Na Magreth Kinabo,Dodoma
Serikali
imesema kwamba Bunge Maalum la Katiba linaendelea kwa mujibu wa Sheria, mjadala
wa hoja ya kusitishwa kwa Bunge hilo, umefungwa rasmi leo.
Aidha
Serikali imewaondoa hofu wananchi kwamba hakuna mgogoro wa kisiasa, hivyo waendelee
na shughuli zao za kujipatia kipato(riziki) kama kawaida, pia ipo macho kupitia
vyombo vyake vya usalama,itasimamia sheria na taratibu zilizowekwa ili
kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na amani na utulivu.
Kauli hiyo
imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.
Asha Rose Migiro kwenye kikao cha Arobaini cha Bunge
hilo wakati akitoa tamko la Serikali
kwenye mjadala wa mwisho wa kujadili sura zote 15 zilizobakia za Rasimu
ya Katiba Mpya.
“Bunge hili
linaweza kuendelea na shughuli zake. Nawaomba Watanzania wafahamu mjadala wa
kusitisha Bunge umehitimishwa hii leo kisheria na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Dk.
Migiro.
Dk. Migiro
aliongeza kuwa kwa taarifa walizonazo
majadiliano baina na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania(TCD) pamoja na
vyama vyote husika yataendelea Septemba 17 na 18, mwaka huu, kwa sababu
mchakato huo si wa chama kimoja, wala viwili au vitatu , bali mchakato wa Watanzania wote kupitia mfumo
ambao umewekwa wa vyama vyote kisheria.
Akizungumzia
kuhusu takwimu za wajumbe wa Bunge hilo, Dkt. Migiro alisema kuwa lina wajumbe 630, kati yao waliotoka nje
ya Bunge hilo ni wajumbe 130 ni sawa na asilimia 21 ya wajumbe wote.
“Wajumbe
waliobakia ndani ya Bunge hili ni 500, sawa na asilimia 79 ya wajumbe wote,
tukitazama mambo ya takwimu kwa kutambua
Kundi la 201. Imejitokeza dhana kwamba wajumbe waliobakia humu ndani ni wa aina
moja, hiyo si kweli,”alisema.
Dk. Migiro
alisema kati ya wajumbe 500, waliobaki
katika Bunge hilo, 189, wanatoka katika kundi la 201.
Alisema wajumbe
wengine waliobakia, 348 wanatoka upande
wa Tanzania Bara, kati ya hao, wajumbe 125 ni wajumbe wanaotoka Kundi la 201.
“ Tukiangalia
upande wa Zanzibar wajumbe waliobakia ni 152, kati yao wajumbe 64 wanatoka Kundi
la 201.Tungependa kusisitiza Kundi la 201 ndio wajumbe ambao kwa wingi wao kitakwimu
na kimakundi wanawakilisha Taifa
letu kwa sura zote.
“ Ni dhahiri
waliobakia humu ndani ni wengi, hii ina maana kwamba kwa kuzingatia matakwa ya
masuala ya kisheria kwa maridhiano, kwa majadialiano na kwa kushawishi hoja.
“Wajumbe waliobakia ni wengi wana uhalali kisheria na kisiasa.
Tutaendelea na shughuli zetu kama sheria inavyotutaka, uwakilishi wa Bunge
umetimia … tuna wajibu wa kisheria wa kufanya yale tunayoyataka kuyafanya,” alisisitiza huku akisema waliotoka nje kwa pande zote mbili hawafikii theluthi moja.
Alifafanua kuwa
vyama vilivyotoka nje ya Bunge hilo, ni vitatu,vilivyobakia ndani ya ni 18 ambavyo vimesimamia na
vinaendelea kusimamia umoja wa kitaifa wa
nchi yetu.
Akichangia mara
baada ya tamko hilo, mjumbe wa Bunge hilo, John Shibuda alimpongeza mtoa
taarifa hiyo ya Serikali na kuipongeza Serikali kwa kushinda kesi.
Aliwataka Watanzania
kuchuja kati ya siasa na maslahi binafsi.
No comments:
Post a Comment