Tuesday, 26 August 2014

KWANI LULU BADO ANA KESI YA KUJIBU?NILIJUA ISHAISHA..Poaa


Kesi Ya Kanumba Na Lulu Yasikilizwa Kimya Kimya

Baada ya kimya cha muda mrefu, imefichuka kwamba kesi ya kuuawa kwa aliyekuwa staa mkubwa wa sinema za Kibongo, marehemu Steven Charles Kanumba  imechukua sura mpya baada ya kuanza kusikilizwa kimyakimya.
WATU WANATAKA KUJUA KINACHOENDELEA

Uchunguzi umebaini kwamba watu wengi wana kiu ya kujua kinachoendelea katika kesi hiyo ambapo ilidaiwa kwamba imehamishwa eneo la wazi (open) na kusikilizwa kimyakimya katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, huku usikilizwaji wa kesi hiyo ukiwa tofauti kama ilivyozoeleka.

Kwa mujibu wa shushushu mmoja anayependa kufuatilia maisha ya mastaa wa tasnia tofautitofauti Tanzania ndani ya mahakama hiyo, akichonga na Globalpublishers alisema kuwa chombo hicho cha kusimamia sheria kimeamua kubadili aina ya usikilizaji wa kesi hiyo.
YAHAMISHIWA BARAZA LA KESI ZA MAUAJI

Habari zilieleza kwamba, kwa sasa kesi hiyo itakuwa ikisikilizwa kwenye kikao cha baraza la kusikiliza kesi za mauaji kwenye mahakama hiyo, kwa lugha ya kigeni kinaitwa High Court Murder Session.

“Kama ukienda pale mahakamani ili kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo, huwezi kufanikiwa kupata chochote kwa sababu ipo kwenye baraza la kusikiliza kesi za mauaji yaani High Court Murder Session ambalo huwa linasikiliza kesi kimyakimya tofauti na kesi nyingine zinazosikilizwa kwenye kizimba,” kilisema chanzo hicho.

ETI LULU HAJUI KINACHOENDELEA

Uchunguzi wetu ulibaini kwamba wakati hayo yakiendelea kortini hapo, aliyekuwa mwandani wa Kanumba aliyekuwa naye chumbani siku ya kifo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ hajui chochote kinachoendelea na wala hajaitwa mahakamani.

“Tangu imeanza kusikilizwa hakuna siku Lulu ameitwa na sidhani kama anajua kinachoendelea.

“Labda anayejua kinachoendelea ni mama Kanumba (Flora Mtegoa) ambaye hupenda kuulizia kuhusu hatima ya mwanaye,” kilisema chanzo hicho.
WAKILI KIBATALA ANASEMAJE?

Baada ya kujikusanyia data hizo, Globalpublishers kuptia gazeti la Ijumaa Wikienda ilimtafuta wakili maarufu nchini anayemtetea Lulu, Peter Kibatala ili kupata ufafanuzi wa aina hiyo ya usikilizwaji wa kesi ya mteja wake ambapo alifichua siri hiyo juu ya kesi ya kifo cha Kanumba.

Wakili Kibatala alikiri kwamba kesi ya kifo cha Kanumba ambayo Lulu ni mshitakiwa wa kwanza akituhumiwa kuua bila kukusudia, imebadilishwa aina ya uitwaji huku akigoma kuingia kiundani kwani bado kesi hiyo ni mbichi na hairuhusiwi kwa wakili kuzungumza nje ya mahakama.

“Ni kweli inaitwa hivyo, huyo aliyekueleza hajakosea na tunategemea mwezi huu wa nane kikao cha baraza hilo la usikilizaji kitaendelea lakini nisingependa kuongea sana kwani mimi siyo msemaji wa Lulu bali ni wakili na si maadili ya kazi yangu kuzungumza nje ya mahakama. Hata Lulu haruhusiwi kuzungumza chochote nje ya mahakama,” alisema Kibatala aliyewahi kuwa wakili wa mwigizaji Kajala Masanja na mwanahip-hop, Waziri Makuto ‘Lord Eyez’.
LULU SASA

Mwanahabari alipomtafuta Lulu ili kujua kama anajua chochote juu ya kesi hiyo, mkali huyo wa sinema za kitanzania aligoma kuzungumza chochote kama aliyoelekezwa na wakili wake, Kibatala.
TUJIKUMBUSHE

Kanumba aliyewatoa mastaa wengi wa filamu unaowaona kwa sasa, alifariki dunia April 7, 2012 nyumbani kwake, Vatican-Sinza jijini Dar. Kifo cha Kanumba kilidaiwa kwamba kilitokana na kuangukia sehemu ya nyuma ya kichwa ambapo alipata mtikisiko wa ubongo kisha kuzikwa kwenye Makaburi ya Kinondoni, Dar.

No comments:

Post a Comment