NA GORDON
KALULUNGA.
UNAWEZA kujiuliza
kwanini waamrishaji wa maandamano hawawaingizi watu barabarani katika matatizo
halisi ya wananchi hata wa chini.
Hakuna
aliyeandamana wala kuamrisha wafuasi wake waandamane kupinga mfumuko wa bei
unaozidi kupanda nchini, matatizo ya dawa hospitalini na ongezeko la dawa
katika maduka binafsi ya dawa.
Wanasiasa
wanawaamrisha watu waandamane kwa malengo yao mahususi ambayo wanaona yana
faida kwa maslahi yao kwanza na kuwawezesha kupata mpenyo wa kushika dola au
kuingia katika serikali ya kitaifa(mchanganyiko wa viongozi wa vyama).
Mwimbaji wa
nyimbo za Injili nchini, Rose Mhando, anao wimbo wake mmoja unaimbwa kuwa (Anacheka..).
anasema Mungu anapoona shetani anashindwa na kuumizwa yeye anacheka.
Nadhani hata
kwa wanaowaamlisha wenzao waingie barabarani na kupewa mkong’oto, nao
wanacheka, kisha wanaita vyombo vya habari kuwa wafuasi wao hawatendewi haki.
Rais Jakaya
Kikwete, nadhani na wewe unapoona watu wazima wanafanya kile ambacho hutarajii
kutoka kwao, unacheka.
Mshauri wako
wa mambo mepesi kwenu watawala lakini ni muhimu kwa wasio na sauti, siku nyingi
sijapaza sauti yangu na kukushauri mambo ambayo washauri wako huko uliko
hawawezi kukueleza kiundani, maana hawana tena uwezo wa kushinda majalalani na
kwenye michezo ya bao.
Katika nyika
unayoiongoza, kitu ambacho ni adimu kukipata ni wataalam wa MSONGO WA MAWAZO (saikolojia).
Afya ya
akili ni muhimu kwa kila mwananchi wa nchi yeyote, lakini hapa nchini, serikali
bado haijalitambua jambo hili muhimu, ndiyo maana linaendelea kuisumbua nchi.
Watalaam wa
saikolojia nchini, wapo vyuoni lakini hawapo kwenye hospitali hata Hospitali ya
Taifa letu (Muhimbili), hatuna.
Baadhi ya wananchi
wanachelewa kulala na wanawahi kwenda makazini, wanamwagiwa maji machafu na
wenye magari, wanakasirika sana.
Wengine
wanaamrishwa sana na wakubwa wao na kunenewa maneno yasiyo na utu, nao hao
huishia kukasirika na kuumwa vichwa na miili yao.
Wanaoenda
hospitali asilimia 60, wengi wao hawaumwi homa kama wanavyoeleza, bali ukweli
ni kwamba wanaumwa akili zao, kutokana na neno(kwanini, kwanini, kwanini),
kutawala akili zao.
Zamani sisi
tunaohusika na masuala ya ushauri, tuliwashauri wafanyakazi na watu wengine
waliopo mijini kuwa, wanapoona kuna matatizo yanawasumbua wawe wanaenda
vijijini kwa Babu na Bibi zao, ambako walikuwa wakipata kupumzika kutokana na
mazingira.
Lakini sasa
jambo hilo halipo kutokana na ugumu wa maisha na kila mmoja kuwa bize(busy),
katika utafutaji.
Wiki hii
baadhi ya walimu waliandamana na kufunga ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri pale
Kigoma, baadhi waligalagala kama watoto, mwingine alisema ameathirika
saikolojia.
Umma uliona,
pamoja na wanafunzi wanaowafundisha. Na mpaka leo hii yule bado hajasema kama
amepona na akili yake kurejea katika hali ya kawaida.
Mtu ambaye
ameathirika kisaikolojia, jambo lolote linapotokea huwa anahisi anaonewa,
kwasababu bado akili yake haijapata afya, lakini siyo (kichaa).
Tabia hii ya
maandamano imeendelea kushika kasi hapa nchini, hili ni sumu mbaya hapo baadae
na sijui kama watawala wetu mnaliona jambo hili kama sisi tuonavyo.(yawezekana
tuonavyo sisi, ndiyo tafsiri mbaya) na ninyi mnacheka.
