Friday, 3 October 2014

SIASA::Picha 3 za jinsi Waziri mkuu wa Uganda alivyonyang’anywa ulinzi nyumbani baada ya kutimuliwa kazi.

ug1
Jana ndio Waziri mkuu mpya wa Uganda Ruhakana Rugunda kaapishwa ila kabla yake alikua ni Amama Mbabazi ambae alifutwa kazi wiki kadhaa zilizopita baada ya kukaa madarakani toka May 2011 akitokea kwenye Uwaziri wa Ulinzi.
September 18 2014 ndio Rais Museveni alimuandikia Spika wa bunge barua kumuarifu kuwa ameamua kumuondoa waziri mkuu huyo na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekua Waziri wa Afya ambae kwa sasa ana umri wa miaka 67.
ug2
Kwa mujibu wa ripota wa TZA (millardayo.com na AyoTV) waziri huyu alietimuliwa alikua Waziri mkuu wa nne toka Rais Museveni aanze kuitawala nchi hiyo January 1986 ambapo mpaka sasa amewahi kuwa na Makamu wa Rais wanaofikia wanne.
Picha zote hizi zinaonyesha wakati Serikali ya Uganda ilipomnyang’anya ulinzi wa Wanajeshi waziri huyu mkuu baada ya kufutwa kazi ambapo kwenye hii picha ya chini anaeonekana ni mke wake akilalamika kwa kutoamini kilichotokea kwani mume wake na Rais Museveni wamekua marafiki wakubwa.
Vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti kwamba kuna mambo mengi yaliyosababisha kufutwa kazi kwa waziri huyu mkuu lakini mambo hayo hayajawekwa wazi.
ug3
Nyumba hii unayoiona ni nyumba anayoishi na inayomilikiwa na Waziri huyu mkuu aliefutwa kazi.

MUONEKANO WA BUSTANI ZA BARABARANI DAR

Wafanya kazi wa Strabag wakimwagia sehemu ya bustani iliyoko barabarani.
Sehemu ya bustani inavyoonekana.
Moja ya mti ulioanza kuchipua.
Wafanyakazi wakijaanda kuondoka baada ya kazi.
Muonekano wa bustani iliyopo pembeni ya daraja la Ubungo karibu na stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani.
KAMERA ya GPL, leo imeangazia bustani iliyopo eneo la Stendi Kuu ya Mabasi yaendayo mikoani ya Ubungo jijini Dar es Salaam na kuona namna wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi ya  Strabag wakimwagia miti na majani yaliyopandwa katika  bustani hizo.

MAHESABU YA MBARALI::HALMASHAURI YA WILAYA YA MBARALI YAPITISHA HESABU ZA MWAKA 2013/2014.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kenneth Ndingo, akifungua mkutano wa baraza la madiwani.

 Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Dk. Boniface Kasululu akitoa taarifa katika mkutano wa baraza la madiwani.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali wakifuatilia kwa makini kikao kikiendelea.

Baadhi wa madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.

Wakuu wa idara mbali mbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali wakifuatilia mkutano wa Baraza la Madiwani.

Baraza la madiwani likiendelea na mkutano wa kupitia na kupisha Hesabu za mwisho wa mwaka.

KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Dk. Boniface Kasululu, ambaye pia ni Mganga mkuu wa Halmashauri hiyo, amewasilisha hesabu za mwaka 2013/2014 katika Baraza la Madiwani.
Alisema mali za Halmashauri kwa mwaka huo ziliingia uchakavu wa zaidi ya Bilioni 1.1 ukilinganisha na uchakavu wa mwaka 2012/2013 uliokuwa shilingi Bilioni 1.
Alisema Mali za kudumu kwa mwaka wa fedha 2013/2014 ziliongezeka kwa kiasi cha Shilingi Bilioni 4.4 kutoka Bilioni 17 hadi kufikia Bilioni 21.4, Ruzuku toka serikali  kuu kwa mwaka 2013/2014 zilipokelewa shilingi Bilioni 20 zikilinganishwa na Bilioni 19.8 kwa mwaka 2012/2013.
Aliongeza kuwa mapato kutokavyanzo vya Halmashauri kwa mwaka 2013/2014 vilikuwa ni shilingi Bilioni 1.5 zikilinganishwa na Shilingi Bilioni 1 zilizokusanywa  mwaka 2012/2013, na kwamba makusanyo hayo yamejumuisha ada za wanafunzi wa shule za Sekondari na Mfuko wa jamii(CHF).
Alisema hadi tarehe ya mwisho ya kufunga hesabu za mwaka wa fedha wa 2013/2014 zilizofanyika Juni 30, mwaka huu, Halmashauri ilikuwa na fedha taslimu benki kiasi cha shilingi Bilioni 1.2.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Kenneth Ndingo, ametoa wito kwa Madiwani  kuwahamasisha Wananchi kuendelea kuchangia katika shughuli za maendeleo ili Halmashauri ipunguze utegemezi kutoka serikali kuu.
Ndingo alisema Halmashauri imejipanga kujitegemea katika kujiendesha kwa kupunguza utegemezi kutoka serikali kuu kwa kuboresha miundombinu ya ukusanyaji wa mapato na kuwahamasisha wananchi kuchangia shughuli za maendeleo zinazofanywa na Halmashauri yao.
Alisema taarifa ya hesabu za Mwisho za Halmashauri inajumuisha mambo muhimu kama vile Mali za Halmashauri zikiwemo fedha taslimu na mali za kudumu, mikakati ya muda mrefu na muda mfupi ya Halmashauri pamoja na Matarajio ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha unaofuata.
Mwenyekiti huo alisema utaratibu wa kujadili na kupitia taarifa za mwisho za fedha ni kutokana na kanuni ambazo zimeainishwa katika muongozo wa taratibu za fedha za serikali za mitaa ya mwaka 2009, kifungu cha 31 (1).
“ Halmashauri kama taasisi zingine za serikali inapaswa kuhakikisha kuwa hesabu za mwisho zinaandaliwa kwa umakini na kwa wakati kwa ajili ya kuwasilishwa katika vikao mbali mbali vya kisheria na kuwasilishwa kwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ndani ya miezi mitatu ya mwaka wa fedha kuisha” alifafanua Mwenyekiti.
Mwisho.
Na Mbeya yetu

HABARI NA PICHA::SIASA SIO CHUKI,SIASA NI UPENDO

TABASAMU LA RAIS na HALIMA

ZAWADI HIZO:::DIAMOND ACHARUKA BMW LA WEMA!

