Stori: Erick Evarist, Musa Mateja na Chande Abdallah
MTIFUANO!
Tamasha la Serengeti Fiesta 2014 limepita lakini nyuma yake limeacha
vita nzito iliyowahusisha mafahari wawili, Nasibu Abdul ‘Diamond’ na Ali
Kiba huku waandaaji wa tamasha hilo, Clouds FM wakisigana na Times FM
kumgombea msanii wa Nigeria, David Adedeji Adeleke ‘Davido’, Risasi
Mchanganyiko linakupa mchongo kamili.
TIFU LILIVYOKUWA
Kwenye shoo hiyo iliyofanyika
wikiendi iliyopita katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini
Dar, mashabiki wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Ali Kiba (Team Kiba),
walipiga kelele za ‘buuu’ pale alipopanda Diamond kutumbuiza ili
kumharibia.
CHANZO CHANENA
Chanzo makini kimedai kuwa,
vurugu hizo hazikutokea kwa bahati mbaya bali zilipangwa na wafuasi wa
Kiba ambapo inasemekana ziliandaliwa gari aina ya Toyota-Costa zipatazo
25 zilizokuwa zimejaa watu na kwenda kuwamwaga viwanjani hapo kwa
shughuli mbili muhimu; kuzomea na kuhamasisha wengine wazomee pindi
Diamond atakapopanda jukwaani.
“Ishu ilipangwa, Team Kiba waliibuka na Costa kama 25 hivi,
wakajipanga katika maeneo tofauti ya uwanja huo lakini zaidi walikaa
karibu na jukwaa ili kuweza kutimiza vizuri azma yao ya kuharibu pindi
Diamond atakapokuwa akitumbuiza,” kilidai chanzo hicho.
WALIFANIKIWA?
Kwa namna moja mashabiki hao
walionekana kufanikiwa kwani waliweza kuwashawishi watu wengi wazomee
kiasi cha kumfanya Diamond ashtukie na kuamua kutamka hadharani:
“Jamani kuna uhuni unaendelea hapa.”
TEAM DIAMOND WACHARUKA
Madai yanasema mara baada
ya Team Kiba kufanya vurugu hizo na kufanikiwa, baadhi ya mashabiki
ambao waliaminika ni wa Diamond (Team Diamond), walicharuka na kusema
hawakubaliani na uhuni huo ambao umefanywa hivyo watahakikisha
wanapambana kulipiza kisasi kwa namna yoyote ile.
“Hatukubali, wao
si walijipanga hapa kumharibia Diamond, sasa na sisi tutahakikisha
tunalipiza kisasi kwa namna yoyote,” walisikika wakisema mashabiki wa
Diamond.
TALE AKIRI KUSIKIA
Paparazi wetu aliwatafuta
Diamond na Kiba ili kujua wanazungumziaje vurugu hizo. Baada ya
kumtafuta Diamond bila mafanikio, alipatikana meneja wake, Hamis
Taletale ‘Bab Tale’ ambaye alikiri kuwepo kwa maandalizi ya zomeazomea
ambayo yalikuwa na lengo ya kumharibia msanii wake.
“Hizi kwetu tumezichukulia kama changamoto, tulisikia kwamba kuna
watu wamelipwa kwa ajili ya kufanya fujo lakini hatukujali sana kwani
lengo letu si kugombana na mtu, sisi tunafanya muziki mzuri ambao ndoto
zetu ni kuufikisha katika levo za Kimataifa,” alisema Bab Tale.
KIBA ANAHUSIKA?
Alipotafutwa Kiba kuzungumzia
suala hilo alikataa kuhusika nalo na kudai halina ukweli wowote kwani si
rahisi kuwalipa pesa mashabiki wengi kiasi kile waliojitokeza uwanjani.
“Hiyo si kweli ni uzushi tu, sasa mimi nitawalipa nini hao mashabiki
wote waweze kumzomea huyo Diamond? Siyo rahisi. Kwanza mimi nifanye
hivyo ili iweje? Mimi si mtu wa kushindana na Diamond hata siku moja,
nafanya muziki wangu, mashabiki wanauelewa, nashukuru Mungu kwa hilo,”
alisema Kiba.
CLOUDS FM VS TIMES FM
Kwa upande mwingine, vita
nzito ilizidi kutokota kupitia tamasha hilo baada ya msanii Davido
kupanda jukwaani na kutumbuiza ilhali akiwa amewekewa pingamizi la
kibali kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) sambamba na zuio la
Mahakama ya Kisutu lililowekwa na Redio Times FM waliodai kuwa na
mkataba wa kufanya shoo na msanii huyo Novemba, mwaka huu Bongo.
TIMES WANASEMAJE?
Mkurugenzi wa Redio Times FM,
Rehure Nyaulawa alipotafutwa kwa simu kuhusiana na suala hilo alisema
mahakama ilishaweka pingamizi, anashangaa kuona msanii huyo alipanda
jukwaani lakini akasema hawezi kukaa kimya, atakwenda mbele zaidi ili
haki itendeke.
CLOUDS JE?
Kwa upande wao, Clouds walipotafutwa
hawakupatikana hewani lakini kimsingi na wao wana hoja zao ambazo
zitabainika pindi kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.
Hata hivyo, kuna madai kwamba, zuio la Davido kutopanda jukwaani
Leaders Club lilipelekwa na mahakama kwa Clouds Media Group wakati
Tamasha la Fiesta linaandaliwa na Kampuni ya Primetime Promotion, kwa
hiyo barua hiyo ilikuwa ‘missing in action’.
No comments:
Post a Comment