Saturday 23 August 2014

USOME WARAKA WA MBUNGE GODBLESS LEMA..endeleaaaaa

Godbless Lema Amshushia Waraka Mzito Jakaya 'Heri Kuitwa Mpumbavu Kwa Ajili ya Haki Na Kweli'

Saturday, August 23, 2014

Mh Rais , bila shaka utakuwa unaifahamu vizuri historia ya Farao

Mh Rais nakusalimu .


Ni usiku wa manane wakati naanza kuandika waraka huu , nimetoka kuangalia historia ya maisha ya Dr Martin Luther Jr na nilipotaka kulala nilishindwa na nilipotafakari jambo jema la kufanya wakati huu nilipokosa usingizi ndipo wajibu huu muhimu wa kuandika waraka huu kwako ulipoanza .


Mh Rais , bila shaka utakuwa unaifahamu historia ya Farao na Wana wa Israel wakati Mungu alipotaka kuwatoa wana wa Israel utumwani Misri , kwa wale Wakristo wanaosoma Biblia wanajua kuwa , maandiko yanasema “ Na Mungu akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu ili apate kujitukuza mbele ya wana wa Israel . Mh Rais siwezi kuandika sana juu ya nini kilitokea kwa Farao na Watu wake ila nikuombe sana umuombe Mch G. Rwakatare hakueleze kwa ufasaha ili upate kujifunza jambo muhimu hapa .


Mh Rais , ukiona unafanya au unatenda hila au dhambi bila kipingamizi wala taabu , maana yake ni kuwa mauti kwako yamekaribia kwani mwizi aliyeambiwa kuwa siku zake ni arobaini kama angeacha uovu katika siku ya thelasini na nane pengine angeponywa na wito wa mauti…. Nchi hii haiko salama hata kidogo , hali ni tete sana na kwa bahati mbaya Watawala hamuoni kwani macho yenu yamepigwa upofu na shetani na ndipo andiko laGodbless Lema litatimia “ Na Mungu akaufanya Moyo wa Kikwete na ccm kuwa mgumu ili apate kuikomboa Tanzania “


Mh Rais sina mashaka na Uhuru wa kweli na wa pili wa Taifa ili katika siku chache zinazokuja ,, , hamtaweza kuzuia mabadiliko hata kama wanayoyataka sasa watakufa wote leo , ila kukosa hekima katika uongozi kunaweza kusabisha mabadiliko haya yakaja na hasara kubwa katika Jamii . Hata hivyo kiburi mlichonacho kinasababishwa na wajibu na mipango ya Mungu katika Nchi yetu .


Mh Rais , Watu wameendelea kuteseka kila kona , maisha ni magumu , mfumuko wa bei umepoteza thamani ya fedha , Wagonjwa mahosiptalini wanakufa kwani panadol imekuwa dawa ya kutibu maradhi yote, jela kumejaa masikini na wanyonge na Watu wanaokwepa kodi na kulibia Taifa wamekuwa marafiki wa watawala , ajira hakuna na vijana wamekata tamaa , dada zetu wamekuwa malaya wa kutafuta chakula cha siku na ada ya kuendelea na masomo .


Mh Rais , pamoja na rasilimali tele tulizonazo kama vile dhahabu , Tanzanite , Gesi , Almasi , Mbuga za Wanyama , Madini ya Urani , Mlima Kilimanjaro , Kahawa , Pamba , Korosho , Bandari , Mito na maziwa na vitu vingine vingi , bado vimeshindwa kutoa mwanga wa maendeleo katika Taifa hili .


Mh Rais , Tuko katika kipindi ambacho tunaandika Katiba ambayo wakati Wananchi wanatoa maoni walikuwa na matumaini makubwa . Mtafaruku uliopo sasa ni kati ya UKAWA na ccm , sio vita rahisi hata kidogo lakini Watu wajinga wanaweza kukushauri vibaya na ukafikiri unyenyekevu kwenye jambo hili ni kujidhalilisha , Wewe ni Rais , ukishindwa kutambua Mamlaka yako na nguvu zako katika kusimamia ukweli na haki basi Nchi itakuwa imepoteza dira . Mh Rais unapaswa kushuka na kuwa mnyenyekevu kwani dhamira njema yenye malengo mazuri haiwezi kumdhalilisha binadamu . Wasira . Lukuvi na Werema na wengine watakushauri nakukuambia ukilihairisha Bunge utawapa Kichwa UKAWA na Nchi itaenda Upinzani .


