Wednesday, 15 October 2014

KARIBU NYIKANI::CHADEMA MBEYA NA SURA ZILIZOJAA MACHOZI


 Kulia ni Mwenyekiti wa (CHADEMA) MBEYA MJINI, John Mwambigija, akizungumza na waandishi wa habari
NA GORON KALULUNGA
NIWASHUKURU wasomaji wangu mliotumia gharama kubwa za muda na fedha kwa kunipigia simu na kuandika jumbe fupi za maandishi kuhusu makala zilizopita ikiwemo ile ya athari ya saikolojia kwa taifa.
Ikumbukwe kuwa, meno ya mbele au sebuleni, hayana nguvu ya kutafuna chakula, bali mara kadhaa yamekuwa shujaa kwa ajili ya mwonekano wa mtu na kung’ata ulimi.
Uongozi ni sanaa, inayofanyika kwa watu, ili wafanye kwa manufaa yako, kwasababu unayoitaka au wanayoitaka wao, lakini mdomo kimya unatunza busara kulio mdomo unaobwatuka.
Dhima ya vyama vingi ni kushika dola, lakini hapa kwetu Tanzania,  dhima imegeuka kuwa ni kuundiana tuhuma na kusingiziana.
Kutokana na hali hiyo, jamii imebadilika, badala ya kuwa jamii moja na tulivu, sasa imekuwa jamii ya vita.
Wahanga wa siasa mara nyingi wanakuwa na hila na machoi katika mioyo na nyuso zao, huku wakiwaaminisha wananchi kuwa wao ni watu safi na wanaaa kwa mabadiliko ya fikra na maendeleo ya jamii.

Baadhi ya watanzania wanahitaji mabadiliko, wanayataka mabadiliko ndani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) na wasipoyapata huko wapo tayari kuyapata nje ya CCM.
Lakini wanakatishwa tamaa kuyaendea huko nje ya CCM kutokana na baadhi ya mambo yanayotendeka na kutokea, kama ifanyavyo CCM, ama zaidi ya CCM.
Tangu tunadai uhuru wa Tanganyika na hata mapinduzi matukufu ya Zanzibar, tulikataa mfumo wa ukoloni na ubeberu na kuhakikisha tunakomboa hata nchi zingine na kulaani mifumo hiyo.
Leo hii, kuna vyama nje ya CCM, vinakuja na mfumo ule ule ambao watanzania tuliukataa na kuupinga.
Kila anayewapinga kwa hoja hasa ndani ya vyama vyao huishia kutishwa kuwa watamfukuza au ajivue  gamba, badala ya kushindana nae kwa hoja.
Katiba ya nchi hii, imetoa uhuru wa kutoa maoni kwa kila mtanzania, lakini ndani ya baadhi ya vyama vya siasa, baadhi ya viongozi hawataki wengine watoe maoni.
Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, amewahi kunukuliwa akisema kuwa, bila kuwa na majadiliano hai ya chemsha bongo, mpaka hivi leo wanasayansi wasingeweza kuzalisha dawa nyingi za kutuliza maumivu, maana wangepigwa marufuku wengine kufikiri na kutengeneza dawa hizo kama ambavyo tume ya Warioba inavyotaka.
“Mfumo wa ukawa ni mfumo wa kudumaza fikra za watanzania na siyo uhisho wa fikra za taifa ambalo wananchi wake wanatakiwa kufikiri na kutoa maoni yao” anasema Shibuda.
Uongozi imara wa mtu yeyote ni ushawishi na wala siyo ubabe wa kutishia na kuhimiza kauli za ubeberu na kuzira.
Ndani ya Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Mbeya, wimbi hilo la kuikana demokrasia huku kikitangaza kuwa ni cha demokrasia, limeshika kasi.
Wanaotajwa kutaka kuwania nafasi za ubunge katika majimbo ya mkoani Mbeya, kupitia chama hicho, wananangwa kuwa wameamua kupeana nafasi za uongozi na kuwang’oa viongozi wasiowaunga mkono.
Baadhi ya viongozi hao ambao wote ni viongozi wa kanda ya nyanda za juu kusini, wanadaiwa, kutumia jina la Katibu Mkuu, Dr. Wilbroad Slaa, kuwa yeye ndiye hawataki viongozi waliokuwepo, hivyo, kuamua kuunda safu yake mpya kupitia wao.
Wanaotajwa kuratibu na kufanikiwa kung’oa wenzao kwa mtazamo wa kugombea ubunge 2015, ni pamoja na Mratibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za juu kusini, Frank Mwaisumbe, mratibu wa hamasa kanda, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mbeya mjini, John Mwambigija.
Wengine ni mkuu wa kitengo cha utafiti na sera kanda ya Nyanda za juu kusini, Fanuel Mkisi,  mkuu wa kitengo cha sheria na haki za binadamu, Fadhil Shombe,  mkufunzi mkuu kanda, Pascal Ahonga na Jamson Mwiligumo ambaye ni mkuu wa Chadema ni msingi.
Baadhi ya viongozi hao, wanatajwa kuwa ni wagombea tarajari wa nafasi za ubunge katika majimbo ya Mkoa wa Mbeya, akiwemo Frank Mwaisumbe, anayetarajia kugombea jimbo la Mbeya vijijini.
Jamson Mwiligumo, anatajwa kuwa mgombea tarajari jimbo la Lupa Chunya, John Mwambigija na Lucas Mwampiki ambaye ni mkuu wa ulinzi na usalama kanda, wanatarajia kugombea Ubunge jimbo la Rungwe Magharibi.
Licha ya nafasi ya katibu wa mkoa kuwa wazi kwa sasa mpaka hapo litakapoletwa jina moja kutoka ofisi ya Katibu Mkuu Taifa, mpaka sasa kikosi hicho kinahusishwa na kumtangaza kuwa Katibu wa Chadema mkoa ni Fanuel Mkisi.
Majina ambayo yamepelekwa ofisi ya Katibu mkuu yakingoja uteuzi ni ya Boid Mwabulanga anayetetea nafasi yake, Jidawaya Kazamoyo na Fanuel Mkisi.
Ofisi ya katibu mkuu taifa tayari imepelekewa barua inayoonesha kusigana kwa viongozi hao mkoani Mbeya.
Tayari baadhi yao, wamemwandikia barua Katibu Mkuu wa Taifa, Dr. Wilbroad Slaa, kuhusu mwenendo wa kundi hilo, barua yenye kumbukumbu namba CDM/G/10/113.
Barua hiyo iliandikwa Agosti 9, mwaka huu, ikieleza jinsi kamati ya rufaa ya kanda ilivyo na mipango ovu dhidi ya chama hicho mkoani Mbeya.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa chama hicho, wanasema walisikitishwa na kauli ya Mwenyekiti wa Chadema Mbeya mjini, John Mwambigija, aliyoitoa kwenye mazungumzo na baadhi ya viongozi wa Mbeya Vijijini katika bustani ya Wagadugu Mbalizi, Agosti 29 mwaka huu, kuwa fitina zake zimefanikiwa baada ya kumng’oa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mbeya Vijijini, Elia Kabolile na aliyewahi kuwa katibu wa Chadema mkoa wa Mbeya, Eddo Mwamalala.
Kwa mipango hii, je watanzania wanaohitaji mabadiliko kuyapata nje ya CCM, malengo yao yatatimia? Au itabaki mpango ule ule wa “tukose” wote?
Karibuni nyikani.

No comments:

Post a Comment