Saturday 11 October 2014

NENO LA SIKU::Siasa madhabahuni zitatufikisha pabaya-Padre Nkwera


Padre Felician Nkwera

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Kiongozi wa Kikundi cha Sala cha Wanamaombi, Padre Felician Nkwera amesema nafasi ya Kanisa katika kuhakikisha mchakato wa kupata Katiba mpya unafanikiwa, ni kufunga na kumwomba Mwenyezi Mungu ili awapatie Watanzania Katiba wanayoitaka.

Alisema ushauri ambao Kanisa linatakiwa kuutoa kwa viongozi wa serikali na vyama vya kisiasa ni kufunga na kusali.

Padre Nkwera alikuwa akijibu maswali kuhusu nafasi ya Kanisa katika kuhakikisha Tanzania inapata Katiba itakayojibu kero za wananchi.

Alisema ni kosa kwa viongozi wa dini kutumia madhabahu yao kuisema serikali pamoja na vyama wa siasa, kinachotakiwa kufanyika ni kuwaita viongozi wa pande zote mbili zinazosigana ili kuzishauri namna ya kufikia mwafaka.

“Kanisa siyo wanasiasa, zamani kazi kubwa ya manabii ilikuwa kumuomba Mungu miongozo yake kwenye masuala mbali mbali.
 
 Manabii walifunga na kumuomba Mungu awape majibu katika masuala ya vita, njaa au shida yoyote iliyolihusu taifa, walimuomba Mungu awasaidie kuwatatulia,” alifafanua.

Kwa sasa Tanzania iko katika mchakato wa kutunga Katiba mpya yenye lengo la kukidhi mahitaji ya wananchi wengi. Katika mchakato huo kumekuwa na mvutano ambao umesababisha mgawanyo wa makundi mawili ya Umoja wa Katiba ya wananchi (UKAWA) na Tanzania Kwanza.

Padre Nkwera alisema nchi itapata Katiba lakini siyo kwa kasi tunayoihitaji sisi kama binadamu. Tanzania ina wenyewe na wao ndio watakaoamua lini Tanzania iwe na Katiba mpya.

“Katiba itapatikana lakini siyo kwa spidi tunayoitaka, itapatikana hata katika kipindi cha awamu inayofuata,”
alisema.
 
Aliwataka Wanamaombi waombe ili Taifa lipate Katiba mpya inayofaa, kwani ni jukumu walilokabidhiwa kuombea mchakato huo ili nchi ipate Katiba mpya katika hali ya utulivu.

Alisema malumbano ya kwenye vyombo vya habari hayatatoa mshindi na badala yake malumbano hayo yataendelea kuivuruga Serikali na kusababisha kutokuelewana kuendelea.

“Jukumu la viongozi wa dini ni kuwashauri viongozi wa Serikali na wale wa vyama vya siasa ili wafikie mwafaka ambao utasaidia kupatikana kwa Katiba ambayo wananchi wanaitamani,” alisema.

Alipoulizwa iwapo Katiba haitapatikana Watanzania wafanye nini, Padre Nkwera alijibu kuwa zamani Waisraeli waling’ang’ania kuwa na mfalme wao kama yalivyo mataifa mengine, Mwenyezi Mungu akawaambia “Nikiwapatia mfalme atawafanya watumwa na atawalipisha kodi, hamtakuwa na amani”.

Waisraeli hawakumsikiliza na badala yake wakaendelea kung’ang’ania mfalme wao, Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Waisraeli hawakupingi wewe bali wananipinga mimi, wapatie mfalme wao”. Mungu aliwapatia Saulo kuwa mfalme wao na toka siku hiyo walikumbuka maagizo ya Mungu.

Akizungumzia suala la upande upi Wanamaombi wasimamie kati ya kikundi kinachojiita UKAWA au Tanzania Kwanza, Padre Nkwera alisema Wanamaombi hawatakiwi kuwa na upande wowote kati ya hizo mbili, wanatakiwa kuwa neutral ndio maana wamepewa jukumu la kuombea mchakato.

Aidha alisema serikali tatu zitabomoa Muungano kwa sababu, serikali ya tatu haitakuwa na sehemu ya kupata mapato yake zaidi ya kutegemea nchi wahisani. 
 
Alisema hatari ya kutegemea mapato kutoka kwa nchi wahisani ni pale nchi moja itakapogoma kutoa fedha kwa nchi ya tatu.

Alisema Tanzania ni nchi ya serikali mbili lakini uroho wa madaraka ndio unaosababisha watake serikali tatu.

Padre Nkwera alisema ili serikali mbili zifanye kazi, Zanzibar haina budi kufunga balozi zote ambazo imeingia nazo uhusiano, iondoe Katiba yake, iondoe bendera na hata wimbo wa Taifa, nchi iwe na bendera moja, wimbo mmoja wa Kaifa na Katiba moja.

Kwa kufanya hivyo Muungano utaendelea kudumishwa vizazi kwa vizazi. 
 
Alitahadharisha kuwa serikali tatu siyo suluhisho la matatizo yaliyopo nchini bali ni kuongeza matatizo na hatimaye kuubomoa Muungano ambapo mwisho wake hautakuwa mzuri.

Source:Jarida kwa wanamaombi:Safina ya Malkia.

No comments:

Post a Comment