Wednesday, 1 October 2014

Washiriki Shindano la Mashujaa wa Kesho Waanza Kurejesha Fomu

Chumba cha kompyuta cha washiriki wa Shindano la Mashujaa wa Kesho. Chumba cha kompyuta cha washiriki wa Shindano la Mashujaa wa Kesho
Baadhi ya washiriki wa Shindano la Mashujaa wa Kesho wakipitia fomu zao. Baadhi ya washiriki wa Shindano la Mashujaa wa Kesho wakipitia fomu zao.

 Na Mwandishi Wetu

  ZOEZI la uchukuaji fomu kwa ajili ya vijana mbalimbali kushiriki katika Shindano la Mashujaa wa Kesho la Statoil limeendelea kushika kasi huku idadi kubwa ya vijana wakiendelea kurejesha fomu kwa lengo la kushiriki katika kinyang’anyiro hicho. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Ofisa Mawasiliano wa Statoil Tanzania, Erick Mchome alisema hadi sasa zaidi ya vijana 150 wamerejesha fomu zao tayari kwa kuyashindanisha mawazo anuai ya miradi yao walioiwasilisha kwa ajili ya kushiriki katika shindano hilo. Mchome alisema vijana hao wamejaza fomu kwa ajili ya kushiriki katika shindano hilo kuwania kitita cha hadi Dola 5,000 kwa mshindi wa kwanza. “Kimsingi zoezi hili la shindano la Mashujaa wa Kesho limepokelewa vizuri na linaendelea vizuri sana vijana wengi wa Mtwara wamejitokeza kuchukua fomu na baadhi wameanza kuzirejesha fomu zao…zaidi ya vijana 150 tayari wamerejesha fomu,” alisema Mchome. Hata hivyo kiongozi huyo aliwataka vijana ambao wamechukua fomu kuzirejesha fomu zao kwa wakati kwenye vituo walivyoelekezwa ili hatua zingine za utaratibu wa shindano hilo ziweze kuendelea. “Ningependa kuwakumbusha washiriki kuwa mwisho wa kurejesha fomu ni Oktoba 10, 2014 saa nane kamili kwenye vyuo vya Naliendele Agricultural Institute, Tanzania Institute of Accountancy, VETA, Chuo cha Utumishi na Chuo cha Stella Maris Pamoja na Pride FM,” alisisitiza Mchome. Akifafanua zaidi, Mchome alisema mchujo wa kupata washiriki 40 watakaoingia hatua ya pili utafanyika mara baada ya zoezi la urejeshwaji fomu kukamilika na kutakuwa na mchujo wa tatu ambao ni wa mwisho na kuwatoa washindi watano watakao wania dola 5,000 kwa mshindi wa kwanza na dola 1,000 kwa wa shindi wa pili, tatu, nne na tano . Shindano hilo la vijana linalojulikana kama Mashujaa wa Kesho lenye lengo la kuhamasisha ujasiriamali lilizinduliwa rasmi Septemba 3, 2014 na kampuni ya Statoil na linatarajiwa kumalizika Desemba 12 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment