Friday, 12 September 2014

SOMO LA LEO::SITTA awapa somo Viongozi wanaojiita UKAWA.


 
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta akiongoza bunge hilo.
 
Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dodoma.
 MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta amewaadaa baadhi ya viongozi wanaojiita UKAWA kwa taarifa yao ya kutaka kumfikisha Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa kwa kuendeleza mchakato huo wa Katiba.
 
Kauli hiyo imetolewa leo 12 Septemba, 2014 mjini Dodoma na Mhe. Sitta kufuatia baadhi ya viongozi hao, kudai kuwa watampeleka katika mahakama hiyo.
 
Mhe. Sitta ameeleza kuwa baadhi ya viongozi wa kundi hilo kuwa wanakipaji kikubwa cha uigizaji huku akifafanua kuwa wakati walipokuwa Bungeni wakati wa mchakato wa kupiga kura za siri, viongozi wa kundi hilo walizifanya kura hizo kuwa wazi na baadaye kuja na kauli kuwa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea sasa sio halali lihairishwe.
 
“Juzi Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekutana nao mara mbili kwa muda wa saa Saba na katika kukutana huko wakafikia maafikiano, lakini siku moja baadaye wao wamekana yote waliyokubaliana hapa mjini Dodoma, kwa hiyo ni vyema wananchi wakawapima hawa watu”, alisema Mhe. Sitta.
 
Aidha, Mhe. Sitta aliasa kwa kusema kuwa wananchi na viongozi wanatakiwa kujua kuwa mchakato wa bunge Maalum la Katiba sio jambo la mzaha na wao hawapo hapo bungeni kwa mzaha mzaha.
 
“Mimi nawaambia kuwa hapo mwakani watakaposhindwa uchaguzi basi warejee katika fani zao ambazo Mwenyezi Mungu kawajalia”, alisema Mhe. Sitta.

No comments:

Post a Comment