Stori: Mwandishi Wetu
Ni sheeedah! Msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ amecharukia gari aina ya BMW 545 alilozawadiwa mwandani wake, Beautiful Onyinye wa Bongo, Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ ambaye ni Miss Tanzania 2006/07, akipinga gari hilo kupewa na meneja wake, Martin Kadinda.
Gari aina ya BMW 545i alilozawadiwa Wema Isaac Sepetu ‘Beautiful Onyinye’ na meneja wake, Martin Kadinda.
DIAMOND ACHANGANYIKIWA
Habari za kipekepeke zilidai kuwa, taarifa ya Kadinda kumpa zawadi ya gari Wema kwenye pati ya bethidei yake Jumapili iliyopita, nyumbani kwake, Kijitonyama, Dar zilimchanganya Diamond na kudai kwamba ni kitu ambacho hakiwezekani kwa maana anamfahamu vyema Kadinda kuwa hana uwezo huo wa kununua BMW la zaidi Sh. milioni 56 za madafu.
Wema Sepetu ‘Beautiful Onyinye’ akifungua shampeni katika bethidei yake.
Chanzo hicho kiliweka wazi kwamba mkali huyo anayekimbiza na Ngoma ya Mdogomdogo alihamaki baada ya kupata taarifa kuwa siyo yeye peke yake aliyekabidhi zawadi ya gari (Nissan Murano) kwa maana aliamini mwenye zawadi ya gari alikuwa ni yeye tu ambayo ilikuwa ‘surprise’ kwa mpenzi wake huyo.
Wema Sepetu ‘Beautiful Onyinye’akipokea funguo ya gari la zawadi kutoka kwa Meneja wake.
BOFYA HAPA KUPATA ‘UBUYU’
 “Unaambiwa Diamond kachanganyikiwa kabisa kusikia Wema kapewa gari, tena BMW na mbaya zaidi aliyempa gari ni Kadinda huku yeye akiamini kabisa zawadi aliyotoa kwa mpenzi wake asingeweza kupata kwa mtu mwingine yeyote, mwenyewe anasema amedhalilishwa kwani hawezi kutoa gari kisha mwanaume mwenzake naye atoe gari,” kilidai chanzo hicho.
Msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’
Mpashaji huyo alizidi kufafanua kwamba baada ya kupokea taarifa hizo na kuona kwenye vyombo vya habari na mitandao mbalimbali akiwa nje ya nchi, Diamond alianza kufanya utaratibu wa kurudi nchini akitokea Canada ili kujua vizuri kuhusu undani wa hilo gari.
“Yaani ninyi mtasikia, nakwambia kimenuka maana Diamond aliposikia na kusoma habari za BMW la Wema alianza kufanya utaratibu wa kurudi Bongo ili kupata ufafanuzi zaidi,” kilisema chanzo hicho.
Msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’
KADINDA AKOMAA
Kwa upande wake Kadinda ameendelea kusisitiza kwamba yeye ndiye aliyenunua gari hilo na kumkabidhi Wema ikiwa ni michango ya watu wanaomsapoti mwanadada huyo.
Kuhusu gari hilo, watu kibao wamekuwa wakitajwa kulinunua akiwemo mfanyabiashara Mkongo mwenye jina linaloanza na herufi S na mume wa mtu ambaye ni kigogo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jijini Dar anayetajwa kwa herufi moja ya L.
WEMA VIPI?
Jitihada za kumsikia Wema ziligonga mwamba baada ya simu yake kuita bila kupokelewa na hata alipofuatwa nyumbani kwake hakuwepo hivyo juhudi za kupata lake la moyoni zinaendelea. Stay tuned kwani inavyoonekana nyuma ya pazia ya gari hilo kuna siri kubwa!

MBUNGE KIGOLA AGEUKWA NA WAPIGA KURA MBELE YA WAZIRI NYALANDU

Kigola akifurahi kabla kibao hakijageuka
Nasifiwe Ponziano Miwoo mbele ya Waziri Nyalandu alipokuwa akihoji uadilifu wa mbunge wa Mufindi Kusini, Mendrad Kigola

SAKATA la  vibali vya uvunaji miti katika msitu wa Taifa wa Sao Hill Mufindi mkoani Iringa limemuweka pabaya mbunge wa  jimbo la Mufindi kusini Mendrad Kigola baada ya wapiga kura  wake kumgeuka mbele ya  waziri maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu  kuwa mbunge huyo ni mchochezi katika  sakata  hilo.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Igowole juzi Kigola alimkaribisha waziri huyo huku akikosoa mgao wa vibali vya kuvuna miti katika msitu wa Taifa wa saohill ambao sehemu yake upo katika jimbo hilo, ulivyofanywa kwa vikundi vya wajasiriamali wa wilaya ya Mufindi.
Huku akipigiwa makofi ya mara kwa mara yaliyomfanya ashindwe kusimama sehemu moja wakati akiongea, Kigola alisema: “sina pingamizi dhidi ya watu na vijiji vilivyopata mgao wa mwaka huu.”
“Shida yangu ni mgao uliotolewa kwa vikundi vya wilaya ya Mufindi yenye majimbo mawili. Wakati jimbo langu la Mufindi Kusini vimepata vikundi 12 kati ya 48, vingine vyote vilivyobaki vimetoka upande mwingine. Mheshimiwa waziri, nakuomba ulione hilo,” alisema.
Kauli ya Kigola ilitafsiriwa na baadhi ya watu waliokuwepo katika mkutano huo kwamba ilikuwa ikimpiga vijembe mbunge wa jimbo jirani la Mufindi Kaskazini, Mahamudu Mgimwa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.
Taarifa zisizo rasmi kutoka ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mufindi zinadai kwamba Mgimwa na Kigola hawapikiki chungu kimoja ikiwa ni matokeo ya kinachoelezwa na walio jirani na wabunge hao kwamba mmoja wao ana wivu wa kisiasa dhidi ya mwenzake.
Taarifa hizo zisizo rasmi ambazo hata hivyo hazijawahi kutolewa ufafanuzi na Kigola mwenyewe zinadai kwamba amekuwa akimuonea wivu Mgimwa baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Naibu Waziri.
Wivu huo ndio umepelekea kuchochea chokochoko ya kuhoji uwiano wa mgao wa vibali vikiwemo vibali 48 vilivyotolewa kwa vikundi 48 vya wilaya ya Mufindi.
Hoja ya Kigola dhidi ya mgao wa vibali hivyo ilionekana ina mashiko kwa muda wote wa mkutano huo mpaka pale Waziri Nyalandu alipotoa ruksa kwa wananchi wa kijiji hicho cha Igowole kuuliza maswali.
Alikuwa Nasifiwe Ponziano Miwoo aliyechafua hali ya hewamara baada ya kupata nafasi ya kuuliza swali alilotoa kwa mtindo aliodai wa kujenga hoja ili wananchi wamuelewe.
Akinukuu vifungu kadhaa vya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano huku akioanisha na uadilifu wa mbunge huyo Miwoo alisema:
“Kuna haja ya kuoanisha hoja za mbunge huyu Kigola na uadilifu wake; na kuna haja ya kujua mali zinazomilikiwa na mbunge huyu ili tuone kama kunasababu kwa familia yake kupata kibali cha kuvuna miti wakati baadhi ya vijiji na vya wilaya ya Mufindi na wajasiriamali wake wakikosa,” alisema.
Alisema katika orodha ya wanufaika na vibali vya mwaka huu, jina namba 388 ni la mtoto wa Kigola anayesoma katika moja ya shule bora zilizoko wilayani Mufindi.
Alisema zipo dalili kwamba Kigola alitumia jina la mwanae huyo kupata kibali hicho jambo linalojenga mashaka dhidi ya uadilifu wake.
“Mheshimiwa Waziri tuna mashaka na huyu mtu na kama kila mwaka anajaza fomu inayoonesha mali anazomilikia. Kwanini jina la mwanae litumike,” Miwoo alisema huku waliokuwa wakimshangilia Kigola wakigeuza kibao na kumshangilia yeye.

SIASA NA MAPENZI::VITA YA WABUNGE WAREMBO, SIRI NJE

Stori: Mwandishi Wetu
IMEFICHUKA! Madai ya Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Geita, Vicky Paschal Kamata kuwatumia meseji za kashfa wabunge wenzake, Lucy Thomas Mayenga (CCM) na Catherine Valentine Magige (UVCCM)Mkoa wa Arusha sasa mambo hadharani.
Mbunge wa CCM kupitia kadi ya Umoja wa Vijana (UVCCM), Mkoa wa Arusha, Catherine Valentine Magige .
Kwa mujibu wa chanzo chetu, wabunge hao warembo wako katika vita baridi ikiendeshwa chini kwa chini kwa Cathy (pichani) na Lucy kudai kwamba wamekuwa wakitumiwa meseji zenye kejeli na kashfa nzito kutoka kwa mheshimiwa Vicky.
KUNA SABABU?
Kwa mujibu wa chanzo chetu, licha ya sababu kutokuwa wazi sana, lakini madai ni kwamba wana bifu linalokimbilia mwezi wa nne sasa.
“Unajua si rahisi wao kuweka wazi bifu lao, lakini wenyewe watakuwa wanajua nini kiini, ukifuatilia utagundua kuwa maisha yao yamekuwa ni ya vikundivikundi, akina Lucy wana kundi lao na Vicky ana la kwake,” kilisema chanzo hicho.
Mbunge wa CCM kupitia tiketi ya Umoja wa Vijana, Lucy Thomas Mayenga
KWA NINI VICKY?
Chanzo kiliendelea kuanika kwamba, baada ya meseji zinazodaiwa kukosa staha kutumwa na asiyejulikana kwenda kwenye simu za mkononi za Cathy na Lucy, waheshimiwa hao hawakupembua sana mchele, moja kwa moja wanadaiwa kumtaja hasimu wao kwenye vyombo vya dola kuwa huenda anahusika na ‘utundu’ huo.
POLISI WAFUATILIA MINARA YA SIMU
Duru za kipolisi zinadai kuwa kufuatia waheshimiwa hao kumlalamikia Vicky, wana usalama hao walianza kuchunguza mawasiliano yake ambapo walibaini mambo makuu mawili.
KWANZA, baadhi ya meseji hizo zilionesha kutumwa kwa kupitia mnara wa simu uliopo maeneo ya bunge. PILI, kuna meseji iliwezeshwa kusafiri kwa nguvu ya mnara uliopo eneo linaloitwa Uwanja wa Ndege ambapo inadaiwa Mheshimiwa Vicky ndiko anakoishi.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Geita, Vicky Paschal Kamata
SERIAL NUMBER
Pia yapo madai kwamba, polisi hao walikwenda kitaalam zaidi na kubaini kwa kutumika namba zilizomo ndani ya simu eneo la kuwekea betri (serial number) ambazo zilionesha kuwa, laini iliyokuwa ikituma meseji za kuudhi kwa waheshimiwa hao pia imekuwa ikutumia na laini ambayo polisi walimjua mhusika, ingawa wasemaji wake wamesita kuthibitisha.
POLISI NYUMBANI KWA VICKY
Habari zaidi zinadai kuwa, Jumanne iliyopita, polisi mkoani Dodoma walifika nyumbani kwa mheshimiwa Vicky na kufanya uchunguzi kama wanaweza kupata simu yenye laini iliyoripotiwa na akina Mayenga (pichani) kwamba imekuwa ikiwakashifu kwa meseji lakini hawakufanikiwa kukuta chochote.
Alipotafutwa Vicky ili kujua undani wa meseji hiyo juzi, simu yake haikuwa hewani. Kwa upande wake Lucy ambaye alidai kutumiwa meseji za matusi katika gazeti moja (siyo la Global), naye simu yake iliita bila majibu, huku Cathy akishindwa kupatikana na kulifanya gazeti hili kuzidi kuchimba kwa kina sakata hili ili kupata mbivu na mbichi na kuzianika bila kusitasita.

