Friday 3 October 2014

MBUNGE KIGOLA AGEUKWA NA WAPIGA KURA MBELE YA WAZIRI NYALANDU

Kigola akifurahi kabla kibao hakijageuka
Nasifiwe Ponziano Miwoo mbele ya Waziri Nyalandu alipokuwa akihoji uadilifu wa mbunge wa Mufindi Kusini, Mendrad Kigola

SAKATA la  vibali vya uvunaji miti katika msitu wa Taifa wa Sao Hill Mufindi mkoani Iringa limemuweka pabaya mbunge wa  jimbo la Mufindi kusini Mendrad Kigola baada ya wapiga kura  wake kumgeuka mbele ya  waziri maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu  kuwa mbunge huyo ni mchochezi katika  sakata  hilo.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Igowole juzi Kigola alimkaribisha waziri huyo huku akikosoa mgao wa vibali vya kuvuna miti katika msitu wa Taifa wa saohill ambao sehemu yake upo katika jimbo hilo, ulivyofanywa kwa vikundi vya wajasiriamali wa wilaya ya Mufindi.
Huku akipigiwa makofi ya mara kwa mara yaliyomfanya ashindwe kusimama sehemu moja wakati akiongea, Kigola alisema: “sina pingamizi dhidi ya watu na vijiji vilivyopata mgao wa mwaka huu.”
“Shida yangu ni mgao uliotolewa kwa vikundi vya wilaya ya Mufindi yenye majimbo mawili. Wakati jimbo langu la Mufindi Kusini vimepata vikundi 12 kati ya 48, vingine vyote vilivyobaki vimetoka upande mwingine. Mheshimiwa waziri, nakuomba ulione hilo,” alisema.
Kauli ya Kigola ilitafsiriwa na baadhi ya watu waliokuwepo katika mkutano huo kwamba ilikuwa ikimpiga vijembe mbunge wa jimbo jirani la Mufindi Kaskazini, Mahamudu Mgimwa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.
Taarifa zisizo rasmi kutoka ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mufindi zinadai kwamba Mgimwa na Kigola hawapikiki chungu kimoja ikiwa ni matokeo ya kinachoelezwa na walio jirani na wabunge hao kwamba mmoja wao ana wivu wa kisiasa dhidi ya mwenzake.
Taarifa hizo zisizo rasmi ambazo hata hivyo hazijawahi kutolewa ufafanuzi na Kigola mwenyewe zinadai kwamba amekuwa akimuonea wivu Mgimwa baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Naibu Waziri.
Wivu huo ndio umepelekea kuchochea chokochoko ya kuhoji uwiano wa mgao wa vibali vikiwemo vibali 48 vilivyotolewa kwa vikundi 48 vya wilaya ya Mufindi.
Hoja ya Kigola dhidi ya mgao wa vibali hivyo ilionekana ina mashiko kwa muda wote wa mkutano huo mpaka pale Waziri Nyalandu alipotoa ruksa kwa wananchi wa kijiji hicho cha Igowole kuuliza maswali.
Alikuwa Nasifiwe Ponziano Miwoo aliyechafua hali ya hewamara baada ya kupata nafasi ya kuuliza swali alilotoa kwa mtindo aliodai wa kujenga hoja ili wananchi wamuelewe.
Akinukuu vifungu kadhaa vya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano huku akioanisha na uadilifu wa mbunge huyo Miwoo alisema:
“Kuna haja ya kuoanisha hoja za mbunge huyu Kigola na uadilifu wake; na kuna haja ya kujua mali zinazomilikiwa na mbunge huyu ili tuone kama kunasababu kwa familia yake kupata kibali cha kuvuna miti wakati baadhi ya vijiji na vya wilaya ya Mufindi na wajasiriamali wake wakikosa,” alisema.
Alisema katika orodha ya wanufaika na vibali vya mwaka huu, jina namba 388 ni la mtoto wa Kigola anayesoma katika moja ya shule bora zilizoko wilayani Mufindi.
Alisema zipo dalili kwamba Kigola alitumia jina la mwanae huyo kupata kibali hicho jambo linalojenga mashaka dhidi ya uadilifu wake.
“Mheshimiwa Waziri tuna mashaka na huyu mtu na kama kila mwaka anajaza fomu inayoonesha mali anazomilikia. Kwanini jina la mwanae litumike,” Miwoo alisema huku waliokuwa wakimshangilia Kigola wakigeuza kibao na kumshangilia yeye.

No comments:

Post a Comment