KWANZA
nianze kwa kuwashukuru wasomaji wote wa safu hii, waliowasiliana na
mimi kwa namna moja au nyingine, katika kubadilishana mawazo juu ya
uhusiano. Ni faraja kugundua kwamba wapo watu wanaofuatilia
unachokiandika na kisha kutaka kuchangia neno.Mada
yangu ya leo inaweza kuniletea ugomvi na waajiriwa wenzangu wanawake,
lakini panapo ukweli ni vyema tukasema, kwa sababu unasaidia katika
kurekebisha na wakati mwingine hata kujua jinsi gani unaweza kujihami,
ili kutokusaliti ndoa au uhusiano wako wa kimapenzi.
Nina uzoefu kidogo na mambo ya kazi za ajira maofisini, nimefanya
hivi kwa muda mrefu. Wakati flani nilifanya kazi katika ofisi zilizo
katikati ya jiji, kule mitaa ya Posta jijini Dar es Salaam.
Ofisi
nyingi za serikali na watu binafsi zinapatikana mitaa ile. Kutokana na
sababu hiyo, kuna idadi kubwa pia ya migahawa, hoteli, mama ntilie, pub
na kadhalika.
Kuna mambo mawili makubwa yenye ushawishi mkubwa wa usaliti. Ofa za
chakula au vinywaji na usafiri. Kwa kawaida, wafanyakazi wa ofisi moja
hupenda kutoka pamoja wakati wa chakula cha mchana, wenyewe tunapendelea
zaidi kusema lunch!
Kila mmoja ana sehemu yake anayokula kulingana na kipato chake, wapo
wanaokwenda Southern Sun kupata chakula cha mchana, na wapo wanaowafuata
mama ntilie wanaojibanza kwenye vichochoro vingi vilivyopo mjini.
Huko ndiko tunakokutana na akina dada waliovalia vizuri na kupendeza,
wakitokea katika maofisi mbalimbali, huwezi kujua yupi ni mhudumu wa
chai, yupi ni bosi, wote wanang’ara. Na hapa ndipo ofa za misosi
zinapoanza kushawishi ngono.Kijana
mmoja mwenye kipato kikubwa ofisini kwake, atavutiwa na msichana mrembo
mwenye mshahara wa wastani. Ili kumsogeza karibu, atalipia chakula cha
siku hiyo na kumualika kwa kesho yake. Kulipiwa chakula ni jambo dogo,
lakini lenye thamani kubwa sana. Si rahisi mtu aliyekulipia chakula kwa
nia njema, ukaacha kumshukuru na hata kumwelekeza unapofanya kazi.
“Mimi nipo pale Oj Traders,” msichana anaweza kujita mbulisha jina na
kusema anapofanyia kazi huku mkaka akimweleza kuwa yeye ni mhasibu
katika ofisi flani. Watakapo
kutana mara ya pili, wataachiana namba za simu.
Baada ya hapo, mkaka atafanya mbwembwe za kuhamahama maeneo ya lunch ili mradi tu mdada wa watu aingie kwenye laini.
Ukimaliza suala la lunch, kuna hii kitu foleni, hasa kwa wakazi wa
Dar es Salaam. Raha ya kufanya kazi katikati ya jiji inaingia shubiri
kadiri jioni inavyozidi kusogea. Kuanzia saa kumi, ni vurugu katika
vituo vya daladala na hasa wakati kama huu ambao bodaboda zimezuiliwa
kuingia mjini.
Wenye magari binafsi ndiyo wakati wao wa kujidai, ingawa foleni
inawakumba wote. Lakini ni afadhali ukiwa kwenye foleni ndani ya gari
dogo, mko wawili kuliko foleni, umeshika bomba kwenye daladala.
Siyo
rahisi kwa mdada kukataa lifti ya kijana mwenye gari. Na katika foleni
ndefu, ni wazi kwamba hadi mwisho wa safari, watakuwa wameshabadilishana
namba. Kwa msichana, kuwa na uhakika wa usafiri kila siku ni ukombozi.
Tusidanganyane, hakuna msichana ambaye hatajua kuwa lunch au usafiri
anaopewa unahitaji malipo maalum, ambayo ni penzi. Hali hii haiko Dar
tu, bali nchi nzima na pengine duniani kote.
Mwanamke aliyeajiriwa
anakuwa katika mitihani mikubwa zaidi ya kusaliti ndoa au uhusiano wake,
kwa sababu hata kama haitakuwa kwenye chakula au usafiri, bado watu
anaokutana nao katika utendaji wake, wanaweza kumghasi. Fikiria
anakutana na mabosi, marafiki wa mabosi wake, wafanya biashara, atapona
kweli?
Hata hivyo, simaanishi kama tabia hii inawakumba waajiriwa wote, isipokuwa nadhani ni sehemu kubwa wanahusika!
No comments:
Post a Comment