SIASA::CHADEMA IRINGA WALIA NA POLISI , WAJIPANGA KUVURUGA MAANDAMANO YA KINANA

Sehemu ya watu waliojitokeza katika mkutano huo

Wakionesha ishara ya chama chao


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelitaka jeshi la Polisi kudhibiti misafara mirefu ya magari na pikipiki, na aina yoyote ya maandamano wakati wa mapokezi ya katibu mkuu wa  Chama cha Mapinduzi (CCM) Abdulahman Kinana wakati wa ziara yake mkoani Iringa .

Kauli ya Chadema  imekuja  ikiwa ni siku takriba tatu kabla ya kuwasili Kinana Oktoba 6-11  mwaka huu kuanzia ziara yake mkoani Iringa 
Sehemu ya watu waliojitokeza katika mkutano huo
 Kwa mujibu wa taarifa  kwa  vyombo  vya habari zilizotolewa na CCM mkoa Kinana ataambatana na Katibu Itikadi na Uenezi wa chama hicho Nnape Nauye wanatarajia kufanya ziara ya kukijenga chama hicho na kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika wilaya zote za mkoa wa Iringa wakati wa  ziara  hiyo.
Akiwahutubia  juzi wananchi wa kata ya  Kihesa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA) Patrick Ole Sosopi alisema  wamesikitishwa na  jeshi la polisi  kuzuia mapokezi yake mkoani Iringa huku  wakitambua wazi kuwa ni haki ya  wanachama  kumpokea  kiongozi  wao ila polisi  waligoma kutoa kibali  zaidi ya kuruhusu mkutano wa hadhara pekee.
Akiwa na Makamu Mwenyekiti Bavicha, Patrick Ole Sosopi
Alisema kuyazuia maandamano ya Chadema na kuruhusu ya CCM kutadhihirisha jinsi Polisi wanavyokibeba chama hicho tawala.
Alisema wakati wakijiandaa kuchukua Dola wanataka kuona wanashindana katika uwanja sawa wa kisiasa kwahiyo hawatakubali kuona jashi la Polisi linaruhusu maandamano katika misafara ya Kinana wakati kwao linakataa.

Sosopi aliyekuwa na Mchungaji Peter Msigwa wakitokea jijini Dar es Salaam kulikofanyika chaguzi mbalimbali za kitaifa za chama hicho, walipokelewa katika eneo la Igumbilo na viongozi wachache wa chama hicho baada ya Polisi kudaiwa kuwazuia wafuasi wao kuwapokea kwa misafara ya magari, bodaboda na maandamano.
“Tumetii maelekezo ya Polisi, vijana wetu wa bodaboda wamezuiwa kutupokea; ili haki itendekea tunataka Kinana na timu yake watakapoingia mjini Iringa, misafara yao isiwe na maandamano ya watu, pikipiki wala magari,” alisema Mchungaji Msigwa katika mkutano wao mkubwa uliofanyika katika kata ya Kihesa mjini Iringa.
Mchungaji Msigwa alisema watashangaa na kuchukua hatua endapo Polisi itairuhusu CCM kuwa na maandamano na misafara ya magari na pikipiki.
Naye Mwenyekiti wa Chadema  wilaya ya Iringa mjini  Frank Nyalusi alisema Kinana atakuwa mjini Iringa Oktoba 11, wakiona bodaboda ama wana CCM wako katika msafara wake wataingia  barabarani  na  wafuasi wa Chadema na madereva boda boda kufanya maandamano yasiyo na kibali

Wednesday, 1 October 2014

SAWA UMZURI, LAKINI UNAJISIKIAJE UNAPOITWA JINA LA ‘CHA WOTE’?

