Kutwa
nzima ya jana, viongozi wa Bunge Maalumu walishinda kwenye vikao vya
mashauriano huku wabunge wa CCM wakitarajiwa kukutana jana usiku kwenye
makao makuu ya chama hicho kupewa taarifa rasmi za uamuzi huo.
Katika
makubaliano baina ya TCD na Rais Kikwete, imeamuliwa kuwa uamuzi wa
Rais kupitia Tangazo la Serikali (GN) 254 la kuongeza siku 60 hadi
Oktoba 4 uheshimiwe na baada ya tarehe hiyo Bunge liahirishwe.
Uamuzi
huo ni kinyume cha azimio la Bunge Maalumu la Agosti 5, 2014 ambalo
lilirekebisha Kanuni ya 14 (4) na kuifuta Jumamosi katika siku
zilizotajwa kuwa za kazi, pia sikukuu na siku za Jumapili.
Mwenyekiti
wa Bunge, Samuel Sitta alikaririwa akiwaambia wajumbe wa Bunge hilo
kwamba Rais alikuwa ameridhia kwamba siku 60 alizotoa hazingejumuisha
Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu.
Ni
kwa msingi huo, Bunge hilo likapanga kwamba lingeendelea na shughuli
zake hadi Oktoba 31, wakati Mwenyekiti wa Bunge atakapokabidhi Katiba
inayopendekezwa kwa Rais Kikwete.
Hata
hivyo, makubaliano yaliyofikiwa baina ya viongozi wa TCD na Rais
yanaonekana kuvuruga kabisa ratiba ya Bunge hilo ambalo jana na juzi,
Kamati ya Uongozi ilikutana mara kadhaa kuona jinsi ya kunusuru mchakato
huo.
Ingawa
haikufahamika mara moja kama vikao hivyo vya kamati ya uongozi
inayoongozwa na Sitta mwenyewe vinajadili nini, lakini taarifa zimedai
huenda kukawa na mabadiliko makubwa ya ratiba.
Habari
nyingine zinadai kwamba mabadiliko hayo huenda yakapunguza muda wa
baadhi ya shughuli za kazi za Bunge hilo ili liweze kukamilisha kazi
yake ikiwamo wajumbe kupiga kura ya uamuzi.
Katika
kikao cha jana asubuhi, kamati hiyo ilishindwa kurekebisha ratiba yake
ili iendane na siku zilizosalia, hivyo kuahirishwa kwa kuwapa kazi
wataalamu wake kuleta mapendekezo ambayo yangejadiliwa jana mchana.
Katibu
wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alithibitisha jana kwamba ratiba
ya Bunge imebadilika kutokana na hoja nyingi kukubalika ndani ya kamati.
“Kamati
ya uongozi itakutana baadaye (jana) kuangalia vipengele ambavyo
hawakukubaliana kwenye kamati ndivyo wavipangie muda na ratiba
itajulikana baada ya kikao hicho,” alisema Hamad.
Hofu ya akidi
Hata
hivyo, habari zaidi zinadai kwamba uongozi wa Bunge Maalumu
ulichanganywa na kuwapo kwa hoja za baadhi ya wajumbe wake kutaka kwenda
Makka kwa ajili ya kushiriki Ibada ya Hijja, hali inayotishia akidi kwa
ajili ya kuendesha vikao.
Kanuni
za Bunge Maalumu zinataka kuwapo kwa nusu ya wajumbe kutoka pande zote
za Muungano wakati wa kuendesha vikao vyake na theluthi mbili ya wajumbe
hao kila upande wakati wa kufanya uamuzi au kupiga kura.
“Tumetoka
kwenye kikao mchana huu na pengine tutaitana tena maana hatujafikia
mwafaka, kuna mambo mengi yamejitokeza lakini kubwa ni hili la wenzetu
ambao wanataka kwenda Hijja, kuondoka kwao kunaweza kuathiri akidi kwa
kiasi kikubwa,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kamati hiyo.
Kutokana
na matakwa hayo, hivi sasa Ofisi ya Katibu wa Bunge inafanya tathmini
ili kufahamu idadi ya wajumbe ambao watakwenda Hijja Septemba 22, mwaka
huu, ambao wengi wanatoka Zanzibar.
Hamad alikiri kwamba kuna mambo mengi ambayo ofisi yake inayafanyia kazi na kwamba hilo la Hijja ni mojawapo... “Kwa
sasa siko katika nafasi ya kuzungumza kwa kirefu, kikao cha Kamati ya
Uongozi kimeisha na bado kuna kazi nyingi za kuona jinsi
tunavyoendelea.”
