HII NDIO HISTORIA YA MAISHA MBWIGA WA MBWIGUKE
Na Maregesi Paul
SIKU moja nilikuwa katika mkutano wa Jukwaa la Wahariri ambao mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginard Mengi.
Katika mazungumzo yake, Mengi aligusia historia ya maisha yake ambapo alisema alikulia katika familia masikini.
Kwa
mujibu wa Mengi, nyumba aliyokulia ilikuwa na panya wengi pamoja na
mende na kwamba kila walipokuwa wakilala usiku, wapita njia walikuwa
wakiwaona kwa sababu nyumba ilikuwa imejaa matobo.
Pamoja
na mazingira hayo, Mengi kwa sasa ni kati ya matajiri wakubwa
wanaoheshimika ndani na nje ya nchi na suala la umasikini aliokulia,
limebaki kuwa historia.
Hivyo
hivyo, hata mimi niliyeandika makala haya, niliwahi kuvua dagaa na
sangara kwa kutumia nyavu haramu ziitwazo makokoro. Lakini sasa mimi ni
mhariri wa gazeti hili na suala la uvuvi, limebaki katika historia.
Wakati
hayo yakitokea, katika Radio Clouds kuna watangazaji wengi wanaovuta
masikio na hisia za wasikilizaji kutokana na lugha na vichekesho
wanavyovitumia pindi wanapokuwa studio.
Miongoni mwao ni Said Seleman maarufu kwa jina la Mbwiga wa Mbwiguke.
Mbwiga
wa Mbwiguke (kuli) akipozi na Shaffih Dauda kwenye moja ya mechi
iliyoihusisha timu ya mpira ya Clouds Media Group maarufu kama ‘The
Dream Team’
Kama
ilivyo kawaida kwa watu kuwa na historia tofauti tofauti kama
nilivyoeleza hapo awali, wakati wa mahojiano maalum na MTANZANIA
Jumatatu, Mbwiga anaeleza kwa kirefu ni wapi alikotokea hadi akawa mmoja
wa watangazaji maarufu katika radio hiyo maarufu nchini.
“Kwanza
nianze na maana ya jina Mbwiga. Mbwiga ni neno la kizaramo ambalo maana
yake ni rafiki. Kwa hiyo mimi ni rafiki wa kila mmoja kwa sababu huwa
napenda sana kuwachekesha watu.
“Lakini pia, maisha ni mzunguko na kamwe hakuna binadamu anayezaliwa na kujua maisha yake yatakuwaje kwa siku zijazo.
“Kwa
maana hiyo, hiki nitakachokieleza ndivyo kilivyo kwa sababu hapa nilipo
sikutarajia kama itatokea siku nikawa mmoja wa watu wanaoungwa mkono na
mamilioni ya Watanzania.
“Kwanza
kabisa niseme tu kwamba, mtu aliyenifikisha hapa ni mtangazaji
mwenzangu aitwaye Shafii Dauda. Huyu ndiye aliyenileta Clouds baada ya
kuniona naweza kuwa na mchango fulani fulani katika redio yetu hii.
“Sikumbuki
ni mwaka gani, lakini nakumbuka ni kama miaka mitatu iliyopita, siku
moja usiku nilikuwa pale Muhimbili Shule ya Msingi kwenye mazoezi ya
mpira unaowahusisha wachezaji wakongwe kama akina Akida Makunda, Mohamed
Binda, Idd Moshi, Ally Mayai, Crement Kahabuka, Dua Said na wengineo
wengi .
“Siku
hiyo nilikuwa sichezi bali nilikuwa shabiki tu nikiwashangilia wenzagu,
kwa hiyo, mazoezi yalipomalizika, Shafii Dauda alikuja mahali
nilipokuwa na akina Ally Mayai na alitukuta tunacheka,” anasema Mbwiga
na kuongeza.
“Alipoona
tunacheka, akauliza tunacheka nini, Ally Mayai akamwambia huyu jamaa
anatuchekesha, hebu mchukue umtumie kwenye kipindi chako kile cha
michezo cha saa tatu usiku atakusaidia sana,” anasema Mbwiga.
Kwa mujibu wa Mbwiga, Shafii alikubali na hapo ndipo ukawa mwanzo wa safari yake kujiunga na Radio Clouds.
Anasimulia
kwamba, baada ya kukubaliwa, Shafii akawa anampigia simu ili aripoti
matukio mbalimbali ya michezo na kwamba taarifa hizo alikuwa akiziripoti
katika mazingira magumu.
“Wakati
mwingine nilipokuwa nikiripoti, kuna wakati Shafii alikuwa akinipigia
simu nikiwa kwenye daladala, kwa hiyo, nilikuwa nikilazimika kushuka ili
nitafute sehemu nzuri iliyotulia ili nirekodi kipindi.
Mtangaaji wa Clouds Fm, Mbwiga wa Mbwiguke (kushoto) akipozi na shabiki wake Imani Ntila.
“Jambo la kuwaeleza wapenzi wa Radio Clouds ni kwamba, wakati ule nilipokuwa nikirekodi kipindi na Shafii, nilikuwa nikifanya kazi pale Uwanja wa Azamu kule Chamazi. Kule Azam nilikuwa nikisafisha uwanja kwa kuokota vyuma na chupa za maji zilizokuwa zikitupwa wakati wa ujenzi na zilizokuwa zikitupwa na wachezaji walipokuwa wakifanya mazoezi.
