Wiki
iliyopita tulieleza kwa kina tatizo la maambukizi katika njia ya mkojo,
leo tunaeleza dalili na tiba yake. Uwepo wa mawe katika figo na mirija
ya figo hata ndani ya kibofu pia ni mojawapo ya chanzo cha maambukizi
haya katika njia ya mkojo.
Dalili
Baadhi ya dalili za mtu kuambukizwa bakteria katika njia
ya mkojo kubwa ni maumivu wakati wa kukojoa, mkojo kuwa na rangi ya
njano kupindukia na kuwa na harufu kali japokuwa siyo kila mwenye dalili
hizo ana maambukizi katika njia ya mkojo au wengine huita UTI yaani
Urinary Tract Infection wana ugonjwa huu.
Dalili nyingine za maambukizi ni maumivu, kutokwa na usaha au
majimaji wakati wa kukojoa kabla au baada ya kukojoa kukiambatana na
maumivu na kuhisi moto wakati wa kukojoa mkojo. Baadhi ya wanaume wakati
mwingine hutokwa na majimaji katika njia ya mkojo wakati wa kujisaidia
haja kubwa.
Wengine wenye maambukizi hujikuta wakipata vichomi
katika njia ya mkojo, au kuhisi kuwashwa sehemu hiyo, kuumwa kiuno au
tumbo na kadhalika.
Mgonjwa anaweza pia kukumbwa na homa kali mara kwa mara na mwili kuwa
mchovu, kwa watoto hupoteza hamu ya kula na mwili kuonesha kuchoka.
Wagonjwa wengine hupata maumivu kwenye kibofu cha mkojo ambapo husikia
maumivu ya chini ya tumbo usawa wa kitovu na huwa hayaishi.
Matatizo haya ya mfumo wa mkojo kama tulivyoona huko juu huwapata watu wote wanawake na wanaume.
Watu wenye matatizo haya kila wakipima huambiwa wana UTI. Kwa
wanaume huhisi hata nguvu za kiume kupungua na wanawake hupoteza hamu ya
tendo la ndoa.
WAJAWAZITO
Kwa wajawazito ugonjwa unaweza kuhatarisha maisha yao
na mtoto aliye tumboni. Bakteria wanaweza kuingilia mfumo wa damu na
kwenda kusababisha madhara mengine kama vile shinikizo la damu kuwa
kubwa kwenye figo na hata kusababisha ufanyaji kazi mbovu wa figo.
TIBA
Maambukizi katika njia ya mkojo hutibika kwa dawa mbalimbali
za kisasa baada ya kufanyiwa vipimo na kuthibitika kuwa mgonjwa ana
maambukizi hayo.
Dawa ambazo anaweza kupewa ni kama vile
Ciprofloxacin--, Fosfomycin, Monurol, Furadantin, Sulfam ethoxazole,
co-trimax, ampicillin, gentamicin na kadhalika lakini asitumie dawa
yoyote bila kupata ushauri wa daktari.
Ushauri
Tunashauri kwa mwanamke kwamba epuka kujisafisha sehemu
za siri na maji yarukayo kwa kasi, pia epuka kupaka marashi sehemu hizo,
ama kutumia pedi zenye kemikali ya kukata harufu kwani hizo huua
bakteria wa asili wa ukeni hali ambayo hukaribisha bakteria wa maradhi
kuzaliana kwa wingi.
Ujisafishapo baada ya kujisaidia anzia mbele
kwenda nyuma kuepusha kuhamisha bakteria walio eneo la haja kubwa
kuingia njia ya mkojo.
Kwa wale walio katika kipindi cha ukomo wa hedhi, wanaweza
kushauriana na daktari juu ya kutumia aestrogen ya ukeni ili kuwasaidia
kujikinga na maambukizi.Kwa mwanaume maambukizi haya huathiri nguvu za
kiume na kujipenyeza hadi katika korodani na huathiri uzalishaji wa
mbegu za kiume na kukufanya uwe mgumba.
Maambukizi ya njia ya mkojo huweza kusababisha matatizo ya tezi ya kiume (prostate), hivyo mgonjwa anatakiwa kumuona daktari.
No comments:
Post a Comment