Mh Rais ukiitwa mpumbavu kwa ajili ya haki na kweli , upumbavu huo una maana kubwa kuliko kusifiwa na watu wanaopenda dhuluma na hila hata kama ni wengi , ninahisi changamoto unazopitia kama Rais na Mwenyekiti wa Chama , lakini Mtu Hodari na shujaa ni yule anayeshinda majaribu na taabu wakati usio muaafaka .Nakuomba ufanye maamuzi kwa ajili ya Watoto wa watoto wa Rizwan na Watanzania na sio Chama chako . Chama chako kitakuwepo leo na siku moja hakitakuwepo lakini Watoto na Wajukuu zako watakuwepo . Hivyo basi isaidie Tanzania kupata Katiba ambayo itampa binadamu yeyote haki , usawa na fursa katika Taifa lake.


Mh Rais , karibu kila mtu mwenye akili timamu amesema juu ya jambo hili hakuna atakaye kulazimisha lakini wakati ukifika wakati utakulazimisha , Polisi wetu na Jeshi halitaweza kushindana na kulishinda Jeshi linaloitwa WAKATI , hali itakuwa ni mbaya , Watoto wataitafuta Tanzania na kuikosa , ndipo watu wazima watasema tulikuwa wapi wakati misingi ikiharibika ? zitakuwa ni siku za taabu na uchungu na UKAWA hawatakuwepo tena ila WAKATI watakuwepo na hawatamsilikiza mtu yeyote , nyumba za kifahari na magari yanayokusanywa sasa kwa hila na wizi hayatakuwa makazi ya Watu isipokuwa popo na mende , Marekani , Uchina na Ulaya watawageuka watawaita wahalifu wa demokrasia na wauaji , watawatafuta ,watawakamata na Maisha yenu yatakuwa ya Uchungu mkubwa wakati Nchi haitakuwepo , mimi sio mtabiri kama marehemu Sheikh Yahaya , lakini najua kwamba ukiwa na mwanamke mjamzito ndani ya nyumba ni bora na ni muhimu ukaanza kuandaa vifaa muhimu vya mtoto kama nguo nk .


Mh Rais , sikutishi , ila Mungu hadhiakiwi apandacho mtu ndicho avunacho , najua watakuja wapambe hapa watakuambia umeona ujinga wa yule Mbunge wa Arusha ? watasema ameandika ujinga , watakebehi na kudharau kama kawaida yao . Hata mimi siandiki kutafuta sifa kwani mke wangu na watoto wangu wanatosha kunisifu na kila siku wanafanya hivyo asubuhi na jioni hasa pale ninapowaletea Ice Cream .


Mh Rais , nisikuchoshe sana , ila tafakari tena , natambua mara kwa mara huwa unakuja Arusha lakini sijawahi kuambiwa wala kutaarifiwa pengine ningekuambia haya mambo kwa mdomo na mara nyingi huwa nakutana na msafara wako barabarani na ndipo natambua kuwa huko Jimboni kwangu . Hata hivyo tunaendelea kupambana vizuri kujenga demokrasia ya kweli na Chama chako kinaendelea kudhoofika vizuri sana hapa Arusha na tunatarajia kumaliza uchaguzi Mkuu wa 2015 wa Jimbo letu hili mwaka huu mwezi wa kumi na mbili .



Mh Rais , naomba nitoke nje ya mada yangu muhimu kidogo , matukio ya Ugaidi na mauaji bado yanaendelea hapa Arusha , lakini sina taarifa za ndani sana kwani na siku nyingi kidogo sijatembelea matajiri wa Arusha ambao Rpc anawapa taarifa zaidi za matukio yanayotishia usalama wa Jimbo langu kuliko mimi Mbunge hata kama nikizihitaji kwa barua , ni jambo la kusikitisha lakini ni jaribu ambalo tumeweza kulisitahimili , nitajaribu kwenda kuwaona matajiri hawa siku chache zinazokuja ili nipate taarifa za hali ya usalama ya Jimbo langu na nitakuandikia waraka mwingine kukueleza ukweli , hata hivyo kuna watu waliokamatwa hivi sasa ila kwa vile sina taarifa za kutosha nina shindwa kujua vizuri kama watu ha ni wahalifu au la , isipokuwa ni na imani Mungu , Shetani na Polisi wa Arusha wanajua vizuri .

Mh Rais , nakushukuru na ninakuombea kwa Mwenyezi Mungu wakati unatafakari tena kuhusu mchakato wa Katiba , hata hivyo Watanzania wasiogope kwani “ Na Mungu akaufanya Moyo wa Kikwete na ccm kuwa mgumu ili apate kuikomboa Tanzania “


Godbless J Lema (MB)

No comments:

Post a Comment