WAKAZI wa kijiji cha
Mbegasera wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, wameshindwa kuzuia furaha
yao na kuamua kusakata muziki baada ya umeme kufika kijijini hapo na
wananchi kuunganishwa kwenye nyumba zao, ambazo walilazimika kuezua
sehemu ya nyasi na kuezeka kwa bati ili kufungiwa nishati hiyo.
Hayo yalionekana hivi
karibuni wakati Watendaji wakuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA),
walipotembelea maeneo mbalimbali nchini kuangalia utekelezaji wa miradi
ya umeme vijijini wanayosimamia.
Msafara wa REA ulipopita
kwenye kijiji hicho, ulishuhudia moja ya nyumba iliyoezekwa kwa nyasi na
kuezuliwa sehemu kidogo na kisha kuezekwa kwa bati, ikiwa imeunganishwa
umeme na unawaka, hivyo kuwafanya wanakijiji hao kuserebuka kwa
kucheza.
"Tunacheza sisi tuna furaha
ya umeme, hatukuwahi kuuona hapa kwetu, hadi uende mjini ndio kuna
umeme, lakini sasa tunao acha tusarebuke, wala hatuleti ugomvi na mtu
hapa", alisema Zanisha Kawaya mkazi wa eneo hilo.
Alisema wakati mradi huo
unaanza kutekelezwa kijijini hapo, wananchi waliambiwa umuhimu wake na
kuhamasishwa kujiandikisha kwa wale wanaotaka kufungiwa umeme, kwa kutoa
shilingi 27,000 na mradi ulipokamilika walipata umeme.
Awali Mkurugenzi wa Huduma
za Ufundi wa REA, Bengiel Msofe alisema hadi sasa wananchi 248 wa vijiji
vinne vya wilaya ya Kilosa wameunganishiwa umeme kupitia mradi wa
nishati vijijini, unaotekelezwa na wakala huyo.
Alisema lengo la
kuwaunganisha wateja 300 wa vijiji hivyo vinne ambavyo ni Kisanga,
Mbegasera, Msolwa na Kibaoni ambavyo wateja hao 300, wanaunganishiwa
nishati hiyo kwa gharama ya bei ya ruzuku ya shilingi 27,000 tu badala
ya ile ya kawaidia ya Sh 139,000.
No comments:
Post a Comment