Namshukuru
Jalali kwa kuniwezesha kukutana tena na wewe msomaji wangu mpendwa wa
safu hii nzuri ambapo tunajuzana, kushauriana na kuelimishana kuhusu
mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi.
Mada
yetu ya leo, kama inavyojieleza kwenye kichwa cha habari, ni mambo
unayopaswa kuyafanya unapogundua mpenzi wako amekusaliti wakati bado
unampenda na unahitaji kuendelea kuwa naye katika uhusiano wa kimapenzi.
Vitabu vya dini zote vinaeleza kuwa kosa pekee linaloweza kuivunja
ndoa, hata ile iliyofungwa kwa baraka za Mungu, iwe ni madhabahuni au
msikitini, ni USALITI. Yaani hata kama ulikuwa unampenda vipi, ikitokea
amekusaliti na umegundua ukiwa na ushahidi, una haki zote za msingi za
kutoa/kudai talaka au kuachana kabisa (kama bado hamjaoana).
Hata hivyo, kuna mazingira ambayo yanaweza kukutokea, ukagundua mkeo,
mumeo, mchumba au mpenzi wako amekusaliti lakini kutoka ndani ya moyo
wako, ukawa haupo tayari kuachana naye kwa sabahu bado unampenda sana
licha ya kwamba amekukosea.
Kutokana na maombi maalum ya wasomaji wangu kadhaa ambao wamekutana
na hali kama hiyo na hawajui cha kufanya, ndiyo maana leo nimeamua
tuijadili mada hii na wewe msomaji wangu.
Naamini mimi peke yangu
sijui kila kitu wala ushauri wangu hauwezi kuwa wa mwisho lakini nataka
kukushirikisha wewe msomaji wangu, hebu niambie utafanya nini
unapotokewa na tukio kama hili? Unampenda kwa moyo wako wote, umemfanyia
mambo mengi lakini mwisho ukagundua kuwa amekusaliti, utafanya nini?
Mapenzi yamegeuka shubiri, usaliti na maumivu ya moyo yamegeuka na
kuwa sehemu ya kawaida katika uhusiano wa kimapenzi. Watu wengi wanalia
kwa sababu wanasalitiwa au waliwahi kusalitiwa na wenzi wao, si
wanawake, si wanaume, si wanandoa, si wachumba wala wapenzi!
Zipo sababu nyingi zinazosababisha usaliti lakini lengo langu leo
siyo kuzungumzia hilo bali ni kujaribu kuiponya mioyo ya wote
waliojeruhiwa na watu wanaowapenda sana kwa kuwasaliti.
Yawezekana
ulitokea kumpenda sana mwenzi wako, ukaamini wewe ndiyo kila kitu kwake,
ukamtimizia kila kilichokuwa ndani ya uwezo wako lakini mwisho,
ukaambulia maumivu baada ya kugundua kuwa yupo mwingine anayekuibia mali
zako.
Sitaki kupingana na maandiko ya vitabu vitakatifu au sheria ambazo
zipo wazi kwamba malipo ya usaliti ni kuvunjika uhusiano lakini nataka
tujadiliane, ni lazima kila unapogundua kuwa mwenzi wako amekusaliti
dawa yake ni kupeana talaka au kuachana kwa ugomvi?
Mathalani
umefunga ndoa na kuishi na mwenzi wako kwa kipindi kirefu mkipendana,
kujaliana na kuoneshana kila aina ya mahaba lakini akateleza na
kukusaliti ilihali bado anakupenda na wewe unampenda, utakapoamua
kuachana naye na kwenda kwa mwingine, ukigundua naye anakusaliti
utafanya nini? Utaachana na wangapi?
Siyo mara zote talaka au kuachana huwa suluhisho la usaliti ndani ya
ndoa. Siwafundishi watu wasaliti ndoa zao au uhusiano wao kwa makusudi
wakitegemea kusamehewa, hapana.
Nataka uelewe kwamba hata baada ya
mwenzi wako kukusaliti, bado mna nafasi ya kuendelea na maisha yenu
ikiwa wote wawili mtaamua kulishughulikia tatizo hilo kwa kina bila
kujali watu wa nje wanasemaje.
Usikilize moyo wako, ni kweli amekusaliti! Amekuumiza, unahisi dunia
yote imekuelemea, unatamani kufa au kuua, lakini je, moyo wako
unakuambia nini? Upo tayari kumruhusu mwizi wako ndiyo awe mmiliki
halali wa mwenzi wako ambaye bado unampenda?
Naiweka hoja mezani mpaka wiki ijayo tutakapokutana kwa ajili ya
mwendelezo, nataka tujadiliane na wewe msomaji wangu. Fikiria kwa kina
kisha uniambie mawazo yako.
No comments:
Post a Comment