiano wowote baina ya mapenzi na pesa. Ndio maana
mapenzi yanaweza kuwepo hata pale pesa inapokosekana.Kwa
kudhibitisha hilo wengi wanaopata penzi kwa njia ya kuhonga, mapenzi
yao hayadumu kutokana na mmoja kati ya wawili hao kushawishika
kutengeneza uhusiano kutokana na pesa ama kitu kingine.
Utafiti unaonesha kwamba, kwa wanaume walio wengi kuhonga ni sehemu ya maisha yao licha ya kwamba ni katika viwango tofauti.
Hakuna mwanaume asiyehonga ukiachilia mbali wale ambao ni waumini
kikwelikweli ambao nao sina uhakika kama hawaingia katika kundi la
wahongaji kwa maana halisi ya kuhonga.Licha ya kwamba wapo pia baadhi ya
wanawake ambao wana tabia ya kuhonga wanaume ili wawapende, kasi
imeonekana kuwepo kwa wanaume ambapo hulazimika kutoa mamilioni ya pesa,
magari, simu za mikononi, na vitu vingine vya thamani kwa mabinti ili
tu waweze kuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Kimsingi niseme tu kwamba, katika uhusiano wa kweli baina ya wawili
waliotokea kupendana, suala la kuhongana hakuna. Usimpe mpenzi wako pesa
ili kumlainisha akufanyie jambo fulani kwani ipo siku utakuwa huna pesa
na unataka akufanyie, hapo ndipo mnaweza kuachana.
Msaidie pale atakapohitaji msaada wako, kama nilivyowahi kusema huko
nyuma kwamba, hutakiwi kuwa mbahili kwa mwenza wako kwani wewe ni yeye
na yeye ni wewe.
No comments:
Post a Comment