KWANZA kama ilivyo ada nimshukuru Mungu kwa kuniweka hai nikiwa na afya njema.
Wiki iliyopita nilieleza jinsi muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ulivyozitesa serikali za muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Nikasema kamati na tume nyingi ziliundwa na fedha za walipa kodi, nyingi
zikatumika lakini mgogoro upo palepale.
Kuna walioshauri kuwa rais alivunje bunge lakini Mwanasheri Mkuu wa
Serikali, Frederick Werema akasema, hawezi kulivunja kwa sababu sheria
haimruhusu, kwa maneno mengine hana meno ya kumaliza tatizo.
Lakini sasa imedhihirika kuwa hatima ya Bunge Maalum la Katiba
imebaki mikononi mwa Rais Jakaya Kikwete, yuleyule aliyetajwa kuwa hana
mamlaka ya kulivunja baada ya kuandikiwa barua na uongozi wa bunge hilo
akitakiwa atoe ufafanuzi wa kisheria kuhusu tarehe ya mwisho ya kumaliza
vikao vyake lakini pia alikutana na wapinzani wa serikali yake.
Ameandikiwa barua kutokana na muda uliopangwa kwenye ratiba ya bunge
hilo kuzua utata wa kisheria na kuwapo uwezekano wa mwingiliano na Bunge
la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi (BLW), Zanzibar.
Ratiba ya Bunge Maalum la Katiba inaonyesha kuwa limepanga
kuhitimisha vikao vyake mwishoni mwa Oktoba, tofauti na tarehe
iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete Julai 28, mwaka huu ambayo
ilitangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) namba 254 la Agosti Mosi.
Tangazo la rais linaonyesha kuwa awamu ya pili ya Bunge Maalum
ingeanza Agosti 5, 2014 na kumalizika Oktoba 4, lakini ratiba ya Bunge
hilo inaonyesha kuwa litamalizika Oktoba 31, siku ambayo Mwenyekiti wa
Bunge hilo, Samwel Sitta anatakiwa akabidhi kwa rais Katiba
inayopendekezwa.
Hadi tunapoandika makala haya serikali bado haijatoa tangazo lingine
kwenye gazeti la serikali kuongeza muda hadi mwishoni mwa Oktoba kama
alivyosema Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Sitta wakati akitoa
ufafanuzi wa siku 60 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge hilo, Agosti 5,
mwaka huu.
Sitta alisema kwa kadiri ya tafsiri, siku za kazi ni Jumatatu hadi
Ijumaa ambazo wajumbe wanapaswa kufanya kazi na kwamba Jumamosi na
Jumapili siyo sehemu ya siku 60 zilizoongezwa na rais.
Kuna mchanganyiko mkubwa kwani Katibu wa Bunge Maalum, Yahya Khamis
Hamad alisema hawajapata maelekezo ya ziada kutoka serikalini ambako
waliiandika barua ya kuomba ufafanuzi wa kisheria kuhusu suala hilo.
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alikiri ofisi yake kupokea barua
kutoka Bunge Maalum ikiomba ufafanuzi ambao ungeliwezesha kuongeza siku
kwa lengo la kukamilisha kazi ya kujadili na kuandika katiba
inayopendekezwa na kwamba maombi yao bado yanafanyiwa kazi.
Utata wa kisheria
Licha ya ahadi iliyotolewa na Sitta ni dhahiri kwamba suala hilo lina
utata wa kisheria kutokana na kauli iliyowahi kutolewa na Mwanasheria
wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema wakati akitoa ufafanuzi wa maana
ya siku 70 ambazo bunge lilikaa mara ya kwanza.
Baada ya kusoma hati ya rais ya kuitishwa kwa bunge hilo, Februari
mwaka huu, Jaji Werema alisema siku 70 zilizotolewa kwa mujibu wa
tangazo la serikali ni za kikalenda na siyo siku za kazi kwa sababu
wajumbe wa Bunge Maalum siyo watumishi wa kuajiriwa.
Kauli ya Jaji Werema haijawahi kutenguliwa na Mahakama au yeye
mwenyewe na kwa msingi huo, kwenda kinyume chake ni kuvunja Sheria ya
Kazi na Majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268 ya 2005.
Mgogoro mwingine unaojitokeza ni ratiba za vikao vya Bunge la
Muungano ambalo limepangwa kuanza Novemba 4, 2014 na Baraza la
Wawakilishi ambalo limepangwa kukutana kuanzia Oktoba 22, mwaka huu.
Kwa kawaida, vikao vya Bunge hutanguliwa na wiki mbili za vikao vya
kamati za kudumu na ikiwa ratiba itabaki kama ilivyo, basi vitaingiliana
na vikao vya Bunge Maalum ambalo ratiba yake imepangwa kuendelea hadi
Oktoba 31, mwaka huu.
Hakuna ambaye atabisha nikisema kuwa kwa jinsi ratiba ya Bunge
Maalum la Katiba ilivyopangwa lazima itaingilia shughuli za Bunge la
Muungano na lile la Baraza la wawakilishi hivyo uamuzi unapaswa ufanywe
ili kuepusha mgongano huo.
Njia pekee ni kumuomba Rais Kikwete asogeze mbele vikao vya mabunge
mengine ili Bunge Maalum la Katiba lipate nafasi ya kuendelea na kikao
japokuwa wapo walioona kuwa hana uwezo wa kulisitisha au kusogeza mbela
vikao vyake.
Hakika masuala haya ni mazito na yanatakiwa kutafutiwa ufumbuzi
haraka. Lakini wengi tunajiuliza, waliokuwa wakipanga vikao vya Bunge
Maalum la Katiba walikuwa hawayajui hayo? Au ni kutaka kumchosha rais
bure na kumsababishia atupiwe lawama?
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
No comments:
Post a Comment