Waziri Mkuu,Mizengo Pinda.
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema uamuzi wa Serikali wa kukopa fedha ili
kuboresha miundombinu kwenye taasisi za elimu ya juu nchini ulichukuliwa
kwa lengo la kujibu tatizo la sasa la wingi wa vijana wanaohitimu
kidato cha sita.
Ametoa kauli hiyo jana
usiku (Ijumaa, Oktoba 10, 2014) wakati akizungumza na wahadhiri,
wakufunzi, wanafunzi na wanajumuiya ya Chuo Kikuu Huria (OUT) mara baada
ya kuzindua jengo la ghorofa 10 linalojulikana kama Ghorofa la Elimu ya
Masafa ya Huria (Open Distance Learning Tower – ODL Tower)
lililogharimu sh. bilioni 3.
Waziri
Mkuu ambaye aliwasili jijini Dar es Salaam jana mchana akitokea
Morogoro, alitembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania ili kukagua utekelezaji wa mradi wa Sayansi na
Teknolojia ya Elimu ya Juu (Science and Technology Higher Education
Project - STHEP) unaoendeshwa chini ya uhisani wa Benki ya Dunia.
“Mradi
huu ni wa miaka mitano ambao ulianza mwaka 2009 na unakamilika mwaka
huu. Lengo hasa lilikuwa ni kujenga uwezo wa wataalamu wetu ambao
watakuja kufundisha watoto wa kidato cha sita ambao idadi yao inazidi
kuongezeka kila mwaka.”
Alisema Serikali iliridhia pia fedha
hizo zitumike kujenga miundombinu mipya ya kufundishia pamoja na
kukarabati baadhi ya zamani kwani kama miundombinu haipo, kazi ya
kufundisha haitakuwepo.
“Tulikubaliana pia fedha hizo zinunue
vifaa kwa maana ya kompyuta, vifaa vya maabara pamoja na samani za
maktaba na baadhi ya madarasa. Ni fedha za mkopo lakini zimetumika
kusaidia Watanzania wote.”
Chini ya uhisani wa mradi huo, Chuo
Kikuu Huria kimesomesha wahadhiri 29 kati 12 ni masomo ya Uzamifu na 17
ni masomo ya uzamili. Pia kimejenga Maabara za kompyuta tatu, maktaba ya
kuweka watu 224 kwa wakati mmoja, vyumba vya mihadhara (seminar rooms)
maabara ya lugha (language lab), ununuzi wa kompyuta na samani.
Mapema akiwa katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Waziri Mkuu alikagua majengo mapya ya ghorofa la
shule kuu ya elimu, sayansi ya majini (Aquatic Sciences and
Technologies), Multi Complex Building ambalo litakuwa na kituo cha
wanafunzi, pamoja kuzindua jengo jipya la Uhandisi Migodi na Usindikaji
Madini (Mining and Mineral Processing Building) lililopo kwenye Chuo cha
Uhandisi na Teknolojia (College of Engineering Technology).
Akitoa taarifa ya miradi yote
hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Rwekaza
Mukandala alisema katika awamu hii ya kwanza ya mradi wa STHEP, Chuo
hicho kilifanikiwa kupata ufadhili wa Dola za Marekani milioni 40.79
(sawa na sh. bilioni 67).
Chini ya mradi huo, Prof. Mukandala
alisema chuo kimefanikiwa kuendeleza kimasomo wafanyakazi wake zaidi ya
150, kujenga majengo mapya manane, kusomesha wahadhiri tarajiwa 163
ambapo 63 wamesoma shahada za umahiri (masters) na 67wamepata shahada za
uzamivu (Ph.D).
“Tumeweza
kununua vifaa mbalimbali vikiwemo vya maabara, kompyuta 864, vitabu
zaidi ya 960, na vifaa vya teknolojia, uhandisi na sayansi. Pia tumeweza
kupanua madarasa, maabara na ofisi .”
“Tumepata
maabara mpya 49 zitakazokuwa zikitumiwa na wanafunzi 3,630 kwa wakati
mmoja; madarasa 53 yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 4,200 kwa wakati
mmoja; ofisi 322 zitakatumiwa na wafanyakazi wasiopungua 600,”
aliongeza.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment