Harufu mbaya ni kitu kisichompendeza mtu yeyote.
Unapotoa harufu mbaya toka mwilini mwako, haikupendezi wewe mwenyewe
wala mtu wa jirani. Kama kitu hukipendi wewe na ukakiona hakifai basi
usimlazimishe mwenzio akipende au akione cha kawaida.
Harufu mbaya mwilini inatoka maeneo yote ya mwili kuanzia kichwani hadi miguuni.
Zipo sababu nyingi zinazomfanya mtu atokwe na harufu mbaya, inaweza kuwa uchafu, maradhi au maumbile.
Hali ya uchafu ipo wazi endapo mtu haogi, hafui au hanawi. Uchafu wa
kichwani inaweza kuwa nywele au wigi au kitu chochote kinachowekwa
kichwani.Uchafu unaweza kuwa maeneo mbalimbali ya mwili.
Maradhi ya
ngozi, kansa au vidonda vyenye maambukizi vinaweza kusababisha kutoa
harufu mbaya au vitambaa vilivyofungiwa vidonda.
Kwa hiyo kundi la maradhi ni pana kwa kuwa tatizo la ngozi pekee linaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa.
Sababu za kimaumbile linawahusu zaidi watu wanene ingawa hata wembamba
pia wanaweza kupatwa na tatizo hili kutegemea na harufu inatoka eneo
gani la mwili.
Watu wanene hupatwa na matatizo ya kutoa harufu mbaya kama
hawatazidisha usafi na kuhakikisha miili yao sehemu za mikunjo inakuwa
mikavu. Sehemu hizo ni chini ya kifua au matiti, nyama za tumboni, chini
ya tumbo, mbavuni, sehemu za siri na mapajani.
Unene pamoja na matatizo mengi yanayoweza kujitokeza pia huweza
kusababisha magonjwa ya ngozi na kutokwa na jasho lenye harufu kali.
MAENEO YANAYOTOA HARUFU MBAYA
Sehemu yoyote ya mwili inaweza
kutoa harufu mbaya kama tulivyoona hapo mwanzoni kuanzia kichwani hadi
miguuni. Lakini yapo maeneo kama masikioni na puani pia harufu mbaya
hutoka. Harufu za maeneo hayo mara nyingi haziwi kali.
KUTOKWA HARUFU MBAYA KINYWANI
Tatizo la kutokwa na harufu mbaya mdomoni au kinywani hutokana na
matatizo mbalimbali kama kuwa na meno mabovu, magonjwa ya fizi, ulimi,
fangasi za kinywani na uchafu kutokana na kutosafisha kinywa vizuri.
Wapo watu ambao kwa asili hutoa harufu mbaya kinywani pasipo kuwa na
magonjwa ya kinywa na huwa makini kusafisha kinywa, lakini harufu
haiishi.
Tatizo hili hutibika baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina katika tabaka linalotandika ndani ya kinywa.
Wakati mwingine harufu mbaya ya kinywa husababishwa na ulaji wa vyakula, unywaji pombe, uvutaji wa sigara, bangi na ugoro.
KUTOKWA NA HARUFU MBAYA KWAPANI
Kutokwa na harufu mbaya kwapani
au kunuka kikwapa inatokana na mambo mbalimbali hata kama unajisafisha
mara kwa mara na kutoa vinyweleo vya kwapani.
Harufu ya kikwapa husababishwa na njia ambazo ngozi ya kwapani
hupumua zinaziba, hivyo kusababisha njia za kutolea jasho kuwa chache na
jasho kutoka kidogo kidogo na kujaa kwapani.
Hivyo kujaa na
kulowesha nguo sehemu hizo, hali hii ikiendelea kwa muda mrefu
husababisha bakteria aina ya ‘staphylloccocus’ kuanza kuishi hapo na
jasho linalojirundika kukauka na kuganda, hivyo kutoa harufu mbaya.
Tatizo la kikwapa likiendelea kwa muda mrefu baadhi ya njia za jasho
huziba kabisa na bakteria kujipenyeza. Hapo ndipo unaweza kusumbuliwa na
majipu ya mara kwa mara kwapani, kutokwa na vipele vikubwa kwapani na
muwasho mkali baada ya kunyoa kwapani na hata vidonda vidogovidogo.
Matumizi ya baadhi ya pafyumu husababisha mzio ambapo kwapa litawasha
sana kila wakati au utatokwa na vipele vingi au ngozi ya kwapani
inabadilika na kuwa nyeusi sana huku ikitoka harufu mbaya. Tatizo hili
linaweza kutibika hospitali.
HARUFU MBAYA SEHEMU ZA SIRI
Harufu mbaya sehemu za siri inaweza
kuwa kwa wanaume na wanawake. Zipo sababu mbalimbali kwa wanaume ambazo
zinahitaji uchunguzi wa kina na tiba.
Kwa wanawake harufu inaweza kutoka ukeni ikiambatana na uchafu au la.
Harufu ya ukeni huwa mbaya inayofanana na shombo la samaki hutokana na
kutokuwa makini kiusafi.
Maambukizi ya fangasi na bakteria, magonjwa ya zinaa, kisonono na kaswende ni sababu mojawapo.
Wapo wanawake ambao hutokwa na harufu sehemu za siri kutokana na
mikunjo ya kwenye mapaja yao, hasa kwa wale wanene. Harufu pia inaweza
kutoka katika sehemu ya haja kubwa na hii ni ya kinyesi endapo hutanawa
vizuri au kuwa na maradhi sehemu hiyo.
NINI CHA KUFANYA?
Endapo utakuwa na tatizo hili la kutoa harufu
mbaya maeneo tofauti ya mwili au unahisi mwenzio ana tatizo hili na
anakukwaza, inashauriwa uwaone madaktari katika hospitali za wilaya kwa
uchunguzi wa kina.
Tatizo hili linatibika na hupotea kabisa na kukuacha huru. Tatizo la
kutokwa na majipu, vipele, kubadilika rangi ya ngozi kwapani, chini ya
matiti na sehemu za siri, pia linatibika kabisa endapo utawaona
wataalamu. Wahi mapema hospitali.
No comments:
Post a Comment