MBOWE: ANAYETAKA KUPIMA KIFUA NA MIMI AJE CHADEMA
Friday, August 29, 2014
Mwenyekiti wa Chadema, Freman Mbowe akisoma fomu ya kugombea uenyekiti wa chama hicho baada ya kukabidhiwa na mwakilishi wa wazee wa Mkoa wa Kigoma, Athumani Mzigo
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe jana alikabidhiwa fomu na makada wa chama hicho na kumtaka awanie tena kiti hicho, ombi ambalo alilikubali na kufungua milango kwa wanachama wengine ‘kupimana naye kifua’.
“Nafasi bado ipo, anayetaka kupima kifua na mimi ajitokeze. Tena nawaomba viongozi wangu msizuie fomu kwa anayetaka,” alisema Mbowe ambaye ameongoza chama hicho kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano.
Makada wa chama hicho kutoka maeneo mbalimbali nchini wakiongozwa na kada maarufu, Athuman Mzigo (Mapigo Saba) kutoka Kigoma, walikutana na Mbowe na kuwasilisha maombi yao ya kumtaka awanie tena nafasi hiyo.
“Kutokana na sifa za mwenyekiti wetu, tumechangishana Sh200 kila mmoja hadi zikafika Sh50,000,” alisema Mapigo Saba huku akishangiliwa na makada wenzake alioambatana nao na kuongeza:
“Tumemwomba mwenyekiti agombee nafasi hiyo kwa kuzingatia sifa; kwanza anaijua vizuri idadi ya Watanzania na matatizo yao, pili anaungwa mkono na watu wengi na amekisaidia chama kukua. Tulikuwa na madiwani 40 leo wamefika 500, wabunge watano leo 48. Halafu hana ubaguzi ndiyo maana ameunganisha vyama vya upinzani na kuunda Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi).”
Huku akichomekea maneno ya lugha ya Kiha, Mapigo Saba alisema kuwa maombi ya kumtaka Mbowe agombee pia yametolewa katika mikoa ya Rukwa, Manyara, Iringa, Njombe, Jimbo la Same Magharibi, Zanzibar, Mwanza na Kilimanjaro.
Hotuba ya Mapigo Saba ilifuatiwa na salamu kutoka kwa wazee wa wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke, Baraza la Wanawake (Bawacha) na Baraza la Vijana (Bavicha).
Akitoa salamu za Bavicha, mwenyekiti wa baraza hilo Njombe, Emmanuel Masonga alisema Mbowe ni sawa na Joshua aliyemalizia kuwaongoza wana wa Israel kuingia nchi ya Kanaani:
“Sisi Wakristo tunajua kuwa Mussa alianzisha safari ya Waisrael kwenda Kanaani, ila hakuwafikisha. Kina Mtei (Edwin), Kimesera (Victor), Bob Makani na wengineo walianzisha safari ya kwenda Ikulu, ila hawakutufikisha. Mbowe ni sawa na Joshua atakayetufikisha Ikulu,” alisema Masonga.
Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Susan Lymo alimsifu Mbowe akisema ameongeza hamasa ya wanawake kushiriki siasa katika chama hicho.
“Mwaka 2000, kulikuwa na mwanamke mmoja katika viti maalumu, mwaka 2005 waliongezeka na kufikia sita na mwaka 2010 wamefikia 26. Mwenyekiti pia ameufanya mwaka huu kuwa wa wanawake kitaifa na ameongeza hamasa ya wanawake kushiriki siasa,” alisema Lymo.
Mbali na viongozi wa chama, alikuwapo pia Sheikh Rajab Katimba kutoka Jumuiya na Taasisi za Kiislamu ambaye alimsifu Mbowe na kuomba agombee tena nafasi hiyo
Mbowe akubali
Baada ya Mratibu wa Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), Nickson Tugara kummwagia sifa Mbowe, Mapigo Saba alimkabidhi fomu, huku makada wakiimba, ‘Jembe, jembe, jembe…”
Mbowe aliishukuru Kamati Kuu ya chama hicho kwa kupanga uchaguzi Septemba 14, mwaka huu ambayo ni siku yake ya kuzaliwa huku akiahidi kujenga chama imara.
“Mtaiona Chadema mpya ifikapo Septemba 14. Hiki chama hakitakufa na hatutamvumilia mtu yeyote wa kabila lolote atakayekivuruga,” alisema.
Mbowe alisema hajawahi kuomba kugombea uenyekiti wa chama hicho tangu aliponza mwaka 2000... “Napata wakati mgumu ninapofikia wakati huu.
Chadema ina watu mbalimbali wenye taaluma na uzoefu, kwa nini mimi? Makundi haya yaliyojitokeza kunichukulia fomu yanaweza kutafsiriwa na wapenda majungu kuwa nimepanga mimi.
“Leo ni mara ya tatu naombwa kugombea uenyekiti, sijawahi kuomba. Mwaka 2004, Mzee Makani aliniomba nikamkatalia, lakini akaunda kikundi cha wazee walionichukulia fomu.
Mwaka 2005, chama hakikuwa na mgombea urais, awali alijitokeza Profesa Mwesiga Baregu lakini akajitoa, nikaambiwa nibebe mzigo. Mwaka 2009 nikaombwa tena kugombea.”
Alisema amedhamiria kujenga chama kimtandao na kimfumo ili kuondokana na mfumo wa kienyeji... “Huko nyuma wakati wa uchaguzi watu walipeana tu nyadhifa kiundugu tukadhani chama kimeongezeka. Lakini wakati huu uchaguzi umefanyika kwa miezi tisa.
Tulisema hatuwezi kufanya uchaguzi wa Taifa bila kupata viongozi wa mkoa, wilaya, kata, kijiji na mtaa, kitongoji na shina.
Tumefanya uchaguzi, watu wamepima na kuona mambo magumu, mara unasikia wanakimbia wakisema wameacha uenyekiti, uache wakati chama kinakua?”
Chanzo;Mwananchi
No comments:
Post a Comment