“Jambo la kuwaeleza wapenzi wa Radio Clouds ni kwamba, wakati ule nilipokuwa nikirekodi kipindi na Shafii, nilikuwa nikifanya kazi pale Uwanja wa Azamu kule Chamazi. Kule Azam nilikuwa nikisafisha uwanja kwa kuokota vyuma na chupa za maji zilizokuwa zikitupwa wakati wa ujenzi na zilizokuwa zikitupwa na wachezaji walipokuwa wakifanya mazoezi.
“Lakini
kumbuka kwamba, pale Azam nilikwenda kuomba kazi za uselemala,
nilipokosa hiyo kazi, nikaangukia katika kusafisha uwanja kama
nilivyokwambia.
“Kwa
maana hiyo, kuna wakati nilipokuwa nikitakiwa kurekodi kipindi na
Shafii, nilikuwa nikijificha kwenye majukwaa chini kabisa kwa sababu
kule pametulia kweli kweli.
“Nilipokuwa
nikifanya hivyo, wenzagu niliokuwa nikifanya nao usafi walikuwa
wakilalamika kweli kwa sababu waliamini nategea kazi, kumbe mwenzao
nilikuwa naandaa maisha,” anafafanua Mbwiga.
Mbwiga Mbwiguke akiwatuliza wanachama wa Yanga waliojitokeza kwenye mkutano mkuu wa klabu hiyo mwaka huu.
Baada
ya kufanya kazi hiyo kwa miezi kama mitatu hivi, anasema baadaye Shafii
aliamua kumpeleka ofisini kwao Mikocheni Dar es Salaam ambako alianza
kutangaza akiwa studio.
Alipofika
ofisini hapo, anasema alikutana na mmiliki wa radio hiyo, Joseph Kusaga
ambaye alisoma naye Shule ya Msingi Forodhani (zamani St Joseph).
“Siku
moja baada ya kuanza kutangaza, ilifanyika sherehe ya wafanyakazi wote
ambapo MC alinipa fursa ya kuzungumza. Hapo nilimshukuru bosi Kusaga kwa
kumwambia amenipa nyavu badala ya samaki, hivyo ni wajibu wangu
kuendelea kuvua,” anasema Mbwiga.
MAISHA YAKE KAZINI
Mbwiga
anasema baada ya kuanza kazi rasmi, anasema alikutana na changamoto
nyingi ambazo ni pamoja na kutakiwa kujua mambo mengi yanayotokea
duniani.
Pia
anasema kwa kiasi fulani amefanikiwa kufikia malengo kwa kuwa pamoja na
kutangaza katika kipindi cha michezo cha saa tatu usiku, hivi sasa
anashiriki katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa kila siku
asubuhi.
“Nashukuru
kwa sababu sasa niko katika vipindi viwili, yaani kile cha usiku na cha
asubuhi na nadhani wakubwa wangu wameniongezea majukumu baada ya kuona
nina msaada fulani kiofisi.
“Jambo
la kushangaza ni kwamba, wakati naanza kutangaza Power Breakfast, moyo
uliuma sana, yaani niliogopa kwa sababu sikujua kama ningeweza
kufanikiwa.
“Lakini
Jerad Hando alinitoa hofu, akaniambia usiogope, hakuna kitu kipya,
nikamuelewa na mwishowe nikawa nimefanikiwa,” anasema.
Mbwiga Mbwiguke (kulia) akiwa na mdau wa michezo
MAISHA YAKE KWA SASA
Mbwiga
anasema kwa sasa anaonekana mtu wa maana mtaani kwake anaokoishi
Magomeni Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla tofauti na alivyokuwa
mwanzo.
“Maisha
yangu yamebadilika sana mtaani kwetu na jambo jingine ninaloshukuru ni
kwamba, nina marafiki wengi na nafahamika kila mahali.
“Yaani hata Rais Kikwete ananifahamu kwa jina kwa sababu mwaka jana nilifuturu naye Ikulu tukiwa naye meza moja.
“Hata
hivi karibuni tulikutana naye kwenye tamasha la wasanii kule Dodoma na
aliponiona, aliniita kwa jina akaniambia, Mbwiga hujambo, nilimjibu,
sijambo mheshimiwa, msimu wa embe nyani hakondi, halafu akacheka,”
anaeleza.
HISTORIA KIFAMILIA
Anasema
yeye ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia yao akitanguliwa na kaka
yake aitwaye Nassor Fadhir anayeishi jijini Cologne, nchini Ujerumani.
MALENGO YAKE
Mbwiga
ambaye anapenda kujitambulisha kuwa ni mzaramo, anasema ana mpango wa
kujiendeleza kielimu ili aweze kuitumikia vizuri kazi yake.
“Elimu yangu siyo kubwa sana ila nimesoma pale VETA Chang’ombe kwa miaka miwili na kutunukiwa cheti cha ujenzi wa barabara.
“Baadaye
nilijiingiza katika masuala ya ufundi selemala, kwa hiyo, naweza kusema
mimi ni fundi selemala mzuri wa fenicha zote za ndani.
“Ili
niweze kwenda na wakati, niko katika mikakati ya kujiendeleza kielimu
kwa sababu hata wafanyakazi wenzangu wamekuwa wakinihimiza juu ya hilo,”
anasema.
Katika
mazungumzo yake, anawashukuru wafanyakazi wenzake wote na kuwataja
baadhi kwa majina kuwa ni Joseph Kusaga, Ruge Mutahaba, Joyce Shebe,
Shafii Dauda, Gerad Hando, Maestro, Alex Luambano, Bonge, PJ na
Simalenga.
“Nimewataja hao, lakini lazima umuweke Babra Hassan, yaani usipomtaja huyo, ataninunia mpaka basi,” anatania Mbwiga.
No comments:
Post a Comment