Clouds FM Yapewa Onyo na Kupigwa Fine Kwa Kukiuka Kanuni za Utangazaji
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),
imetoa onyo pamoja na kutoza faini ya takribani Sh milioni 5 kwa kituo
cha redio na televisheni cha Clouds, kwa kukiuka kanuni za utangazaji za
mwaka 2005.
Wakielezea uamuzi huo jana jijini Dar es
Salaam, Kamati ya Maudhui ya mamlaka hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti
wake, Margaret Munyagi ilisema kuwa ukiukwaji wa kanuni hizo ulifanywa
kwa nyakati tofauti na vituo hivyo.
Alisema kwa upande wa kituo cha redio
cha Clouds, kupitia kipindi chake cha ‘Njia Panda’ kilichorushwa hewani
Juni 15 mwaka huu kati ya saa 8.00 mchana na saa 10.00 jioni kilikuwa na
mada iliyohusu safari ya kuzimu ambapo maudhui yake yalijaa simulizi za
kufikirika, za kishirikina na kichawi.
Aidha alisema kosa lingine kituo hicho
hakikufuata kanuni za Utangazaji(maudhui) za mwaka 2005 zinazowataka
kuwasilisha ratiba ya vipindi vyao kwa TCRA ili viidhinishwe na vilevile
kuvichapisha katika gazeti kabla ya kurushwa hewani ambapo kipindi cha
Njia Panda hakikuwasilishwa kwa ajili ya kuidhinishwa.
Wakati huo huo, kituo cha televisheni
cha Clouds kilirusha kipindi cha ‘Bibi Bomba’ Mei 16 na Juni 6 mwaka huu
kati ya saa 3.00 na saa 4.00 usiku ambacho kilikiuka kanuni za
Utangazaji (maudhui) za mwaka 2005.
Alisema kipindi hicho kilidhalilisha
mabibi hao walioshiriki pamoja na wanawake kwa ujumla kutokana na
maswali ya aibu waliyokuwa wakiulizwa na waamuzi wa shindano hilo ambayo
ni kinyume na kanuni hizo.
Aidha alisema kituo hicho kinatozwa
faini ya Sh milioni moja na kutakiwa kuwasilisha TCRA mwongozo wa
kuchuja na kusimamia maudhui yasiyofaa kabla ya kutangazwa.
TCRA imesema kama Kanuni za Utangazaji zitaendelea kukiukwa hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
No comments:
Post a Comment