Wednesday 1 October 2014

SAWA UMZURI, LAKINI UNAJISIKIAJE UNAPOITWA JINA LA ‘CHA WOTE’?

Niwiki nyingine tena tunakutana kupitia safu hii nikiamini kwamba umzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida.
Mimi niko poa na kama ilivyo ada leo nimekuja na mada ambayo inawagusa wanawake kwa asilimia kubwa. Nazungumzia hii tabia ya baadhi ya wasichana kutumia uzuri wao vibaya kwa kuwapanga foleni wanaume bila kujali madhara yanayoweza kujitokeza.Wewe msomaji wangu utakuwa ni shahidi juu ya uwepo wa wasichana ambao hawawezi kusema ‘no’ pale wanapotamkiwa masuala ya mapenzi.
Katika uchunguzi wangu mdogo, wapo wasichana ambao wameridhika na maisha ya kutokuwa na mwanaume ‘pamanenti’, wao imekuwa ni fasheni kubadili wanaume kama nguo.
Ninapozungumzia wanawake wa sampuli hii, simaanishi machangudoa. Nawazungumzia wale ambao wanafanya kazi zao au wako mtaani lakini hawajabahatika kuwa na wanaume wa kuwashika.
Sasa kutokana na hisia zao za kimapenzi, anayetokea mbele yao ni halali yao na mapenzi yao huwa hayadumu. Unamkuta msichana mzuri mwenye kila sifa ya kuwa na mpenzi wake lakini yupoyupo tu.
Leo katembea na huyu, kesho na yule na wakati mwingine ni kwamba si tamaa ya pesa, ni tamaa ya mwili au kutafuta tu sifa kuwa katembea na flani. Hii ni sawa kweli?
Unajisikiaje pale unapopachikwa jina la cha wote mtaani kwenu au eneo lako la kazi? Hata kama hawakuiti hivyo, huoni unajivunjia heshima kwa kuwa na uhusiano na wanaume tofauti ndani ya kipindi kifupi tena baadhi yao wakiwa ni marafiki?
Nyie ambao mnajirahisi kwa wanaume mjue mnachoreka sana na mnaonekana msiyoithamini miili yenu.
Matokeo yake sasa watu wanapasiana kama mpira kwenye eneo la 18. Leo unatembea na Shabani, akikuchoka anamsukumia mshikaji wake John na wewe unakubali kirahisi.
Huku ni kujirahisi kulikopitiliza.
Ni sawa unaweza kuwa na sura na umbile zuri linaloweza kukufanya kila unapopita ukatongozwa. Hiyo inatakiwa kuwa changamoto kwako na siku zote simamia utu wako.
Kwa jinsi ulivyo, unatakiwa kuwa na mpenzi kama siyo mume, mtu ambaye anakupenda kwa dhati na aliyetayari kuchukua nafasi yake kama mpenzi. Mtu ambaye atakupa furaha, atakulinda, atakushauri kuhusu maisha na kukusaidia pale ambapo utahitaji msaada wake.
Usipokuwa na mtu ‘pamanenti’, hayo huwezi kuyapata. Utayapataje wakati uliyenaye anataka akuonje kisha kesho atafute sababu akutose na kuhamia kwa mwingine?Nadhani ifike wakati kama ni msichana ambaye unastahili kuwa na mpenzi, utulie na uchague mtu mmoja ambaye utampa dhamana ya maisha yako. Chukua muda kuwa peke yako kwa kipindi flani lakini siku moja amini utampata mtu atakayekulindia heshima yako.Kwa ulimwengu wa sasa siyo sifa kuwa na msururu wa wanaume. Hivi unadhani ni sifa kuwa umetembea na wanaume kibao katika eneo lako la kazi? Hivi unajisikiaje unapokuwa msichana ambaye umetembea na idadi kubwa ya wanaume katika mtaa wenu?
Ukweli ni kwamba kila utakapopita utakuwa kama hujavaa nguo na ujue wanaume zaidi ya mmoja ambao wametembea na wewe wakikutana na kugundua wote wamekupitia, watakushusha thamani na watakuwa wa kwanza kukuponda kwa wengine kwamba wewe ni kicheche.
Ifike wakati ujitambue na ujue thamani yako. Uzuri wako hautakuwa na faida yoyote kama kila anayekuambia vipi unamwambia poa! Unamjibu poa, dhamira yake unaijua? Unadhani ukishamuonjesha mara moja ndiyo atakuwa na wewe?
Kama ulikuwa hujui, wanaume wengi sasa hivi wanakwepa sana kuwa na wasichana wazuri. Wanahisi kutakuwa na ugumu katika kuwatuliza kwani wanaume kibao watawatolea macho. Lakini sasa shangaa, wanaume wengi wanajisikia ujiko sana kuwapitia wasichana wazuri. Yaani wanajiona ni wajanja kutongoza na kukubaliwa na akina dada warembo.
Ndiyo maana nasema, usipowajulia hawa watakufanya kama vile mpira wa kona kisha watakuacha na makovu ya aibu na usipate wa kukuoa. Kama atatokea lazima atakuwa ni mtu wa mbali asiyejua nyendo zako, kwa nini ujiwekee historia mbaya?
Tukubali kwamba kuna wakati tunakosea na tubadilike. Hapo ulipo jiulize ni wanaume wangapi ambao umewapa nafasi waujue mwili wako kirahisi? Huoni aibu? Badilika wewe, acha ushamba!

No comments:

Post a Comment