*Ni wa kujenga maghala makubwa ya kuhifadhia chakula
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kupata
mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland utakaoliongezea
Taifa uwezo wa kuhifadhi chakula tofauti na hali ilivyo sasa.
Alisema
uzalishaji mwaka huu umetoa ziada ya tani milioni 1.5 za nafaka na tani
800,000 za mpunga ikilinganishwa na ziada ya tani 300,000 iliyokuwepo
mwaka jana. “Serikali inakabiliwa na changamoto ya kupata soko la
uhakika kwa mazao ya wakulima kwa sababu tulizoea kumtumia Wakala wa
Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kama mnununzi mkuu na uwezo wezo wake
ni tani 240,000 tu kwa mwaka,” alisema.
Akizungumza baada ya kutembelea kampuni
ya MLYNPOL ambayo inanunua mazao kwa wakulima na kusindika nafaka jana
mchana (Ijumaa, Oktoba 24, 2014) Waziri Mkuu alisema teknolojia ya
ujenzi wa maghala makubwa ya kuhifadhia chakula katika muda mfupi ndiyo
suluhisho pekee kwa wakulima wa Tanzania katika kipindi tulichonacho.
“Wenzetu
wana teknolojia ya kisasa ya ujenzi wa SILOS (maghala makubwa ya
kuhifadhia chakula) pamoja na namna bora ya kuhifadhi chakula, na sisi
tuna changamoto ya kuwasadia wakulima kuuza mazao kutokana na uzalishaji
mkubwa wa nafaka ambao umetokea mwaka huu,” alisema.
Alisema ni mapema mno
kujua kiasi cha fedha ambacho Serikali inatarajia kukopa lakini
alithibitisha kwamba atatuma timu ya wataalamu kutoka sekta husika ili
wafanye mazungumzo rasmi na Serikali ya Poland na kukamilisha taratibu
za upatikanaji wa mkopo huo.
Waziri Mkuu ambaye
alisafiri km. 500 kwenda mji wa CHOJNOW kilipo kiwanda cha kutengeneza
maghala (SILOS) na kusindika nafaka aliguswa na teknolojia inayotumika
kwenye kiwanda hicho cha MLYNPOL ambapo kwa siku moja kina uwezo wa
kusindika tani 360,000.
Mji wa CHOJNOW upo
kusini Mashariki mwa Poland na pia hauko mbali na mipaka ya nchi za
Ujerumani, Czeck na Austria. Kwa gari dogo ni kati ya saa 3 hadi 4 hadi
kufika miji mkuu ya nchi hizo ambayo ni Berlin, Prague na Vienna.
Akitoa maelezo kwa
Waziri Mkuu, mmiliki wa kiwanda hicho kikubwa nchini Poland, Bw. WITOLD
KARCZEWSKI alisema kiwanda hicho kinaposindika ngano kina uwezo wa kutoa
unga laini wa mikate (refined flour), unga wa lishe (grain/brown
flour), unga wa kutengeneza pasta na tambi na wa mwisho hutolewa kwa
ajili ya chakula cha mifugo.
“Nafaka zikifika,
zinasafishwa, zinakaushwa, zinapimwa unyevunyevu uliopo na kuanza
kusindikwa kulingana na aina ya nafaka inayoletwa. Tunakusanya mazao
haya kutoka kwa wakulima kwenye majimbo 16 ya nchi hii,” alisema.
Akifafanua kuhusu
matumiai ya umeme kwenye kiwanda hicho, Bw. ALEKSANDR ZINGMAN ambaye pia
ni mshauri na mbia wa Bw. KARCZEWSKI, alisema kiwanda hicho kinatumia
megawati moja ya umeme kwa saa moja lakini matumizi yanaweza kupungua
kuligana na ukubwa ama udogo wa kiwanda.
“Kama Serikali inahitaji kiwanda kidogo zaidi ya hapa, tunaweza kuwajengea na matumizi ya umeme lazima yatapungua,” alisema.
Kampuni ya MLYNPOL ina wafanyakazi 250 ambao kato yao, 200 wanafanya kazi kiwandani kwa shifti tatu za saa nane nane kila moja.
Waziri Mkuu anamalizia
ziara yake ya siku tatu nchini Poland jana mchana ambapo asubuhi
alikutana na Watanzania waishio Poland na baadaye kufanya vikao na
baadhi ya wafanyabiashara wa jiji la Warsaw. IMETOLEWA NA: OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment