Wednesday, 1 October 2014

KAZI SAWA, LAKINI MUMEO KILA KITU

He he he heeee, acha nicheke miye mwana Kibatari mjukuu ya Kandili, unajua vitu vingine vinachekesha kama si kusikitisha, unalalamika mwanamke mzima uliyekamilika tena bila aibu eti mfanyakazi wako wa ndani anakulia mali zako kwa mumeo kuhamishia mapenzi kwake.
Unajua kauli hiyo hunifanya nikumbuke ile kauli isemayo mpambe awe mwenye mali na mwenye mali aonekane mpambe. Ooh, nilikuja na kasi ya ajabu. Na miye bila salamu kwa kuwahi kuzima moto ambao sasa hivi umetanda kila kona ya nyumba zetu, hasa wafanyakazi ambao wameolewa na wao kumweka hausigeli.
Kwa kuwa na mfanyakazi wa ndani, basi kila kitu unamuachia, akifanya ambacho ni makosa kwa mwanamke aliyefundwa akafundika kumuacha hausigeli amfanyie mumeo kazi zinazokuhusu.
Tokea lini Fisi akaachiwa bucha, wewe na mfanyakazi  wako wa ndani mnazidiana nini kimaumbile, pengine mfanyakazi wako Mungu kampendelea kuliko wewe. Kwa vile unafanya kazi basi ukirudi unautupa mkoba wako unakwenda kuoga ukila unapanda kitandani kutokana na uchovu wa kutwa nzima!
Unamwacha mfanyakazi wa ndani afanye kazi zote, kumsubiri mumeo wewe umelala akirudi amtengee maji ya kuoga wewe umelala, amtengee  chakula huna habari unajigeuza kitandani.
Anaondoa vyombo pengine amevaa upande wa kanga bila kitu ndani, na kama anajua yupo katika mkao wa kula naye hufanya vibweka vya kuchezesha makalio, kuacha matiti nje.Sehemu hizo ndizo huwatoa imani wanaume na kujikuta wakijaribu kwa vile naye ana hamu zake, basi shoga wee unalala watu wanajilia vyao. Ulikuwa wa kuamshwa usiku.
“Honey leo nimeshikwa mwenzio.”
Unajikuta unalala kila siku bila kuguswa kutokana na uchovu wa kazi unaona sawa, kumbe nyani kaingia shambani wee wapiga usingizi mali zako zinaliwa.Leo na kesho mfanyakazi wako wa ndani anageuka mke mwenzio tena mapenzi yote mumeo anayahamishia kwake kwa vile ndiye anayemfanyia zaidi ya mke.
Utakalia kulia “Aah, nyani kavamia shamba langu naanza kuvuna mabua,” we mwenyewe umemchekea unategemea nini.Shoga nataka nikueleze sheria za ndoa, hata kama unafanya kazi gani hakikisha baadhi ya vitu hasa vimuhusuvyo mumeo, mfanyakazi wa ndani havigusi. Kufuliwa nguo, kutengewa maji ya kuoga, kula, lazima ale mumeo ukiwa pembeni hata kama umeshiba basi mlishane hata tonge mbili.
Mumeo ni lulu isiyotaka kuguswa na mtu, itunze kwa nguvu zako zote, hakikisha hakuna mtu atakayeigusa hata shoga yako ila wewe mwenyewe. Mfanyakazi ana mipaka yake wala asiwe na mazoea ya kuvuka mipaka na mumeo.
Narudia, wewe na mfanyakazi hampishani kitu, kila ulichonacho anacho, naye ana matamanio vilevile, anataka vitu vizuri. Kufanya kazi usijisahau na kuona kazi ni bora kuliko mumeo, kazi ina umuhimu kwa sehemu zake na ukifika nyumbani mwenye nafasi ya pekee ni mumeo kuhakikisha anapata huduma zote muhimu.
Kinachowaumiza wanawake wengi ni uvivu, kwa sababu wanafanya kazi wanaamua kumuachia fisi bucha.Usije kushangaa kukuta amekula hadi gogo la kupasulia mifupa. Yangu nimemaliza, la muhimu kuyafanyia kazi la sivyo utaachika na nyumba unaipenda.

Ni mimi anti Nasra, Shangingi Mstaafu.

No comments:

Post a Comment