Wednesday, 17 September 2014

WEMA AZIMA JEURI YA KAJALA


Stori: Erick Evarist
FEDHA haina mwenyewe! Siku chache baada ya kudaiwa kuyumba kiuchumi kiasi cha kuzidiwa jeuri na aliyekuwa shosti wake, Kajala Masanja ‘K’, Beautiful Onyinye, Wema Sepetu ameibuka na kujibu mapigo kwa kumwaga ‘mafedha’ ukumbini, Risasi Mchanganyiko linashuka na mzigo kamili.
Wema akimwaga manoti kwa mwimbaji wa Skylite Band.
Tukio hilo lililowaacha watu midomo wazi lilichukua nafasi Ijumaa iliyopita katika Ukumbi wa Thai Village, Masaki jijini Dar kulipokuwa na sherehe maalum ya kuzaliwa kwa mwanzilishi wa vinywaji vikali vya Jack Daniel, Mr. Jack’s.
WEMA ALIUMIA MOYONI
Chanzo kilicho karibu na Wema, kilipenyeza habari kuwa, msanii huyo hakufurahishwa na kitendo cha watu kumuona kafulia kiasi cha kuzidiwa na K ambaye aliwahi kumlipia faini ya shilingi mil. 13 kumnusuru na kifungo cha miaka mitano jela.
KIFUNGO KILIKUWAJE?
Kajala alikuwa anakabiliwa na kesi ya kuuza nyumba iliyowekwa kizuizini na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) baada ya mumewe, Faraji Agustino kukumbwa na tuhuma za kutakatisha fedha haramu.
Wema akizidi kumwaga manoti kwa mwimbaji huyo.
TUJIUNGE NA CHANZO
“Wema hakufurahishwa na kitendo cha watu kumsemasema kila siku kwamba kafulia, hakupenda kuambiwa kazidiwa fedha na K wakati anaamini bado fedha anazo sema aliamua kukaa kimya kwani hakupenda majibizano ya kwenye vyombo vya habari,” kilisema chanzo hicho.
JEURI YAANZIA TEN LOUNGE
Awali, mwanahabari wetu alimshuhudia Wema akiwa na wapambe wake katika Ukumbi wa Ten Lounge (zamani Business Park) uliopo maeneo ya Victoria, Makumbusho jijini Dar ambapo alifika kushuhudia burudani za wasanii mbalimbali.
RAUNDI ZAZUNGUSHWA
Akiwa ukumbini hapo, wapambe wake walionekana kutumia vinywaji mbalimbali (vilivyo na visivyo na kilevi) huku mwenyewe naye akitumia mvinyo wake ambao kwa macho ya kawaida unaonekana si wa pesa za mawazo.
FULL KUREKODIWA
Kuonesha kwamba fedha ipo, kila tukio alilokuwa akilifanya Wema na wapambe wake ukumbini hapo, lilikuwa likirekodiwa na mtu maalum waliyekuja naye na kisha kuondoka pamoja.
Pesa aliyotunzwa mwimbaji huyo na wema.
THAI VILLAGE SASA
Baada ya kutumia vya kutosha Ten Lounge, msururu wa Wema ulihamia katika Ukumbi wa Thai Village ambako ndipo jeuri ya fedha ilipokwenda kukamilika.
Chanzo makini kilichokuwepo ukumbini humo kilimwaga data kwamba, Wema alifika akiwa na kundi la wapambe wake na kwenda kukaa mahali kwa muda huku raundi za vinywaji zikizungushwa kwa staili ya kata mti, panda mti.
AKUNWA NA MUZIKI WA SKYLIGHT
Wakati Miss huyo asiyechuja tangu alipotwaa taji hilo mwaka 2006 akiendelea kupata vinywaji vya hapa na pale, muziki mzuri wa Skylight Band ulimuinua na kujikuta yupo jukwaani chini ya himaya ya mwanamuziki mahiri anayefahamika kwa jina la Sam Mapenzi.
“Sam alimpagawisha kinoma Wema pale alipopiga wimbo wa All of Me ulioimbwa na John Legend, mtoto wa kike akapanda jukwaani na kukaa karibu yake, akawa anasikiliza mashairi hayo huku akimwaga manoti ya hatari katika kumtunza,” kilisema chanzo hicho.
ZAMZIDI KAJALA
Chanzo hicho kilizidi kutiririka kuwa, kwa hesabu za harakaharaka, Wema alimwagia Sam noti za elfu kumikumi zisizopungua mia moja (jumla milioni moja) hivyo kuzipiku zile za Kajala alizomwaga hivi karibuni wakati akiwatunza Yamoto Band katika Viwanja vya Leaders zilizodaiwa kufikia shilingi laki saba.
Mwigizaji wa filamu za Kibongo, Beautiful Onyinye, Wema Sepetu.
“Chezea Madam (Wema) wewe, kamwaga pesa kama hana akili nzuri, alitoa pochi ndogo iliyokuwa ndani ya pochi kubwa, balaa.“Zile alizotoa Kajala kwa Yamoto Band zilikuwa fedha za mboga, Madam kamwaga fedha ya maana leo,” kilisema chanzo hicho.
MPAMBANO UNAENDELEA?
Baadhi ya wadau wa burudani waliozungumza na mwandishi wetu, walidai Kajala hawezi kukubali kuzidiwa, hivyo lazima naye atasababisha tukio la maana hivi karibuni.
“Unafikiri Kajala atakubali? Subirini mtaona jeuri yake hivi karibuni,” alisema mdau huyo huku akiomba hifadhi ya jina.
TUJIKUMBUSHE
Makabrasha ya Risasi Mchanganyiko yanaonesha kwamba, Wema na Kajala walikuwa marafiki wa kushibana lakini baadaye walipishana kauli na sasa kila mmoja anaishi kimpango wake.

No comments:

Post a Comment