Tayari
Bunge hilo limetikiswa na kutokuwapo kwa wajumbe waliosusia vikao tangu
Aprili 16, mwaka huu ambao ni wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) ambao unaundwa na vyama vya CUF, Chadema na NCCR
Mageuzi na baadhi kutoka Kundi la 201.
Taarifa ya TCD
Jana
saa 7:00 mchana, Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo alikutana na wanahabari
na kueleza kuwa katika mazungumzo yao na Rais wamekubaliana mambo matano
ya msingi kwa mustakabali wa nchi.
Alisema
pamoja na kazi ya msingi iliyofanywa na Bunge Maalumu, mchakato
unaoendelea hauwezi kutoa Katiba Mpya ambayo itatumika katika Uchaguzi
Mkuu wa 2015.
“Muda
hautoshi kukamilisha mchakato na kufanya mabadiliko yatakayohitajika ya
sheria, kanuni na taasisi mbalimbali zinazohitajika,”alisema Cheyo ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP).
Alisema
kura ya maoni ilipangwa kufanyika Aprili 2015 na kama itabidi irudiwe,
basi itabidi irudiwe itakuwa Juni au Julai 2015, muda ambao Bunge la
Jamhuri linatakiwa livunjwe.
“Ili
Katiba Mpya itumike katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, itabidi uhai wa Bunge
na Serikali uongezwe zaidi ya 2015, jambo ambalo sisi viongozi wote
hatuliungi mkono,” alisema Cheyo.
Alisema
kwa kutambua kuwa kama kura ya maoni ikifanyika, italazimisha Uchaguzi
Mkuu wa 2015 kuahirishwa, wamekubaliana kura hiyo iahirishwe hadi baada
ya uchaguzi huo.
Bunge Maalumu
Cheyo
alisema Bunge Maalumu kwa sasa linafanya kazi kwa mujibu wa Tangazo la
Serikali (GN), namba 254 lililotolewa na Rais Kikwete ambalo uhai wake
utakoma Oktoba 4.
“Inategemewa
kuwa Oktoba 4 Katiba inayopendekezwa itapatikana. Tulikubaliana hatua
hii iachwe ifikiwe na baada ya hapo Bunge liahirishwe hadi baada ya
Uchaguzi Mkuu 2015.
“Tarehe
4 Oktoba ndiyo mwisho. Hiyo ndiyo sheria iliyopo, sisi hatuna mamlaka
ya kuandika GN mpya, GN imetolewa na Bunge hili liko kihalali.
Tulichokuwa tunabishana lisife kesho,” alisema.
Akijibu maswali ya wanahabari kama ana uhakika Bunge hilo litaweza kukamilisha kazi yake ndani ya siku zilizobaki, Cheyo alisema“Tumeheshimu
sheria iliyopo tarehe nne Watanzania wanategemea Katiba Mpya itakuwa
imepatikana, sasa kama haitapatikana hilo msiniulize kwa sababu hilo si
jukumu langu.”
Alipoulizwa kama rais ajaye baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 ataendeleza mchakato pale ulipoishia alisema:
“Naomba
Mungu rais ajaye awe anayejali maoni ya wananchi hilo naomba kabisa.
Sasa tukipata rais ambaye hatutambui sisi wote na mawazo yetu, basi
tutakuwa tumekosea katika kupiga kura.”
Mabadiliko ya 15 ya Katiba
Cheyo
alisema kwa vile Uchaguzi Mkuu wa 2015 utafanyika kwa kutumia Katiba ya
1977, ni vyema yakafanyika mabadiliko madogo ili kuruhusu uchaguzi huru
na wa haki.
Mabadiliko
hayo yatalenga kuwezesha uwapo wa tume huru ya uchaguzi, mshindi wa
urais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50, kuruhusu mgombea binafsi na
kuingiza ibara itakayoruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani.
“Vyama
vya siasa ambavyo vinapenda kupendekeza mambo mengine ya kurekebisha
katika Katiba ya 1977 vinaombwa kufanya hivyo kwa vile muda tulionao ni
mdogo,” alisema Cheyo.
Alisema
walikubaliana kuwa marekebisho hayo yafanyike katika Bunge la Jamhuri
litakaloanza Novemba 5 na ikishindikana yafanywe Februari 2015.
Ukawa kurudi bungeni
Cheyo
alisema suala la kurudi au kutorudi ndani ya Bunge Maalumu la Katiba
kwa wajumbe wa Ukawa halikuwa sehemu ya mkutano kati ya Rais na TCD.
No comments:
Post a Comment