SAUTI KUTOKA NYIKANI.... MULUGO, MWANASIASA MREFU KAMA UTAJIRI WA CHUNYA MBEYA
MBUNGE WA JIMBO LA SONGWE PHILLIPO MULUGO.
NA GORDON
KALULUNGA
MWAKA 2011,
Mwandishi Mubelwa Bandio, aliwahi kuandika kuwa, anatamani angekuwepo Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere ili ayaone yanayotendeka hivi sasa.
Alisema
tamaa yake ni kuhusu uchumi wa dunia unakoelekea na namna mataifa yanavyochukua
umiliki wa uendeshaji wa shughuli muhimu za kiuchumi kisha anaishia kujiuliza
kama hii si sehemu ama aina mpya ya ujamaa?
“Kama Baba
wa Taifa Mwl Nyerere angekuwepo, basi angeweza kurejea kusema mawili matatu
ambayo alishawahi kusema miaka kadhaa iliyopita na ambayo yamekuwa katika
hotuba zake na nukuhu zilizopo sehemu mbalimbali” anasema Mubelwa.
Anaendelea
kwa kusema kuwa, anatamani angekuwepo akaona viongozi wetu wa sasa ambao
hawawezi kusimamisha mapigano mpaka watishiwe na mataifa fulani, ama wawekewe
vikwazo na fulani.
Katika
andiko la makala yangu wiki iliyopita ukurasa huu, kuhusu baadhi ya wajumbe wa Bunge
la katiba kutoka Chadema na kurejea Bungeni, lilileta maoni mengi na
ninawashukuru wasomaji wote waliopiga simu na kutuma ujumbe mfupi wa maandishi.
Kabla ya
Bunge hilo kuisha, nitaleta takwimu ambazo wengi hawataki kuzisikia ili mradi
wahalalishe walichokisikia/wanachokitaka kuhusu serikali tatu, na hapo
nitakumbusha neno “ukweli mchungu” la Mhariri wa Mtanzania Jumapili, Ratifa
Baranyikwa.
Kwa leo
sauti hii inatokea katika nyika ya wilaya ya Chunya mkoani Mbya.
Aliyekuwa
Naibu waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi, Philipo Mullugo, kabla hajaangukiwa
na jumba bovu la uteuzi mpya, alikuwa akionekana mchapa kazi na jambo hilo halina
ubishi, labda ubishi uwe kwenye siasa chafu zinazoendelea kuishi hapa nchini.
Mulugo ni
Mbunge wa Jimbo la Songwe, wilayani Chunya mkoani Mbeya. Mwonekano wake ni
kiongozi kijana, umbile lake ni mwembamba na mrefu wa kutosha.
Katika
wilaya hiyo ya Chunya kuna majimbo mawili ambayo ni Jimbo la Lupa linaloongozwa
na Mbunge, Victor Mwambalaswa na linaloongozwa na Mulugo, liitwalo Jimbo la Songwe.
Historia
inaonesha kuwa wilaya hiyo ndiyo wilaya kubwa kuliko zote nchini Tanzania.
Wilaya hiyo
ina kilomita za mraba zipatazo 29,219 tarafa 4, kata 30 vijiji 73 na idadi
ndogo ya watu wapatao 290,478.
Chunya
ilianzishwa kwenye miaka ya 1948 na wakati huo ikiwa kama makao makuu ya wilaya
ya Mbeya.
Wilaya hiyo
ni moja kati ya wilaya za zamani au za mwanzo na zenye historia kubwa na ya
pekee nchini.
Upekee wake
unaazia kuwa ni wilaya ambayo imesahaulika kimaendeleo licha ya kuwa na
rasilimali nyingi ikiwemo misitu ya mbao na dhahabu.
Enzi za
ukoloni wakati nchi ikijulikana kwa jina la Tanganyika, waingereza walichagua
wilaya ya Chunya kuwa makao makuu ya jeshi la polisi katika eneo la mgodi wa
Saza(mine).
Sababu kubwa
ya kuchagua eneo la mgodi wa Saza au Saza Mine kuwa makao makuu ya polisi katika
koloni la Tanganyika ilikuwa ni kulinda maslahi ya dhahabu.
Sehemu
nyingine za machimbo ya dhahabu katika wilaya hiyo zilikuwa zinasimamiwa na
wakoloni, na maeneo hayo ni Chunya mjini, matundasi na Makongorosi.
Wilaya ya
chunya imepata umaarufu wa kuwa eneo la kwanza hapa nchini kuleta wachimbaji
madini katika maeneo ya Saza na Matundasi kutoka nchi za Northern Rhodesi kwa
sasa Zambia na South Africa yaani Afrika kusini.
Enzi za
ukoloni kabila wa wawemba kutoka Zambia na makaburu(Boers) kutoka Afrika
kusini, ndiyo watu waliokuwa wakifanya kazi za migodini kwasababu walikuwa
ndiyo wataalamu.
Utaalamu wao
unaelezwa kuwa ulitokana na sababu kwamba nchi zao zilikuwa na migodi mingi ya
shaba, dhahabu, Almasi na makaa ya mawe.
Hadi leo hii
ukienda Matundasi, Chunya mjini na Saza utawakuta Wawemba wengi ambao zama hizo
walitoka Zambia na kwa sasa wamebakia kuwa walowezi.
Marais wa
zamani wa Afrika kusini Frederick deKlerk na Pietha Botha wote walizaliwa
katika eneo la mgodi wa Saza wilayani Chunya kati ya miaka 1938 na kuendelea.
Viongozi hao
mashuhuri baadaye walisoma shule katika sekondari ya Iyunga iliyopo Jijini
Mbeya, ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kwa jina la Mbeya European
School(shule ya wazungu) kati ya miaka ya 50.
Rais wa
Zamani wa Namibia Sam Nujoma na akina Thabo Mbeki, wamewahi kuishi Matundasi
katika kambi ya wapigania uhuru iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Tumbu.
Wilaya hiyo
ya Chunya, ndiyo wilaya ya kwanza kuwa na kiwanja cha ndege na huduma za benki
Tanzania, lakini mpaka sasa ni wilaya ya inayoonekana change kati ya wilaya
tisa za mkoa wa Mbeya na wananchi kukosa huduma za kijamii.
Hapa hakuna
mchawi, bali mchawi wa wilaya hiyo ni serikali yenyewe ambayo inaelezwa kuwa
viongozi wengi wa nchi hii ama kwa kuingia ubia na makampuni ya watu wengine,
wanaendelea kuila Chunya.
Wananufaika na
rasilimali za wilaya hiyo hasa upande wa madini aina ya dhahabu na mbao za
asili.
“Kuliwa” kwa
Chunya hakujaanza leo, bali ni miaka mingi tangu enzi za Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere. Sauti hii ya nyikani, ndiyo maana imeamua kufananisha urefu
wa Mbunge Mullugo na utajiri wa mkoa wa Mbeya, ambapo serikali ikiamua, wilaya
ya Chunya itakuwa na maendeleo marefu kama alivyo Mullugo.
Mwandishi anapatikana kwa simu 0754 440749
No comments:
Post a Comment