NIJumanne tena, safu hii ya maisha na mapenzi ipo kukuelimisha na kukupa maujuzi ili ikibidi siku moja msomaji wangu ubadilike.
Wiki iliyopita tulimalizia mada yetu ya; Unaachana naye unachukua
kila kitu ulichomnunulia. Wiki hii tuna mada nyingine ndiyo hiyo hapo
juu; mwanamke na mwanaume katika uhusiano nani anaongoza kwa kutoa siri
nje? Au kufanya umbeya.
Nilibahatika kuzungumza na jinsia zote
kuhusu mada yetu wakati naiandaa, hoja ilikuwa nusu kwa nusu, yaani
ilionekana kama wote tu na si suala la jinsia.
WASEMAVYO WANAWAKE
Nilibaini kuwa baadhi ya watu walizungumza na mimi kwa utetezi huku
wakiwa na ukweli mwingine moyoni, lakini pia nilijifunza kitu cha ziada
kwamba, kumbe baadhi ya wanawake wenyewe wana majibu ya wazi.
Mama Piliani, mkazi wa Sinza-Palestina jijini Dar, yeye alisema kwa
kawaida, mwanamke anamudu kutoa siri za ndani wakati wote, akiwa na
furaha na akiwa na hasira lakini mwanaume mara nyingi hufanya hivyo pale
anapokuwa na hasira ya jambo fulani.
“Mwanamke akiwa na hasira anamwambia shoga yake; ‘mimi huyu mwanaume
wangu nadhani amenishinda sasa. Nikitaka tendo la ndoa anakuwa mvivu,
hawezi, sijui nitoke nje, eti unanishauri vipi?’
“Akiwa na furaha
atamwambia shoga yake; ‘yaani mwanaume wangu nampenda sana, kitandani
yuko vizuri, ukikutana naye leo, unaweza kukaa hata wiki maana anakuwa
amekata kiu yote.’
WANAUME WAO
Utafiti nilioufanya nilibaini kuwa, wanaume wengi
hutoa sira za uhusiano pale tu wanapohitaji ushauri wa masuala magumu
yanayowatokea. Lakini pia wapo baadhi ya wanaume nao wanapenda sana
‘ubuyu’ hivyo huanika siri zao za uhusiano bila kutaka ushauri.
ETI NI TIBA
“Mimi siwezi kumficha rafiki yangu kipenzi kuhusu
magumu yanayonitokea ndani ya uhusiano. Unajua kusema pia ni tiba tosha.
Kama wewe huna tabia ya kuficha mambo magumu unaweza kuja kufa kwa
presha,” alisema Tamimu, mkazi wa Tandale Kwatumbo, Dar.
Kauli ya Tamimu iliungwa mkono na mkewe aliyekuwa naye kwenye Kituo cha Daladala cha Kwaremi, Dar wakisubiri usafiri.
Mke huyo alisema: “Unajua hata mtoto, akitendewa ubaya asipolia
anapata tabu sana, lakini akilia anakuwa sawa. Ndiyo umbeya pia, kama
una magumu katika uhusiano halafu huwaambii wenzako utapata tabu, watu
watakushangaa kukuona unakonda tu, lakini ukisema unapata nafuu.”
Kuhusu kutoa sifa ya mambo mema, mke huyo alisema: “Huo sasa ni
uendawazimu. Unamwambia shoga yako kuhusu mumeo anavyokutosheleza
kitandani si ndiyo mwanzo wa kuibiwa!”
KITABIA
Kwa mujibu wa wataalam wa mambo ya tabia za binadamu,
mwanamke kwa siku anazungumza maneno 20,000 na kumzidi mwanaume kwa
maneno 13,000. Ina maana mwanaume anazungumza maneno 7,000 tu kwa siku!
Wataalam hao wanatanabaisha kwamba, tabia hiyo ndiyo inayomfanya
mwanamke kuongoza katika kutoa siri za uhusiano kuliko mwanaume kwa vile
wanaongea sana.
Wataalam hao wanakwenda mbele zaidi kwa kusema, umbeya au kutoa siri
za uhusiano kwa mwanamke ni jambo la asili ndiyo maana watoto wa kike
huanza kutangulia kuongea kuliko wa kiume ambaye yeye huwa mwepesi
kwenye kuanza kutembea.
Baadhi ya wanawake wanalijua hilo ndiyo maana unaweza kumsikia
mwanamke akisema: “We mwanaume mzima unakuwa mbeya kama mwanamke
bwana.”Kuthibitisha hilo, vuta kumbukumbu kama kuna siku ulikuta ugomvi
kati ya mwanamke na mwanaume, nani alishindwa kwa sababu ya kusema sana,
lazima mwanaume alishindwa!
MADHARA
Si vibaya kwa mtu kuanika mabaya anayokumbana nayo kwenye
uhusiano lakini ni vyema kufaya hivyo kwa nia ya kusaka suluhu na si
kumsema mwenzako kwa lengo la kumwanika, madhara yake marafiki
unaowaambia nao watawaambia wengine na wengine, na mwenzio atakuwa mtu
wa kudharauliwa kwa sababu udhaifu wake utajulikana.
Ni vyema kama mwenzako katika uhusiano ana udhaifu, umsitiri kwani
wewe ndiyo mwenzake. Kama udhaifu wake ni wenye kukera na kutokuvumilika
nenda kwa viongozi wa dini au wazazi ili suala liwe ni shauri lenye
kutatuliwa kwa hekima.
No comments:
Post a Comment