Bila
shaka wasomaji wa safu hii mko vizuri na mnaendelea na majukumu yenu ya
kila siku. Kwa upande wangu mimi ni mzima wa afya.Ni siku nyingine
Mungu ametujalia uzima tunakutana kupeana mawili matatu yahusuyo maisha
ya uhusiano.
Mapenzi
yana nafasi kubwa katika maisha ya wanadamu, mapenzi ni hisia kali
zilizoko ndani ya miili yetu ndiyo maana inatokea mtu anampenda mtu
kiasi cha kutaka hata dunia nzima ijue kama amependa.
Uzuri wa
mapenzi ni kupendana, kila mmoja ampende mwenzake. Ikitokea mmoja
amempenda mwenzake halafu huyo anayependwa haoneshi ushirikiano hapo
ndipo kunapokuwa na tatizo.
Anayependa anafanya jitihada za nguvu
kuhakikisha somo lake linaeleweka lakini wapi, jibu linakuwa ni ‘no’.
Jibu linakuwa hilo kwa sababu unayempenda yeye hakupendi.
Nimekuwa nikipata maswali mengi katika safu ya ushauri, wengi
wanang’ang’ania kupenda mahali ambapo kimsingi hapapendeki. Yule
anayependwa, moyo wake unakuwa hautaki tu kuridhia. Upendo haupo kwake,
kuna aina ya mtu ambaye yeye anampenda na si wewe.
Kwa kuwa mapenzi ni hisia, mtu anakuwa mgumu kukubaliana na matokeo.
Anang’ang’aniza penzi kwa nguvu zote. Anakuwa tayari kuligharamia penzi
hilo kwa namna yoyote. Akili inamtuma kwamba ipo siku atamuelewa na moyo
wake upate pumziko.
Akili yake hapo haiwazi kabisa kwamba kuna mtu unaweza ukampenda na
yeye asikupende. Anasahau kabisa ule msemo wa ndege mzuri hutua katika
mti aupendao. Hawazi kwamba sifa alizoziona kwa huyo anayempenda naye
ana sifa zake kwa mtu anayempenda.
Kabla hatujaendelea, ngoja nikupe mfano hai. Kuna mtu tumpe jina la A
(jina lake halisi lipo). A yeye ameteseka kwa muda mrefu kumpenda mtu
ambaye hampendi, amefanya jitihada nyingi kuhakikisha anampata binti
mmoja lakini wapi. Majibu anayopewa ni zaidi ya kuudhi lakini eti akawa
hakati tamaa.
Anasema amemweleza binti huyo kwamba anampenda,
amewatuma marafiki zake, ametuma zawadi mbalimbali kama maua, vocha na
nyinginezo lakini vyote hivyo vilikuwa ni kazi bure.
Mtoto wa kike haoni wala hasikii, hataki tu! Alionyesha msimamo wa
hali ya juu. Hakutaka kugeuka nyuma. Sasa je, kupitia mfano huo
tunajifunza nini?
Binti alifanya vile kwa sababu moyo wake haupo pale. Kama ingekuwa ni
tamaa basi pengine angekubali mapema kutokana na mbinu mbalimbali
ambazo A alizitumia. Ndugu zangu, penzi halilazimishwi maana
ukilazimisha athari zake ni kubwa huko mbele ya safari.
Mbaya zaidi, uking’ang’ania sana, anaweza kukubalia leo kwa kuwa
umemwonyesha fedha au zawadi mbalimbali, kesho zinaweza kuwa hazipo,
hawezi kuona umuhimu wako tena. Wapo watu wa aina hiyo, wanaweza
kukuvumilia kwa muda mrefu wakachoka na kwa kuona unazo, wanaamua
kukubali ili wakutumie.
Watu wa namna hiyo ndiyo wale wanaosema: “acha nimlie maana kila
unavyomueleza hakuelewi. Mwanaume king’ang’anizi huyu.” Atakula,
atatumia fedha zako lakini akili na mawazo yake yanakuwa kwa mtu
mwingine tofauti ampendaye.
Atakuficha juu ya mpenzi wake, atakuongopea na kukurubuni kwa maneno
ya wizi ili aweze kukuibia vizuri kumbe akili yake haipo kwako.
Utamsindikiza katika safari yake ya kuelekea kwenye ndoa huku wewe
ukiamini ndiyo mume wako, kisha anakuacha solemba.
Watu wa namna hiyo ni hatari. Wanakuua huku unajiona. Tena wengine
wanakuchekea kabisa machoni kumbe akili zao hazipo kabisa. Hatoangalia
ameishi na wewe muda gani zaidi ya kuufuata moyo wake unapopenda.
Utajuta!
Wakati anataka kuchukua maamuzi magumu, hatoangalia umedumu naye
miaka kumi au kumi na tano. Siku moja tu anaamka na kukwambia hakutaki,
hakutaki kwa sababu hakupendi...
No comments:
Post a Comment