Saturday, 6 September 2014

Pigo Jingine Bunge Maalumu la Katiba, Linapoelekea Sipo Kabisa

Kuna dalili hali si shwari ndani ya Bunge Maalumu la Katiba baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kujiuzulu ujumbe wa Kamati ya Uandishi wa Katiba inayopendekezwa.

Habari za uhakika zilizopatikana jana bungeni mjini Dodoma, zinaeleza kuwa kigogo huyo wa SMZ amemwandikia barua Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta akimwarifu juu ya uamuzi wake huo.

Kamati hiyo ndiyo moyo wa Bunge hilo katika kuandika vifungu, ibara na sura za rasimu kulingana na mapendekezo ya kila kamati na baada ya majadiliano na mwisho inawajibika kuandika Katiba itakayopendekezwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

Kujiengua kwake ni pigo kwa Bunge Maalumu, kwani kunapunguza uhalali wa Katiba itakayopendekezwa kwani Othman akiwa Mwanasheria Mkuu wa upande huo wa Muungano ndiye anayepaswa kuwa kinara wa kulinda masilahi ya Zanzibar wakati wa uandishi wa Katiba inayopendekezwa.

“Ni sahihi kwamba nimejiuzulu…hizo sababu ndiyo siwezi kukutajia maana kwa mujibu wa taratibu za Bunge Maalumu zinapaswa kuzungumzwa na Mwenyekiti maana barua yangu ya kujiuzulu anayo yeye,”alisema Othman alipozungumza na gazeti hili kupitia simu yake ya mkononi jana.

No comments:

Post a Comment