Sunday 14 September 2014

AFYA YA UZAZI WANAWAKE::MZUNGUKO WA HEDHI USIOPEVUSHA MAYAI (ANOVULATORY CYCLE)

Katika makala zilizopita tuliwahi kuzungumzia kwa undani kuhusu mzunguko wa hedhi na jinsi mwanamke anavyoweza kupanga kupata ujauzito.Tuliona mpangilio wa kupata ujauzito huwa kwa mwanamke mwenye mzunguko unaopevusha mayai ambapo mwanamke huyu hupata ute wa uzazi.
Ute wa uzazi umegawanyika katika sehemu tatu ambapo ni ute mwepesi, ute mzito na unaovutika na ute mzito usiopevuka.Mwanamke atapata mimba endapo mayai yanapevuka kama tulivyoona dalili za ute, kwa hiyo ni muhimu mwanamke akafahamu mzunguko wake wa siku za ute wa uzazi, kama hufahamu vizuri siku za ute, kuna vifaa maalum unaweza kutumia mwenyewe ili kujua kama unapevusha mayai au la.
Mzunguko usiopevusha, mwanamke anaweza kuwa na mzunguko mzuri tu wa hedhi, anapata damu ya hedhi kama kawaida, mfano damu inaweza kutoka kawaida kati ya siku tatu hadi tano, hana shida nyingine yoyote lakini mimba hashiki kwa kipindi cha mwaka mmoja anapotafuta.
Nani anaweza kupata tatizo hili?
Mwanamke anayaweza kupata tatizo hili ni yeyote, mwanamke anaweza kuwa hana historia ya kupata ujauzito au hajawahi kutumia njia yoyote ya kuzuia mimba lakini anatafuta mtoto ndani ya mwaka mmoja anakosa.
Mwanamke mwenye historia ya kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango iwe bado anatumia au ameacha hivi karibuni, hali hii inaweza kumtokea. Mwanamke mwenye historia kama ameshawahi kuzaa mara moja au zaidi au alipata ujauzito au akatoa pia yupo katika hatari ya kupata tatizo hili.
Mwanamke ambaye anabadilishabadilisha hali ya hewa, mgonjwa, anayetumia baadhi ya dawa kwa muda mrefu hasa dawa za kansa na nyingine za magonjwa ambayo ni sugu, hupatwa na tatizo hili la kushindwa kupevusha mayai. Msongo wa mawazo pia huathiri upevushaji mayai.
Matatizo mengine yanayohusiana na tatizo hili ni kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi, maumivu ya tumbo ya muda mrefu chini ya kitovu, maumivu makali ya hedhi, maumivu wakati wa tendo la ndoa.
Wanawake wenye maambukizi ya mara kwa mara katika viungo vya uzazi husumbuliwa sana na tatizo hili. Maambukizi ya mara kwa mara katika viungo vya uzazi huambatana na kutokwa na uchafu ukeni wenye harufu na muwasho. Maambukizi hutokana pia na kutoa mimba au mimba kuharibika.
Mwanamke anayesumbuliwa na tatizo la maambukizi huathiriwa pia na mirija ya uzazi ambayo inaweza kuvimba kwa kujaa maji au usaha. Hali hii inapotokea, mwanamke huwa na maumivu chini ya tumbo kulia na kushoto.
Mirija ya uzazi huziba, uzibaji unaweza kuwa mwanzoni mwa kizazi au katika mwisho wa mirija ambapo vidole vya mirija  hujikunja na kushindwa kuchambua na kusafirisha mayai.
Dalili za kutopevusha  mayai
Mwanamke anakaa muda mrefu akitafuta mtoto kwa zaidi ya mwaka, haoni ute wa uzazi kama tulivyoeleza, anaweza awe na maumivu au asiwe nayo.
Siku za hedhi zinaweza kwenda vizuri au zinakuwa zimevurugika. Wengine hupoteza hamu ya kufanya tendo la ndoa. Kuvurugika kwa mzunguko ni  kutojua mpangilio wa siku za damu.
Nini cha kufanya?
Ukiwa unaendana na maelezo hapo juu, basi ni vuzuri ukamuona daktari bingwa wa masuala ya uzazi kwa uchunguzi wa kina.

No comments:

Post a Comment