Kwa
mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni na jarida moja la masuala ya
afya la nchini Uingereza (BMC Public Health), unywaji wa vinywaji
vyenye sukari, kiasi cha mara tatu kwa wiki, huweza kunenepesha matiti
na unenepaji wa matiti huongeza hatari ya mwanamke kupatwa na saratani
ya matiti.
Waliofanyiwa utafiti huo ni wanawake 776 ambao hawajafikia ukomo wa
hedhi (Premenopausal) na wanawake 779 waliofikia ukomo wa hedhi
(Postmenopausal).
Pamoja na maswali mengine waliyoulizwa, wanawake hao waliulizwa kiasi
wanachokula kwa upande wa vyakula na vinywaji vyenye sukari kama vile
chokoleti, keki, ice cream, soda, n.k na huwa wanaweka vijiko vingapi
vya sukari kwa vinywaji wanavyotayarisha, kama chai au juisi.
Akiongelea matokeo ya utafiti wao, mtafiti na mwandishi kiongozi wa
utafiti huo kutoka Chuo Kikuu cha Laval cha Quebec, nchini Canada,
Caroline Diorio alisema kuwa matokeo yalionesha kuwepo kwa uhusiano
mkubwa kati ya utumiaji wa sukari kwa wingi na kuongezeka kwa ukubwa wa
matiti ya wanawake kutoka makundi yote mawili (wasichana na watu
wazima).
Katika utafiti wao, wamegundua zaidi kuwa wanawake waliofikisha ukomo
wa hedhi matiti yao yaliongezeka ukubwa zaidi kwa kula vyakula vingi
vyenye mafuta, wakati wanawake ambao hawajafikisha ukomo wa hedhi,
waliongezeka ukubwa wa matiti yao kwa kula vinywaji vyenye sukari
visivyopungua vitatu kwa wiki.
Matokeo ya utafiti huo yanatoa picha kwamba kuwa na matiti makubwa
kunakosababishwa na ulaji wa sukari pamoja na mafuta kwa wingi huongeza
hatari ya kupatwa na saratani ya matiti kwa asilimia 3.
Dk. Dioro anamalizia kwa kusema kuwa utafiti zaidi unahitajika,
hususan katika makundi ya watu wenye matumizi makubwa ya sukari. Lakini
hata hivyo, amesema kuwa hadi utafiti mwingine utakapofanyika na
kuthibitisha vinginevyo, kwa sasa uhusiano wa matumizi makubwa ya sukari
na unenepaji wa matiti kwa wanawake uko wazi.
Kwa kuwa unenepaji wa matiti una uhusiano mkubwa na ulaji mkubwa wa
mafuta na sukari kwa njia mbalimbali kama zilivyoanishwa hapo juu, na
kwa kuwa unenepaji wa matiti unaongeza pia hatari ya mwanamke kupatwa na
saratani ya matiti, ni sababu tosha kabisa ya wewe kuamua kuachana na
unywaji wa vinywaji baridi vyenye sukari nyingi kwa faida ya afya yako.
Kama ambavyo mara kwa mara tumekuwa tukisisitiza, tuepuke sana
matumizi makubwa ya sukari na tunapoitumia basi tuitumie kwa kiasi
kidogo sana na badala yake tupendelee kutumia asali na kula kwa wingi
matunda na mboga za majani ambazo huwa na sukari asilia ambayo haina
madhara mwilini.
endelea
No comments:
Post a Comment