Wanasiasa
wanaandamana, viongozi wa dini na wafuasi wao, wanafunzi, waandishi wa habari
na walimu (jamii nzima sasa inaandamana).
Ni dalili
mbaya kwa taifa. Nalisema jambo hili chini ya mwamvuli wa kiapo cha Chama Cha
Mapinduzi(CCM) kisemacho (Nitasema ukweli daima fitina kwangu ni mwiko).
Watu wa
nyikani wanaona chimbuko la tatizo hili la maandamano kuwa linatokana na
watawala kutokuwa na vipaumbele, kama vipo basi havitekelezwi na
kinachotekelezeka ni mambo ya dharula.
Moja ya
mambo ya dharula ambayo hata wenyewe(watawala), hamkujiandaa, ni suala la
Mabadiliko ya Katiba, ambalo halimo hata kwenye ilani ya chama kinachotawala.
Jambo hili nalo linaonesha ni jinsi gani taifa limekumbwa na tatizo la saikolojia.
Suala la
walimu kudai malimbikizo na kuendelea kukatwa asilimia mbili za mishahara bila
idhini yao na kinachoitwa Chama cha walimu Tanzania(CWT), halijaanza leo,
lakini serikali inaonesha kutoshindwa, bali kutosimamia vema kwa nia thabiti ya
kumaliza tatizo, kutokana na kuwa na mambo mengi ambayo nayo hayaishi bali
yanaguswa.
Suala la
(mabwana/mabibi) shamba kutokuwepo kwenye vituo vyao vya kazi, halina majibu
sawasawa.
Suala la
Afya, hususani wajawazito kujifungua (bure) na utoshelevu wa wahudumu wenye
sifa na vitendanishi, nalo linatekelezwa kwa kuguswa.
Suala la
Polisi kuwa na makazi yasiyo na utu na hadhi yao, bado haliishi.
Wakandarasi
kwa sasa wamefikia hatua ya kucheza na akili za watu, wanaanza kukarabati
barabara nyakati za mvua kwasababu wanajua zitabomoka kirahisi na watasema mvua
zilikuwa nyingi.
Wanafanya
hivyo kwa makusudi, maana watoa tenda na waandaaji wa miradi hiyo nao wanataka
(Ten Percent).
Siyo kwamba
ninabeza jitihada zote zinazofanywa na serikali, la hasha, bali nataka kama
nchi, tushughulikie jambo moja mpaka tunamaliza kuliko kuwa na mambo mengi
ambayo yote tunaishia kuyagusa badala ya kuyatekeleza.
Tunawasikia
watawala mnasema kuwa, Tanzania tunataka tuwe sawa na wenzetu!
Sisi
tunajiuliza, tuwe sawa na wenzetu akina nani? Wa wapi? Katika mipango ipi
inayotekelezeka? Watumishi wepi wenye lengo moja la kutufikisha huko ambako
hatukujui?
Si jambo
jema kulitabiri, lakini ni vema tukalisema kuwa ipo siku hata hawa wanaotawanya
maandamano nao wataandamana kutokana na makazi yao yalivyo, huku wakiona
watawala wanatapanya fedha hata katika mambo ambayo hayamo kwenye ilani ya
vyama vyao na hata yangeachwa yasingekuwa na athari na mwisho fedha hizo
zingeweza hata kuezeka nyumba 100 za makazi yao.
Kumbuka
hakuna kibaya kisicho na uzuri, tibu saikolojia za unaowatawala, nchi
itatawalika.
Rais
Kikwete, karibu sana huku kwetu nyikani, kama ujuavyo, unapotaka kuendelea
kunisikiliza zaidi, mimi mshauri wako wa mambo yasiyo na maana sana kwa
watawala, ndipo huwa namaliza kuipaza sauti kutoka hapa nyikani.
Mwandishi wa makala haya, anapatikana kwa simu 0754 440749 au barua pepe; kalulunga2006@gmail.com
No comments:
Post a Comment