Hatua zaidi kuzuia kusambaa kwa Ebola
14 Agosti, 2014....
Jitihada zinaendelea kuzuia
kusambaa kwa maradhi ya Ebola, Afrika Magharibi.Tangu mwezi Machi kirusi
hicho kimeua zaidi ya watu elfu moja, wengi wao kutoka Sierra Leone,
Liberia na Guinea.
Nigeria nayo imetangaza kuwepo kwa mtu wa tatu
aliyekuwa na ugonjwa huo. Wakati huohuo, Shirika la Afya Dunia
limeielezea Kenya kuwa katika hatari kwani kuna uwezekano mkubwa wa
kusambaa kwa virusi hivyo kutokana na kuwepo safari nyingi za ndege
kutoka nchi hiyo kuelekea Afrika magharibi.Huko nchini Nigeria ambako tayari Ebola imesababisha vifo vitatu, serikali imewataka watu wote kushirikiana na wataalamu wa afya hasa baada ya kuwapo kwa taarifa ya muuguzi aliyetoroka hosipitalini baada ya kuwekwa chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya kufuatia kuhofiwa kuwa ameathirika na Ebola. Muuguzi huyo ameelekea nyumbani kwake huko mashariki mwa Nigeria hali inayowatia hatarini watu wengi.
Hivi sasa kiasi kidogo cha dawa za majaribio kimefika nchini Liberia kuwatibu madaktari wawili. Maabara iliyotoa dawa hiyo huko marekani inasema imeishiwa kabisa dawa hizo.
Siku moja tu baada ya shirika la afya duniani kutoa ruhusa ya kutumiwa dawa hizo Canada nayo imetangaza kuwa itatuma dozi 1000 za chanjo kwenda afrika magharibi ambako wahudumu wa afya ndio watakaopewa dawa hiyo ingawa haijawahi kufanyiwa majaribio.
Huko Sierra Leone daktari bingwa mwingine amefariki kwa ugonjwa wa ebola. Modupeh Cole amekuwa akifanya kazi mjini Freetown na kifo chake kinakuja baada ya mtaalamu pekee wa virusi nchini humo kufariki wiki mbili tu zilizopita.