Niwiki nyingine tena tunakutana kupitia safu hii nikiamini kwamba umzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida.
Mimi niko poa na kama ilivyo ada leo nimekuja na mada ambayo inawagusa wanawake kwa asilimia kubwa. Nazungumzia hii tabia ya baadhi ya wasichana kutumia uzuri wao vibaya kwa kuwapanga foleni wanaume bila kujali madhara yanayoweza kujitokeza.Wewe msomaji wangu utakuwa ni shahidi juu ya uwepo wa wasichana ambao hawawezi kusema ‘no’ pale wanapotamkiwa masuala ya mapenzi.
Katika uchunguzi wangu mdogo, wapo wasichana ambao wameridhika na maisha ya kutokuwa na mwanaume ‘pamanenti’, wao imekuwa ni fasheni kubadili wanaume kama nguo.
Ninapozungumzia wanawake wa sampuli hii, simaanishi machangudoa. Nawazungumzia wale ambao wanafanya kazi zao au wako mtaani lakini hawajabahatika kuwa na wanaume wa kuwashika.
Sasa kutokana na hisia zao za kimapenzi, anayetokea mbele yao ni halali yao na mapenzi yao huwa hayadumu. Unamkuta msichana mzuri mwenye kila sifa ya kuwa na mpenzi wake lakini yupoyupo tu.
Leo katembea na huyu, kesho na yule na wakati mwingine ni kwamba si tamaa ya pesa, ni tamaa ya mwili au kutafuta tu sifa kuwa katembea na flani. Hii ni sawa kweli?
Unajisikiaje pale unapopachikwa jina la cha wote mtaani kwenu au eneo lako la kazi? Hata kama hawakuiti hivyo, huoni unajivunjia heshima kwa kuwa na uhusiano na wanaume tofauti ndani ya kipindi kifupi tena baadhi yao wakiwa ni marafiki?
Nyie ambao mnajirahisi kwa wanaume mjue mnachoreka sana na mnaonekana msiyoithamini miili yenu.
Matokeo yake sasa watu wanapasiana kama mpira kwenye eneo la 18. Leo unatembea na Shabani, akikuchoka anamsukumia mshikaji wake John na wewe unakubali kirahisi.
Huku ni kujirahisi kulikopitiliza.
Ni sawa unaweza kuwa na sura na umbile zuri linaloweza kukufanya kila unapopita ukatongozwa. Hiyo inatakiwa kuwa changamoto kwako na siku zote simamia utu wako.
Kwa jinsi ulivyo, unatakiwa kuwa na mpenzi kama siyo mume, mtu ambaye anakupenda kwa dhati na aliyetayari kuchukua nafasi yake kama mpenzi. Mtu ambaye atakupa furaha, atakulinda, atakushauri kuhusu maisha na kukusaidia pale ambapo utahitaji msaada wake.
Usipokuwa na mtu ‘pamanenti’, hayo huwezi kuyapata. Utayapataje wakati uliyenaye anataka akuonje kisha kesho atafute sababu akutose na kuhamia kwa mwingine?Nadhani ifike wakati kama ni msichana ambaye unastahili kuwa na mpenzi, utulie na uchague mtu mmoja ambaye utampa dhamana ya maisha yako. Chukua muda kuwa peke yako kwa kipindi flani lakini siku moja amini utampata mtu atakayekulindia heshima yako.Kwa ulimwengu wa sasa siyo sifa kuwa na msururu wa wanaume. Hivi unadhani ni sifa kuwa umetembea na wanaume kibao katika eneo lako la kazi? Hivi unajisikiaje unapokuwa msichana ambaye umetembea na idadi kubwa ya wanaume katika mtaa wenu?
Ukweli ni kwamba kila utakapopita utakuwa kama hujavaa nguo na ujue wanaume zaidi ya mmoja ambao wametembea na wewe wakikutana na kugundua wote wamekupitia, watakushusha thamani na watakuwa wa kwanza kukuponda kwa wengine kwamba wewe ni kicheche.
Ifike wakati ujitambue na ujue thamani yako. Uzuri wako hautakuwa na faida yoyote kama kila anayekuambia vipi unamwambia poa! Unamjibu poa, dhamira yake unaijua? Unadhani ukishamuonjesha mara moja ndiyo atakuwa na wewe?
Kama ulikuwa hujui, wanaume wengi sasa hivi wanakwepa sana kuwa na wasichana wazuri. Wanahisi kutakuwa na ugumu katika kuwatuliza kwani wanaume kibao watawatolea macho. Lakini sasa shangaa, wanaume wengi wanajisikia ujiko sana kuwapitia wasichana wazuri. Yaani wanajiona ni wajanja kutongoza na kukubaliwa na akina dada warembo.
Ndiyo maana nasema, usipowajulia hawa watakufanya kama vile mpira wa kona kisha watakuacha na makovu ya aibu na usipate wa kukuoa. Kama atatokea lazima atakuwa ni mtu wa mbali asiyejua nyendo zako, kwa nini ujiwekee historia mbaya?
Tukubali kwamba kuna wakati tunakosea na tubadilike. Hapo ulipo jiulize ni wanaume wangapi ambao umewapa nafasi waujue mwili wako kirahisi? Huoni aibu? Badilika wewe, acha ushamba!

KAZI SAWA, LAKINI MUMEO KILA KITU

He he he heeee, acha nicheke miye mwana Kibatari mjukuu ya Kandili, unajua vitu vingine vinachekesha kama si kusikitisha, unalalamika mwanamke mzima uliyekamilika tena bila aibu eti mfanyakazi wako wa ndani anakulia mali zako kwa mumeo kuhamishia mapenzi kwake.
Unajua kauli hiyo hunifanya nikumbuke ile kauli isemayo mpambe awe mwenye mali na mwenye mali aonekane mpambe. Ooh, nilikuja na kasi ya ajabu. Na miye bila salamu kwa kuwahi kuzima moto ambao sasa hivi umetanda kila kona ya nyumba zetu, hasa wafanyakazi ambao wameolewa na wao kumweka hausigeli.
Kwa kuwa na mfanyakazi wa ndani, basi kila kitu unamuachia, akifanya ambacho ni makosa kwa mwanamke aliyefundwa akafundika kumuacha hausigeli amfanyie mumeo kazi zinazokuhusu.
Tokea lini Fisi akaachiwa bucha, wewe na mfanyakazi  wako wa ndani mnazidiana nini kimaumbile, pengine mfanyakazi wako Mungu kampendelea kuliko wewe. Kwa vile unafanya kazi basi ukirudi unautupa mkoba wako unakwenda kuoga ukila unapanda kitandani kutokana na uchovu wa kutwa nzima!
Unamwacha mfanyakazi wa ndani afanye kazi zote, kumsubiri mumeo wewe umelala akirudi amtengee maji ya kuoga wewe umelala, amtengee  chakula huna habari unajigeuza kitandani.
Anaondoa vyombo pengine amevaa upande wa kanga bila kitu ndani, na kama anajua yupo katika mkao wa kula naye hufanya vibweka vya kuchezesha makalio, kuacha matiti nje.Sehemu hizo ndizo huwatoa imani wanaume na kujikuta wakijaribu kwa vile naye ana hamu zake, basi shoga wee unalala watu wanajilia vyao. Ulikuwa wa kuamshwa usiku.
“Honey leo nimeshikwa mwenzio.”
Unajikuta unalala kila siku bila kuguswa kutokana na uchovu wa kazi unaona sawa, kumbe nyani kaingia shambani wee wapiga usingizi mali zako zinaliwa.Leo na kesho mfanyakazi wako wa ndani anageuka mke mwenzio tena mapenzi yote mumeo anayahamishia kwake kwa vile ndiye anayemfanyia zaidi ya mke.
Utakalia kulia “Aah, nyani kavamia shamba langu naanza kuvuna mabua,” we mwenyewe umemchekea unategemea nini.Shoga nataka nikueleze sheria za ndoa, hata kama unafanya kazi gani hakikisha baadhi ya vitu hasa vimuhusuvyo mumeo, mfanyakazi wa ndani havigusi. Kufuliwa nguo, kutengewa maji ya kuoga, kula, lazima ale mumeo ukiwa pembeni hata kama umeshiba basi mlishane hata tonge mbili.
Mumeo ni lulu isiyotaka kuguswa na mtu, itunze kwa nguvu zako zote, hakikisha hakuna mtu atakayeigusa hata shoga yako ila wewe mwenyewe. Mfanyakazi ana mipaka yake wala asiwe na mazoea ya kuvuka mipaka na mumeo.
Narudia, wewe na mfanyakazi hampishani kitu, kila ulichonacho anacho, naye ana matamanio vilevile, anataka vitu vizuri. Kufanya kazi usijisahau na kuona kazi ni bora kuliko mumeo, kazi ina umuhimu kwa sehemu zake na ukifika nyumbani mwenye nafasi ya pekee ni mumeo kuhakikisha anapata huduma zote muhimu.
Kinachowaumiza wanawake wengi ni uvivu, kwa sababu wanafanya kazi wanaamua kumuachia fisi bucha.Usije kushangaa kukuta amekula hadi gogo la kupasulia mifupa. Yangu nimemaliza, la muhimu kuyafanyia kazi la sivyo utaachika na nyumba unaipenda.

