Monday 29 September 2014

AFYA: Sumu huathiri waume, watoto wa wanawake wanaotumia mikorogo



“Tunafanya kampeni ya kupambana na vipodozi vyenye sumu kwa sababu tatizo ni kubwa nchini.“Hadi sasa asilimia 52 ya Watanzania hutumia mkorogo. matokeo yake wengi wameathirika na wanashindwa kuacha.” Euphrasia Shayo 
Na Elias Msuya, Mwananchi0
Share

Nuru Masoud, mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, amekuwa akijishughulisha na biashara za vipodozi vya asili, maarufu kama mkorogo.
Hata hivyo, biashara hiyo aliisitisha mwaka 2013 baada ya kupata madhara makubwa ya ngozi ambayo yaliambukiza pia familia yake.
“Nilianza kuwashwa ngozi mfululizo, nikadhani nimeathirika na Ukimwi,” anasema akikumbuka jinsi ugonjwa huo ulivyomtesa.
 “Niliamua kwenda Hospitali ya Muhimbili kwa daktari wa ngozi ambaye alichukua kipande cha ngozi yangu na kwenda kuipima na kubaini tatizo ni mkorogo.”
Nuru anasema alipewa dawa aina ya scaboma ambayo ilimsaidia na inaendelea kumsaidia hadi sasa. Kwa sasa ameachana na biashara hiyo na badala yake anatoa ushuhuda wa madhara ya dawa hizi.
Akizungumzia biashara hiyo, Nuru anasema licha ya kusitisha biashara iliyokuwa ikimpa fedha za kujikimu kimaisha, sasa amekuwa balozi wa kueleza madhara ya mkorogo kwa jamii.
Alianza biashara hiyo mwaka 1998 baada ya kufanya majaribio ya kupaka losheni hizo na kuona zinampendeza na watu wanazipenda na hivyo akawa anachanganya na kuuza.
“Kwa kipimo kimoja nilikuwa nauza kati ya Sh25,000 hadi 30,000 na ningeweza kupata hadi Sh400,000 kwa mwezi,” anasema.
Hata hivyo, mwaka 2013, mambo yalianza kwenda vibaya baada ya kujikuta akiwashwa ngozi na kuharibika ikawa kavu, yenye mikunjo na kubadilika rangi.
Licha ya Serikali kupambana na utengenezaji na matumizi ya vipodozi vyenye sumu, imeelezwa kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania hutumia vipodozi hivyo kwa lengo la kuongeza urembo.
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Evirocare ya Dar es Salaam mwaka 2013 umeonyesha bado tatizo hilo ni kubwa.
Utafiti huo ulifanyika kwa kuhusisha mkoa mmoja katika kanda sita nchini. Mikoa hiyo ni Dar es Salaam ukiwakilisha Kanda ya Mashariki, Mbeya (Kanda ya Nyanda za Juu Kusini), Tanga (Kanda ya Kaskazini) na Dodoma (Kanda ya Kati).

No comments:

Post a Comment