Na Richard Bukos
MSHAMBULIAJI
nyota wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, Mrisho Khalfan Ngassa,
amefunguliwa kesi ya madai ya talaka namba 30/2014, katika Mahakama ya
Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam na mkewe Latifa Abdul Fundi.
Ngassa amefunguliwa kesi hiyo akidaiwa kumtelekeza na kumnyima
matunzo ya ndoa mke wake tangu Juni mwaka 2011, migogoro ilipoanzia.
Kesi hiyo iliyoanza kuunguruma Baraza Kuu la Waislamu nchini
(Bakwata), Kitengo cha Mashauri ya Ndoa, mambo yalikwenda ndivyo sivyo
kufuatia Ngassa kutotoa ushirikiano katika baraza hilo.
Baada ya baraza hilo kushindwa kesi hiyo, liliihamishia mahakamani
hapo ambapo juzi (Jumatatu), mchezaji huyo na mkewe walitakiwa kupanda
kizimbani mbele ya hakimu waliyepangiwa, Timothy Lyon, lakini Ngassa
alishindwa kutokea kutokana na majukumu aliyokuwanayo kwenye timu ya
taifa iliyokuwa nchini Burundi.
Kufuatia udhuru huo, Hakimu Lyon aliiahirisha kesi hiyo mpaka
Septemba 30, mwaka huu ambapo Ngassa na Latifa wanatakiwa kupanda
kizimbani katika shauri hilo.
Katika kesi hiyo, Latifa anamdai, Ngassa talaka pamoja na mgawanyo wa
mali walizochuma wakiwa katika ndoa yao ikiwemo nyumba mbili, moja
iliyopo Yombo na nyingine Tegeta Basihaya jijini Dar es Salaam.
Kiwanja kimoja kilichopo Tegeta Basihaya jijini, gari aina ya Toyota
Cresta, vitanda viwili, kabati dogo la vipodozi, seti ya masofa, meza,
pasi ya umeme, majiko mawili ya kupikia, televisheni, redio kaseti,
brenda na draya.
Pamoja na mali hizo, Latifa anamdai Ngassa ampe pesa taslimu shilingi
laki mbili na nusu (250,000/) kila mwezi, tangu Juni 2011, mpaka siku
ya hukumu ambazo ni kwa ajili ya matunzo tangu alipositisha kumhudumia.
Jalada la kesi hiyo liliambatanishwa na cheti cha ndoa kinachoonyesha
wawili hao walifunga ndoa Mei Mosi, mwaka 2009, mashahidi wakiwa Imani
Madega na Saidy Rashid.
No comments:
Post a Comment