Ni mimi anti Nasra, Shangingi Mstaafu.

Washiriki Shindano la Mashujaa wa Kesho Waanza Kurejesha Fomu

Chumba cha kompyuta cha washiriki wa Shindano la Mashujaa wa Kesho. Chumba cha kompyuta cha washiriki wa Shindano la Mashujaa wa Kesho
Baadhi ya washiriki wa Shindano la Mashujaa wa Kesho wakipitia fomu zao. Baadhi ya washiriki wa Shindano la Mashujaa wa Kesho wakipitia fomu zao.

 Na Mwandishi Wetu

  ZOEZI la uchukuaji fomu kwa ajili ya vijana mbalimbali kushiriki katika Shindano la Mashujaa wa Kesho la Statoil limeendelea kushika kasi huku idadi kubwa ya vijana wakiendelea kurejesha fomu kwa lengo la kushiriki katika kinyang’anyiro hicho. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Ofisa Mawasiliano wa Statoil Tanzania, Erick Mchome alisema hadi sasa zaidi ya vijana 150 wamerejesha fomu zao tayari kwa kuyashindanisha mawazo anuai ya miradi yao walioiwasilisha kwa ajili ya kushiriki katika shindano hilo. Mchome alisema vijana hao wamejaza fomu kwa ajili ya kushiriki katika shindano hilo kuwania kitita cha hadi Dola 5,000 kwa mshindi wa kwanza. “Kimsingi zoezi hili la shindano la Mashujaa wa Kesho limepokelewa vizuri na linaendelea vizuri sana vijana wengi wa Mtwara wamejitokeza kuchukua fomu na baadhi wameanza kuzirejesha fomu zao…zaidi ya vijana 150 tayari wamerejesha fomu,” alisema Mchome. Hata hivyo kiongozi huyo aliwataka vijana ambao wamechukua fomu kuzirejesha fomu zao kwa wakati kwenye vituo walivyoelekezwa ili hatua zingine za utaratibu wa shindano hilo ziweze kuendelea. “Ningependa kuwakumbusha washiriki kuwa mwisho wa kurejesha fomu ni Oktoba 10, 2014 saa nane kamili kwenye vyuo vya Naliendele Agricultural Institute, Tanzania Institute of Accountancy, VETA, Chuo cha Utumishi na Chuo cha Stella Maris Pamoja na Pride FM,” alisisitiza Mchome. Akifafanua zaidi, Mchome alisema mchujo wa kupata washiriki 40 watakaoingia hatua ya pili utafanyika mara baada ya zoezi la urejeshwaji fomu kukamilika na kutakuwa na mchujo wa tatu ambao ni wa mwisho na kuwatoa washindi watano watakao wania dola 5,000 kwa mshindi wa kwanza na dola 1,000 kwa wa shindi wa pili, tatu, nne na tano . Shindano hilo la vijana linalojulikana kama Mashujaa wa Kesho lenye lengo la kuhamasisha ujasiriamali lilizinduliwa rasmi Septemba 3, 2014 na kampuni ya Statoil na linatarajiwa kumalizika Desemba 12 mwaka huu.

MWANAMKE AKIOLEWA KUNA ULAZIMA AITWE JINA LA UKOO WA MUMEWE?

KARIBUNI tena na tena, wasomaji wa safu hii motomoto inayozungumzia maisha kwa ujumla. Lengo sa safu hii ni kuwekana sawa katika mazingira ya maisha ya uhusiano tunayoishi.
Mada yetu ya leo imetokana na kuzidi kushamiri kwa hoja kwamba je, mwanamke akishaoelewa kuna umuhimu wa kuitwa kwa jina la ukoo wa mumewe?Mfano, awali mwanamke aliitwa Julieth Thomas Rupia, akaolewa na Samuel Aloyce Masumbuko. Je, Julieth akishaolewa aitwe Julieth Thomas MASUMBUKO?
Tangu miaka na miaka, wanawake wamekuwa wakibadili majina yao ya mbele na kuachana na ya wazazi wao kwa kutumbukiza ya waume zao, hasa ya ukoo ndiyo zaidi.
Lakini miaka ya hivi karibuni, baadhi ya wanawake wameachana na dhana au utaratibu huo, wanatoa hoja kwamba hawaoni sababu ya kutumia majina ya ukoo wa waume zao baada ya kuolewa.
MADAI YAO
Nilibahatika kuzungumza na baadhi ya wanawake waliotoa hoja ya kupinga matumizi ya majina ya waume zao.
Wengi walisema kuwa, kwa ndoa za siku hizi ni kujisumbua tofauti na zamani.
“Unajua ndoa za sasa tofauti na zile za mababu na mabibi zetu, wao walikuwa wanadumu katika ndoa, lakini sisi siyo. Ndiyo maana tunahofia kwamba, leo ukiitwa kwa jina la mumeo, watu wakikuzoea, kesho ukaachika na kurudi kwenye jina lako unakuwa mgeni katika jamii.
“Hali hii inasababisha wanawake wengi siku hizi tukiolewa tunapenda kuendelea kuitwa kwa majina ya ukoo wa wazazi wetu,” anasema mama Patrick, mkazi wa Bunju jijini Dar.
KUNA UKWELI?
Labda hili ndiyo swali la msingi kuliko yote, kwamba kuna ukweli wowote kuwa ndoa za siku hizi hazitoi fursa kwa mke kutumia jina la mumewe?
Ni kweli, ndoa za sasa si za kutilia maanani wala kujiapizia hata kidogo. Zipo ndoa zinazovunjika miezi michache baada ya kufungwa, nyingine mwaka mmoja tu. Ukikutana na ndoa zina miaka mitano ni majaliwa au neema ya Mungu.NI KIGEZO?
Si kigezo hata kidogo, ni jukumu la wanandoa wenyewe kutengeneza mazingira safi na salama ili hali ya kuachana isiwepo. Lakini tangu miaka na miaka, mwanamke akiolewa hupaswa kutumia jina la ukoo wa mumewe.
MR & MRS INATOA MWANGA
Haya ni maneno yanayojulikana na wengi, wakiamini kuwa ni bibi na bwana! Ni sawa kabisa, lakini ukifuatilia tafsiri ya Kiingereza, Mr au Mister ni bwana! Ili liendelee lazima liwe Mr fulani. Mfano, Mr Ndauka (bwana Ndauka).
Mrs ni bibi lakini kwa maana ya mke (Kenya wanatumia sana mke kumwita bibi). Lakini pia mrs katika tafsiri ya Kiingereza lina maana mke wa… Mfano, Mrs Kapipi (mke wa Kapipi). Lakini neno Mr haliwezi kutafsirika kuwa ni mume wa…yaani haiwezekani kuwa mr Margaret ikawa ni mume wa Margaret.
Ufafanuzi huo unaonesha kuwa asili ya wanawake kuitwa kwa majina ya waume zao ilitokana na kutambulishwa kuwa mke wa fulani (mrs).
MIFANO YA VIONGOZI
Wako wake wa marais, mawaziri nakadhalika wanaitwa kwa kutumia majina ya ukoo wa waume zao. Mfano, mama Salma Kikwete, mama Tunu Pinda, Anna Kilango Malecela, Anna Kajulumo Tibaijuka, Asharose Mtengeti Migiro, mama Hillary Rodham Clinton.
MAJINA KUFA
Ndoa kama inavyotakiwa kuwa na uvumilivu ili idumu ndiyo silaha ya matumizi ya majina ya waume lakini wapo wanawake walioachwa kwa talaka au kufiwa, waliendelea kujulikana kwa majina ya waume zao bila kuathiri maisha. Mfano, Winnie Madikizela Mandela na Graca Simbine Machel.
MADHARA YAKE SASA!

