MWANAFUNZI Hamimu Mussa (11), wa Shule ya Msingi Uhuru Manispaa
ya Kigoma Ujiji, amefariki dunia baada ya kuanguka kwenye mti wa mwembe
na mwingine kuvunjika mguu na mkono.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Kamishna Msaidizi (ACP), Japhari Muhamed,
alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 10 jioni wakati
wanafunzi wakiwa mapumziko, ambako wawili hao walipanda juu ya mwembe
kwa lengo la kutafuta maembe.
Alisema kuwa wakati wanafunzi hao wakiwa juu ya mwembe, ghafla
walianguka wote na Hamimu kupasuka kichwa na kufariki papo hapo, huku
Baraka Ramadhani akivunjika mkono na mguu.
“Mti waliokuwa wameupanda ni mkubwa na mrefu, hivyo walikuwa
mbali sana na ndio maana walipoanguka mmoja akafariki na mwingine
kuvunjika,” alisema Kamanda Muhamed.
Alisema kuwa mwili wa marehemu tayari umeshakabidhiwa kwa ndugu
zake kwa ajili ya taratibu za mazishi, wakati majeruhi amelazwa
hospitali ya Mkoa Maweni kwa matibabu.
Kamanda Muhamed, amewataka walimu na wazazi kwa ujumla kuwa
waangalifu kwa wanafunzi ili kuwaepusha na michezo ambayo ni hatarishi
kwa maisha yao.
No comments:
Post a Comment