WAKATI Rais Jakaya Mrisho Kikwete Jumanne wiki hii alisherehekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa kwa kutimiza miaka 64, Mchekeshaji Steven Mengere ‘Steve Nyerere’, Jumatano iliyopita alimpa zawadi baada ya kumvunja mbavu wakati wa hafla ya makabidhiano ya Katiba Mpya Inayopendekezwa iliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Steve, aliyepanda jukwaani kuwakilisha wasanii, alitumia dakika zisizozidi tano kumsifu Rais Kikwete kwa mchango wake mkubwa kwa wasanii, akidai ndiye amewafungulia milango ya mafanikio na kwamba watamkumbuka kwa kitendo cha kutambuliwa kwao kikatiba.
Baada ya hapo, mchekeshaji huyo maarufu wa kuiga sauti za watu mbalimbali, alianza kwa kuigiza sauti ya Rais Barack Obama wa Marekani, akimuigiza kumsifu Rais Kikwete kwa kutengeneza katiba mpya na kisha kuwasifu Watanzania na nchi yao kisha akawashukuru kwa kuwaambia asante.
“Mbona hamuitikii jamani Watanzania, au
Kiingereza not reachable, naona mna-vibrate tu,” maneno hayo licha ya
kuwachekesha mamia ya waliomsikiliza, pia walimfanya Rais Kikwete na Dk.
Shein, kuvunjika mbavu hadi kulazimika kulalia meza zao.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho kikwete na Rais
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Mohamed Ali Shein, kwa pamoja
wakionyesha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
Alipomaliza kuiga sauti ya Obama, akaendelea kwa kumuiga Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akimnukuu akielezea jinsi Rais Kikwete
alivyokwenda kwake na kumuambia kuhusu nia yake ya kutaka kuwa Rais wa
Tanzania.Baada ya kumaliza kumuiga Mwalimu, Steve Nyerere alimgeukia JK na kuiga sauti yake na jinsi anavyofanya baadhi ya mambo katika hotuba. Aliiga staili ya Rais anapowasalimia watu walio mbali, anavyojishika kichwani na maneno yake, hali ambayo kwa muda wote ilimchekesha Rais na viongozi wengine wengi waliokuwepo meza kuu, akiwemo Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Shein, Rais Mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Makamu wa Rais Mohamed Bilal na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta.
Kabla ya Rais kukabidhiwa Katiba hiyo inayopendekezwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Bunge Maalum la Katiba, Andrew Chenge, alitoa muhtasari wa kilichomo ndani ya Katiba hiyo mpya, ambayo hatua itakayofuata ni kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni kabla ya kuthibitishwa na kuanza kutumika rasmi.
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, ndiye aliyekabidhi katiba hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete aliyeasisi mchakato huo, akizima ajenda ya muda mrefu ya vyama vya upinzani.
No comments:
Post a Comment