NI RAHISI MWANAMKE ALIYEAJIRIWA KUSALITI!

KWANZA nianze kwa kuwashukuru wasomaji wote wa safu hii, waliowasiliana na mimi kwa namna moja au nyingine, katika kubadilishana mawazo juu ya uhusiano. Ni faraja kugundua kwamba wapo watu wanaofuatilia unachokiandika na kisha kutaka kuchangia neno.Mada yangu ya leo inaweza kuniletea ugomvi na waajiriwa wenzangu wanawake, lakini panapo ukweli ni vyema tukasema, kwa sababu unasaidia katika kurekebisha na wakati mwingine hata kujua jinsi gani unaweza kujihami, ili kutokusaliti ndoa au uhusiano wako wa kimapenzi.
Nina uzoefu kidogo na mambo ya kazi za ajira maofisini, nimefanya hivi kwa muda mrefu. Wakati flani nilifanya kazi katika ofisi zilizo katikati ya jiji, kule mitaa ya Posta jijini Dar es Salaam.
Ofisi nyingi za serikali na watu binafsi zinapatikana mitaa ile. Kutokana na sababu hiyo, kuna idadi kubwa pia ya migahawa, hoteli, mama ntilie, pub na kadhalika.
Kuna mambo mawili makubwa yenye ushawishi mkubwa wa usaliti. Ofa za chakula au vinywaji na usafiri. Kwa kawaida, wafanyakazi wa ofisi moja hupenda kutoka pamoja wakati wa chakula cha mchana, wenyewe tunapendelea zaidi kusema lunch!
Kila mmoja ana sehemu yake anayokula kulingana na kipato chake, wapo wanaokwenda Southern Sun kupata chakula cha mchana, na wapo wanaowafuata mama ntilie wanaojibanza kwenye vichochoro vingi vilivyopo mjini.
Huko ndiko tunakokutana na akina dada waliovalia vizuri na kupendeza, wakitokea katika maofisi mbalimbali, huwezi kujua yupi ni mhudumu wa chai, yupi ni bosi, wote wanang’ara. Na hapa ndipo ofa za misosi zinapoanza kushawishi ngono.Kijana mmoja mwenye kipato kikubwa ofisini kwake, atavutiwa na msichana mrembo mwenye mshahara wa wastani. Ili kumsogeza karibu, atalipia chakula cha siku hiyo na kumualika kwa kesho yake. Kulipiwa chakula ni jambo dogo, lakini lenye thamani kubwa sana. Si rahisi mtu aliyekulipia chakula kwa nia njema, ukaacha kumshukuru na hata kumwelekeza unapofanya kazi.
“Mimi nipo pale Oj Traders,” msichana anaweza kujita mbulisha jina na kusema anapofanyia kazi huku mkaka akimweleza kuwa yeye ni mhasibu katika ofisi flani. Watakapo
kutana mara ya pili, wataachiana namba za simu.
Baada ya hapo, mkaka atafanya mbwembwe za kuhamahama maeneo ya lunch ili mradi tu mdada wa watu aingie kwenye laini.
Ukimaliza suala la lunch, kuna hii kitu foleni, hasa kwa wakazi wa Dar es Salaam. Raha ya kufanya kazi katikati ya jiji inaingia shubiri kadiri jioni inavyozidi kusogea. Kuanzia saa kumi, ni vurugu katika vituo vya daladala na hasa wakati kama huu ambao bodaboda zimezuiliwa kuingia mjini.
Wenye magari binafsi ndiyo wakati wao wa kujidai, ingawa foleni inawakumba wote. Lakini ni afadhali ukiwa kwenye foleni ndani ya gari dogo, mko wawili kuliko foleni, umeshika bomba kwenye daladala.
Siyo rahisi kwa mdada kukataa lifti ya kijana mwenye gari. Na katika foleni ndefu, ni wazi kwamba hadi mwisho wa safari, watakuwa wameshabadilishana namba. Kwa msichana, kuwa na uhakika wa usafiri kila siku ni ukombozi.
Tusidanganyane, hakuna msichana ambaye hatajua kuwa lunch au usafiri anaopewa unahitaji malipo maalum, ambayo ni penzi. Hali hii haiko Dar tu, bali nchi nzima na pengine duniani kote.
Mwanamke aliyeajiriwa anakuwa katika mitihani mikubwa zaidi ya kusaliti ndoa au uhusiano wake, kwa sababu hata kama haitakuwa kwenye chakula au usafiri, bado watu anaokutana nao katika utendaji wake, wanaweza kumghasi. Fikiria anakutana na mabosi, marafiki wa mabosi wake, wafanya biashara, atapona kweli?
Hata hivyo, simaanishi kama tabia hii inawakumba waajiriwa wote, isipokuwa nadhani ni sehemu kubwa wanahusika!

