MJINI
kuna maneno mengi kweli yanasemwa, kila siku linazaliwa jipya. Lakini
mara zote, kinachoendelea ni kujifariji tu. Eti mara utasikia mjini
hakuna wazee kila mtu baby, wapiii. Wazee wapo wengi sana, sema tu
wanajitoa ufahamu.
Kati
ya mambo yanayojadiliwa sana mitaani, hasa inapotokea mtu amefumaniwa
ni ile kwamba mke au mume wa mtu ni sumu. Hivi ni kweli jamani ni sumu?
Moja kati ya ahadi muhimu sana ya uandishi tunayofundishwa, ni
kusimamia katika ukweli, hata kama wakati mwingine unaweza kukuumiza
wewe mwenyewe. Baadhi ya mambo tunajua ukweli wake, lakini labda ili
tuonekane tunazingatia mila na desturi zetu, tunaukana.
Kwa mfano, tunasema mke au mume wa mtu ni sumu, hivi ni kweli
tunasema kutoka moyoni? Sina uhakika, lakini tukisema Mungu atokee
ghafla na kusimama mbele yetu kisha aseme ambaye hajawahi kutembea na
mke au mume wa mtu atoke mbele, simuoni atakayejitokeza.
Wengi tunashiriki tendo hili ovu, ila tu inapotokea mwenzetu mmoja 40
zake zimefika, ndipo tunasema mke au mme wa mtu sumu. Juzikati
nilikutana na dada mmoja aliyeomba nimshauri kidogo kuhusu jinsi
anavyotakiwa aishi na mpenzi wake.
Lakini kadiri tulivyokuwa tukizungumza, hatimaye nikabaini kwamba
kumbe mpenzi anayemzunguzia, ni mume wa mtu. Ni binti wa miaka 20 na
mwenzake ana miaka 50, baba wa familia yenye watoto wanne.
Msichana anaonekana amekufa kwelikweli kwa huyo mbaba, maana anataka
naye awe analala nyumbani kwake, walau mara mbili kwa wiki, kitu ambacho
mwanaume anakipinga, yeye hataki kulala nje ya mke wake, lakini yupo
tayari kuwa naye kila wakati mchana kutwa.
“Yaani huyu baba jamani, natamani tu niwe nachat naye kila saa,
nampenda sana. Najua ni mume wa mtu, lakini nampenda, siamini wanaosema
mume wa mtu sumu, mbona huyu baba mtamu sana?”
Huyu dada ni mmoja
kati ya maelfu wanaotembea na wanawake au wanaume wa wenzao. Uzoefu
unaonyesha kuwa ni wanandoa wachache wanaoficha kuwepo katika uhusiano.
“Mke
wako akijua je, wee mi naogopa kupigwa” ni maneno yao akina dada
wanapotongozwa na waume za watu. Ingawa hujichelewesha, lakini mwisho wa
siku hukubali kuwa katika uhusiano.
Unamkuta mtu yuko bize na simu, anachat na aliyemsevu kwa jina la
Baby, ukimfuatilia, ni mume wa mwenzie!Hata wanaume, wanajua kabisa huyu
binti anayemmezea mate ni mke wa mtu, lakini kwa makusudi anampa
majaribu, anamkaribisha lunch, kumtoa out, anampeleka shopping na vitu
chungu nzima za ulaghai, mwisho wa siku wanafanya kile ambacho wenyewe
wanasema ‘tunaiba’.
Kama tutafanya sensa sasa hivi, tutagundua kwamba asilimia kubwa ya
wasichana tunaopishana nao mitaani, wanatoka na waume za watu, lakini
wakiona fumanizi la mwenzao, wanasema mume wa mtu sumu.
Pamoja na ukweli huu kuwa mchungu, lakini bado inawezekana sana
kujihadhari na wake au waume wa watu kwa sababu kama tunavyoshuhudia
mara zote, ni hatari sana. Tunawaona wanaume wanaokutwa wanavyofanyiwa
unyama na wengine hata kutolewa roho.
Tatizo ni kubwa zaidi kwa wasichana wanaosema kuwa ni afadhali ya
kuwa na wapenzi watu wazima kuliko vijana wenzao, kwani siyo waaminifu
katika uhusiano wao. Kwa hiyo wanaona hata kama atakuwa ni mume wa mtu,
lakini angalau anamuondolea stress na kumpa mahitaji yake muhimu ya
maisha.
No comments:
Post a Comment