Kuna dalili hali si shwari ndani ya
Bunge Maalumu la Katiba baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kujiuzulu ujumbe wa
Kamati ya Uandishi wa Katiba inayopendekezwa.
Habari za uhakika zilizopatikana jana
bungeni mjini Dodoma, zinaeleza kuwa kigogo huyo wa SMZ amemwandikia
barua Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta akimwarifu juu ya uamuzi
wake huo.
Kamati hiyo ndiyo moyo wa Bunge hilo
katika kuandika vifungu, ibara na sura za rasimu kulingana na
mapendekezo ya kila kamati na baada ya majadiliano na mwisho inawajibika
kuandika Katiba itakayopendekezwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa
kura ya maoni.
Kujiengua kwake ni pigo kwa Bunge
Maalumu, kwani kunapunguza uhalali wa Katiba itakayopendekezwa kwani
Othman akiwa Mwanasheria Mkuu wa upande huo wa Muungano ndiye anayepaswa
kuwa kinara wa kulinda masilahi ya Zanzibar wakati wa uandishi wa
Katiba inayopendekezwa.
“Ni sahihi kwamba nimejiuzulu…hizo
sababu ndiyo siwezi kukutajia maana kwa mujibu wa taratibu za Bunge
Maalumu zinapaswa kuzungumzwa na Mwenyekiti maana barua yangu ya
kujiuzulu anayo yeye,”alisema Othman alipozungumza na gazeti hili
kupitia simu yake ya mkononi jana.
No comments:
Post a Comment