TAMKO LA KULAANI VITISHO DHIDI YA WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA


Mtandao wa Watezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umefuatilia kwa karibu mchakato wa kupata katiba mpya unaondelea Bungeni,  mjini Dodoma na kuona ya kwamba mchakato huu  umegubikwa na mambo mengi yenye kuashiria ukiukwaji wa haki za wajumbe wa Bunge hilo.  Mchakato wa kupiga kura ya NDIO au HAPANA kwenye rasimu ya katiba inayopendekezwa umezua vitisho  na ‘sintofahamu’ nyingi dhidi ya wajumbe walio piga kura ya HAPANA.
 
Mtandao wa Watetezi kama  Sauti ya  watetezi wote nchini Tanzania imepokea taarifa zenye kusikitisha kutoka kwa baadhi ya wajumbe wanaounda Bunge Maalumu la Katiba kuwa wabunge waliopiga kura za HAPANA  zenye kuashiria  kukataa katiba inayopendekezwa wamelalamika na kukiri kuwa maisha yao yapo hatarini Mjini Dodoma. Mtandao unalaani vitendo hivyo pamoja na wote wanaohusika na vitisho hivyo dhidi ya wajumbe hao wa Bunge la Katiba.
Mtandao  baada ya kuwasililina na  wajumbe hao umebaini kuwa wanaotishwa ni miongoni mwa wajumbe watokanao na kundi la 201 hasa upande wa Zanzibar ambao wamesisitiza kwamba maisha yao yapo hatarini na wanaishi kwa wasiwasi huku wengine wakifanya mipango ya kuondoka upesi katika Mkoa huo ambao bunge linaendeshwa.
Kwa mujibu wa maelezo yao,  inaonekana kuwa toka walipo piga kura za wazi za HAPANA baadhi ya wabunge  na hata mawaziri wamekuwa wakiwatishia maisha kwa kuwa wametekeleza haki yao ya kupiga kura ambazo hazikuwafurahisha watawala.  Miongoni mwa wajumbe waliopiga kura za hapana na  waliopokea vitisho hivyo baada ya kupiga kura ya ‘HAPANA’ ni:
1.      Salma Said- Asasi zisizo za Kiraia (AZAKI)
2.      Ali Omary
3.      Adil Mohammed- Chama cha Walemavu Zanzibar
4.      Fatma Mohamed-  Taasisi za Kidini
5.      Jamila Abeid-   Vyama vya Siasa
6.      Dr Alley Nasor- Vyuo Vikuu Zanzibar
7.      Mwanaid Othman
Vitisho vivyo vilianza baada ya Mwenyekiti kuhofu kutopata idadi ya theluthi mbili kutoka Zanzibar. Wajumbe hawa kwa sasa wanahishi kwa ofu kubwa na mashinikizo makubwa toka kwa  baadhi ya watawala na wajumbe waliopo katika  Bunge hilo la kuwataka wabadili msimamo wao. Mashinikizo hayo ni pamoja na tendo la kura za hapana kuundiwa kamati ya kuzijadli bila kujulikana lengo lake ni nini hasa, kwani kura ikishapigwa hairudiwi tena.
  WITO WETU
Tunapenda kuwakumbusha Wajumbe na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba kuwa Katiba  Bora inatokana na maridhiano na kwa kuheshimu mchakato na si kwa mabavu au nguvu ya dola.
1.      Kila mtu anahaki ya kutoa maoni yake binafsi na kupiga kura bila kulazimishwa achague nini.
2.      Sheria ya mabadiliko ya katiba inatakiwa kufuatwa  ili kuepusha nchi kuingia kwenye machafuko.
3.      Tuna msihi kiongozi wa Bunge Maalumu la Katiba kufuata misingi ya utawala bora, haki za binadamu, na demokrasia anapoliendesha Bunge hilo.
4.      Mtandao unawasihi wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kuacha kuwadhalisha na kuwanyanyapaa wale ambao wataonekana wakipiga kura za  HAPANA, kwani lengo la kuwepo kwa zoezi la upigaji kura lilikuwa linatambua uwepo wa kura za NDIYO na HAPANA.
5.      Tunalisihi jeshi la polisi kutimiza dhamana yake ya kulinda raia na mali zao kwa kuhakikisha hatua muhimu zinachukuliwa kutokana na vitisho walivyopokea baadhi  ya Wajube Maalumu wa Bunge la Katiba.
6.      Tunawasihi wajumbe wote waliopo mjini Dodoma kwenda kuripoti katika vyombo vya usalama pamoja na kutoa taarifa kwa THRDC endapo wataona mazingira yoyote ya kuhatarisha maisha yao.

KAULI TATA::Atakae leta fujo na APIGWE TU....WAKUPIGA HAO

MAJI BADO TATIZO VIUNGA VYA DAR

Wauza maji  wakiwa na mikokoteni yao maeneo ya Kimara Mwisho.
Mikokoteni ya maji ikiwa imepakiwa kijiweni, eneo la Kinondoni, Manyanya.
Vijana wakiwa na mikokoteni ya maji maeneo ya Ubongo.
Mikokoteni ya maji ikiwa maeneo ya Makumbusho.
KAMERA ya GPL imefanikiwa kuzunguka katika baadhi ya viunga vya Jiji la Dar es  Salaam na kubaini huduma ya maji safi na salama bado ni tatizo, kutokana na kuwepo kwa vijiwe vingi vya kuuzia maji japokuwa ni moja ya ajira kwa vijana walio wengi.