Friday, 3 October 2014

AFYA::UCHOVU MARA KWA MARA NI DALILI ZA KISUKARI?

Ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa hatari kutokana na madhara yake kuwa makubwa endapo mtu  hatazingatia uchunguzi na matibabu.
Ugonjwa huu umegawanyika katika makundi mawili ambayo kitaalamu tunaita ‘Type One’ na mwingine ‘Type Two.’‘Type one’ siyo tatizo sana ingawa ni tatizo kwa wale waliokuwa nao, ni aina ya kisukari mtu anakuwa nao tangu utotoni ambapo hukosa kabisa kichocheo cha ‘Insulin’ ambacho kipo mwilini kikiwa na kazi ya kushusha sukari iliyozidi na kuiweka sawa iliyopo.
Aina ya kisukari ‘Type Two’ ndiyo janga kubwa la sasa hivi. Aina hii humpata mtu yeyote hata wewe unayesoma hapa usipoangalia huchomoki.Aina hii ipo sana katika jamii kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha.
Mabadiliko haya ya mitindo ya maisha humletea mtu kisukari na athari zake tutaziona. Mabadiliko tunayozungumzia ni maisha kuwa mazuri.
MABADILIKO YA MAISHA NA UGONJWA
Inawezekana kabisa maisha yanapokuwa mazuri ukawa na uhuru wa kuchagua unachokula na unachokunywa na hupendi kuupa tabu mwili wako.
Katika hali hii utajikuta mwili unaanza kuongezeka, taratibu unanenepa na kunawiri.
Kwa kuwa sasa hutembei kwa mguu umbali mkubwa, ofisini kama ni ghorogani unapanda lifti, au unashuka mlangoni unaingia ofisini au nyumbani.
Chakula unakula kizuri tena vile vitamu, unakuwa bize sana na kazi ukiingia asubuhi unatoka jioni, ukitoka utapata bia kidogo halafu unarudi nyumbani unapumzika hadi kesho tena asubuhi.Hapa unajikuta hata mwisho wa wiki ndipo unaposema ni muda wako wa kumpumzika.  Mapumziko ni kukutana na marafiki, ndugu na jamaa au kukaa na familia na kuburudika.
Mwili unatulia na ku-relax. Hali hii inasababisha hata mzunguko wa damu mwilini unakuwa taratibu, mafuta yanaanza kujikusanya katika mishipa ya damu, moyo na chini ya ngozi, kwa mwanaume unaanza kupata kitambi, shingo nene na mashavu yanaongezeka, ukipima uzito utaonekana unaongezeka.
Mwanamke, unapata pia kitambi, kifua kinaongezeka, mabega na mikono vinaongezeka unene, makalio hasa usawa wa kiuno unaongezeka, uzito pia unaongezeka na mashavu yanajaa. Hali hii sasa tunaita ‘Over weight’ yaani uzito mkubwa na baadaye unakuwa bonge.
DALILI ZA UGONJWA
Ukishafikia hatua hiyo ni kwamba umelimbikiza nishati nyingi mwilini mfumo wa wanga na unashindwa kuutumia, hivyo nishati hiyo inabadilishwa kuwa mafuta.
Baada ya nishati kuwa mafuta ndipo huhifadhiwa mwilini na nyingine katika mishipa ya damu na moyo.
Nishati ikizidi, kongosho ambalo kazi yake kubwa ni kuzalisha ‘Insulin’ inayoyeyusha sukari linazidiwa kutokana na mzigo wa sukari au nishati mwilini kuwa mkubwa ndipo sukari iliyozidi huanza kuzunguka kwenye damu.
Hapa sasa tunasema umeshaanza kuwa mgonjwa na kuanza kuwa na dalili za ugonjwa; unahisi mwili unakuwa mzito, ukipandisha ngazi au mlima mdogo unachoka sana na pumzi zinakuishia, ukikimbia kidogo unaishiwa pumzi na kifua kinauma, baada ya zoezi au pilikapilika fupi unachoka sana na viungo vinauma.
Hapa ni dalili kwamba unaanza kupata matatizo ya mishipa ya damu na misuli ya moyo.
Dalili za kisukari huanza taratibu sana, kwanza utajikuta unapata sana hamu ya kula na unakula sana tena chakula kizuri, ukipitiliza kidogo muda wa kula njaa inauma sana.
Utapata hamu ya kunywa juisi, soda zaidi kuliko maji na hata pombe hamu itaongezeka. Utajiona kabisa kwamba mwili unaongezeka kutokana na nguo kukubana. Muda wa kupumzika utajikuta unapata usingizi mzito.
Ukilala usiku unalala sana na asubuhi unakuwa mzito kuamka, unahisi mwili hauna nguvu, kama ulikunywa pombe unaweza  kuhisi ni pombe, wakati mwingine hata kama hujanywa pombe utahisi jana yake ulikunywa.Wakati mwingine mdomo unakuwa mchungu na mate kujaa mdomoni hadi ukipiga mswaki ndipo unakaa sawa.
Hali inaweza kukaa vibaya na wakati mwingine unajihisi una dalili zote za malaria, unahisi homa, mwili mzito na viungo kulegea, ukienda sehemu zisizokuwa makini utaambiwa una malaria na utakunywa dozi za malaria dawa za kila aina lakini bado.
Utaambiwa una taifodi, hivyohivyo utamaliza dawa zote bila nafuu, utaambiwa una yutiai pia hali itakuwa hivyohivyo, utamaliza dozi zote bila nafuu yoyote.

No comments:

Post a Comment