Ripoti
kuhusu utumizi wa madawa ya kusisimua misuli michezoni, miongoni mwa
wanamichezo nchini Kenya, imebainisha kuwa idadi kubwa ya wanariadha wa
Kenya wanatumia madawa hayo yaliyoharamishwa.
Kwa mujibu wa ripoti
iliyotolewa hii leo na waziri wa michezoi nchini Kenya, jumla ya
wanamichezo thelathini na saba kutoka Kenya wamepatikana na hatia na
miongoni mwa michezo iliyoathirika zaidi ni riadha, raga, soka,
unyanyuaji wa uzani na table tennis.Mwenyekiti wa kamati hiyo ya uchunguzi Profesa Moni Wekesa amesema tatizo hilo ni kubwa na linahitaji suluhisho la haraka.Amesema miongoni mwa madawa yanayotumiwa zaidi ni bangi, mirraa na 'Steroids.'
Aidha ripoti hiyo imenadi kuwa makocha na meneja wa kigeni ndio wanaowapa wanariadha madawa hayo ili kuandikisha matokeo bora katika mashindano ya kimataifa.
Waziri wa Michezo nchini Kenya, Hassan Wario naye ameilaumu shirikisho la mchezo wa riadha nchini kwa kutowajibika.
Kati ya wanamichezo 37 waliopatikana na hatia ya kutumia madawa hayo yaliyoharamishwa 31 ni wanariadha.
Hata hivyo waziri huyo amesema baadhi ya wanariadha hao walitumia madawa hayo bila kujua, akitoa mfano wa mwanariadha Lydia Cheromei ambaye alipigwa marufuku kwa muda licha ya kuwa alikuwa amepewa dawa za uzazi na wala sio dawa ya kuongeza nguvu.
Shirikisho la riadha nchini humo pia limeshutumiwa kwa kutoimarisha mikakati ya kupambana na utumizi wa madawa hayo, kwa kutoa mafunzo kwa wanariadha wake na pia kwa kutoa vibali vya kuwaruhusu mawakala wa kigeni kupiga kambi nchini humo, bila kufuata masharti yaliyopo.
Kinyume na taasisi zingine za michezo, shirikisho la riadha nchini Kenya lilisusia uzinduzi wa ripoti hiyo, hali iliyozua shaka kuwa huenda wao hawaiungi mkono.
Mbali na wanariadha, wachezaji wa soka, pia walishutumiwa kwa kutumia miraa na bangi. Mwenyekiti wa shirikisho la mchezo wa soka nchini Kenya, Sam Nyamweya amekiri kuwa wachezaji wengi wa timu ya taifa na wale wanaoshiriki ligi kuu baadhi yao huvuta bangi kabla na baada ya mechi.
Wakati huo huo serikali ya Kenya imetangaza mpango wa kubuni shirika maalum litakalokuwa na jukumu la kupambana na utumizi wa madawa ya kusisimua misuli michezoni.
Waziri wa michezo amedokeza kuwa shirika hilo litashirikiana kwa karibu na shirika la kimataifa la WADA, kujenga kituo maalum ambacho kitatumia kupima sampuli za wanamichezo wote.
Kuhusu usajili wa maagenti wa kigeni, serikali imeipokonya shirikisho la mchezo wa riadha nchini kenya, idhini ya kutoa leseni na badala yake, maagenti wote wa kigeni watalazimika kutuma maombi yao upya kwa wizara ya michezo, kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi.
No comments:
Post a Comment